Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Meneja adai MultiChoice ilimkosesha Ditto Sh1.8 bilioni

Mwanamuziki, Lameck Ditto (mwenye kofia) akiingia kwenye chumba (court) cha Mahakama Kuu kanda ya Dar es Salaam sanjari na mawakili wake, Elizabeth John na Ally Hamza na meneja wake, Rodney Rugambo (mwenye fulana nyeupe). Picha na Imani Makongoro

Muktasari:

  • Ditto alifungua kesi hiyo akidai fidia ya jumla ya Sh6.2 bilioni kwa madai ya kutumia wimbo wake kibiashara, wakati wa kampeni za fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) ya mwaka 2019 bila makubaliano au ridhaa yake.

Dar es Salaam. Rodney Rugambo ambaye ni meneja wa mwanamuziki Lameck Ditto ameieleza Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam kuwa mwanamuziki huyo alikosa mapato ya Sh1.8 bilioni, baada ya wimbo wake wa ‘Nchi Yangu’ kutumiwa na Kampuni ya Multchoice Tanzania Limited katika matangazo yake ya biashara.

Rodney amebainisha hayo leo Machi 23, 2024, wakati akitoa ushahidi katika kesi ya madai iliyofunguliwa na mwanamuziki huyo dhidi ya Kampuni ya MultiChoice Tanzania Limited, maarufu kama DSTV, inayosikilizwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Salma Maghimbi.

Ditto alifungua kesi hiyo akidai fidia ya jumla ya Sh6.2 bilioni kwa madai ya kutumia wimbo wake kibiashara, wakati wa kampeni za fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) ya mwaka 2019 bila makubaliano au ridhaa yake.

Katika ushahidi wake Rodney, aliieleza Mahakama hiyo kuwa amekuwa meneja wa mwanamuziki huyo tangu mwaka 2016, amedai kuwa mwanamuziki huyo aliandika wimbo huo mwaka 2017, akilenga kuutumia kama nembo (brand) kwenye kampeni ya Kibanda umiza.

"Wimbo ulipotengenezwa, tulikuwa na mpango wa kuutumia kwenye kampeni ya Kibanda umiza," amesema, Rodney, ambaye ni shahidi wa nne katika kesi hiyo.

Akiongozwa na Wakili wa Ditto, Ally Hamza, Rodney amedai kuwa kwenye kampeni hiyo, katika kipindi cha miaka mitano, Ditto angelipwa Sh1.8 bilioni.

Amedai kuwa kabla ya kuanza kwa kampeni hiyo, waratibu wa Tamasha la Urithi, waliuomba kuutumia kwenye tamasha hilo. "Kwenye tamasha la urithi wimbo huo haukutumika kibiashara."

Tukiwa tunaendelea na mchakato wa kuutumia kwenye kampeni ya Kibanda umiza,  tulishangaa kuona DSTV (Kampuni ya MultiChoice Tanzania Limited) wameutumia kwenye matangazo yao ya kibiashara," ameeleza meneja huyo.

Amedai kuwa jambo hilo lilimuathiri Ditto kwa kuwa  hakuweza kuendelea kwenye kampeni ya Kibanda Umiza.

"Wimbo wa ‘Nchi Yangu’ haukutumiwa tena kwenye kampeni ile na yeye (Ditto) kushindwa kuendelea na mkataba ule, kwani tayari  ulishatumika kibiashara na kampuni nyingine hivyo thamani yake kushuka," amesema Rodney.

Baada ya kutoa ushahidi wake, mawakili wa MultiChoice Thomas Mathias na Lyimo walimuuliza maswali kadhaa shahidi huyo, ikiwamo endapo anafahamu kuhusu mashindano ya Afcon, lakini akajibu kuwa hajui chochote kuhusu mpira wa miguu.

Katika kesi hiyo Ditto ambaye jina lake halisi ni Dotto Bernard Bwakeya amedai kuwa kampuni hiyo imemnyima fursa ya kunufaika na wimbo huo anaodai ni kazi yake, kwa kuutumia kwenye matangazo yao ya biashara bila ridhaa yake.

Hivyo ameiomba Mahakama hiyo iamuru kampuni hiyo  imlipe Sh6.2 bilioni,  kama fidia ya hasara ya kukosa kipato.

Pia anaiomba Mahakama iamuru alipwe Sh200 milioni ikiwa ni fidia ya madhara ya jumla,  riba ya asilimia 25 tangu siku alipofungua kesi hiyo.

Kesi hiyo itaendelea tena Jumatatu, Machi 25, 2024a ambapo shahidi wa tano upande wa madai anatarajiwa  kutoa ushahidi wake.