Meya Moshi akana kushirikiana na Sabaya

Meya Moshi akana kushirikiana na Sabaya

Muktasari:

  • Wakati aliyekuwa mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya akitarajiwa kufikishwa mahakamani kwa mara ya pili leo, Meya wa Manispaa ya Moshi, Juma Raibu aliyetajwa kuchunguzwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) katika tuhuma kuwa alishirikiana na Sabaya katika uhalifu,  amekana kuhusika.

Dar es Salaam. Wakati aliyekuwa mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya akitarajiwa kufikishwa mahakamani kwa mara ya pili leo, Meya wa Manispaa ya Moshi, Juma Raibu aliyetajwa kuchunguzwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) katika tuhuma kuwa alishirikiana na Sabaya katika uhalifu,  amekana kuhusika.


Takukuru imesema miongoni mwa tuhuma hizo ni ile iliyotolewa na mfanyabiashara maarufu mjini Moshi, Elioth Lyimo aliyedai kuwa Sh25 milioni zake zilichukuliwa na Sabaya isivyo halali huku ikimtaja meya huyo kuhusika.


Katika maelezo yake, Raibu alisema tuhuma hizo ni za siku nyingi na hazina ukweli wowote.
“Tukio la siku nyingi hili limeshazeeka na ni la uongo,” alisema Raibu bila kutaka kufafanua kwa kina kuhusu suala hilo.


Juzi,  Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Kilimanjaro, Frida Wikesi aliliambia gazeti hili kuwa wapo baadhi ya watu wanatajwa kushirikiana na Sabaya kufanya uhalifu mkoani hapa, akiwamo Raibu ambaye naye anachunguzwa na endapo uchunguzi ukithibitisha kwamba, alihusika atafikishwa mahakamani
Wakati Wikesi akieleza hayo, siku hiyohiyo mkurugenzi mkuu wa taasisi hiyo, Salum Hamduni alisisitiza kuwa ametuma vijana wake kuchunguza madai ya Lyimo aliyedai kuwa Sh25 milioni zake zilichukuliwa na Sabaya isivyo halali.

Taarifa za mfanyabiashara huyo zilisambaa mitandaoni kuanzia juzi jioni. Juni 4, mwaka huu Sabaya (34) na walinzi wake watano walifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Arusha wakikabiliwa na tuhuma mbalimbali, ikiwamo uhujumu uchumi, utakatishaji fedha na kupokea rushwa.


Sabaya ambaye alisimamishwa na Rais Samia Suluhu Hassan Mei 13, 2021 kupisha uchunguzi, alifikishwa mahakamani hapo akiwa amefungwa pingu, huku waendesha mashtaka wakisema mtuhumiwa huyo na wenzake wanadaiwa kutenda makosa hayo Januari 20 na Februari 9, mwaka huu.


Katika ufafanuzi wa tuhuma zao, Sabaya na wenzake watano wanatuhumiwa kwa makosa ya kuunda genge la uhalifu, uhujumu uchumi, kujipatia fedha kwa njia ya rushwa na utakatishaji fedha, huku Sabaya alijipatia Sh90 milioni kutoka kwa mfanyabiashara, Francis Mroso, mkazi wa kwa Mromboo ambaye alikuwa anatuhumiwa kwa makosa ya ukwepaji kodi ili amsaidie, jambo ambalo ni makosa kwa mujibu wa sheria.


Pia, Sabaya na walinzi wake wawili, Sylivester Nyengu (26) maarufu kicheche na Daniel Mbura (38) wanakabiliwa na makosa mawili ya unyang’anyi wa kutumia silaha wakidaiwa kuyatenda Februari 9, 2021.


Wanadaiwa walimfunga pingu na kumpiga Bakari Msangi, ambaye ni diwani wa CCM Sombetin na kumuibia Sh390,000