Mfanyabiashara akutwa amejinyonga Arusha

Kamanda wa Polisi Mkoa Arusha, Jonathan Shana
Muktasari:
- Mfanyabiashara wa mitumba katika soko la Chini ya mti jijini Arusha, Kelvin Didas (26) amekutwa amekufa kwa kujinyonga leo asubuhi jirani na nyumbani kwake.
Arusha. Mfanyabiashara wa Mitumba na Mkazi wa Sanawari Mtaa wa Texas jijini hapa, Kelvin Didas (26) anadaiwa kujinyonga hadi kufa eneo la jirani na nyumbani kwake.
Mke wa mfanyabiashara huyo, Jack Denis amesema mumewe hakurudi nyumbani usiku wa kuamkia leo Jumapili Februari 2, 2020 kutokea kazini na yeye hakushtuka maana huwa ni kawaida yake siku zingine kutorudi nyumbani akijua wamefuata mzigo mkoani Tanga.
Akizungumza na Mwananchi, amesema mapema leo asubuhi alipata taarifa kutoka kwa jirani yake aliyefika nyumbani kwake na kumuulizia alipo mumewe naye alimjibu hajarudi tokea jana.
“Nikaambiwa nitoke nje nielekee eneo alipo, nikamkuta tayari amekufa akiwa amenyongwa na nguo zake,” amesema.
Marehemu ameacha mtoto mmoja anayejulikana kwa jina la amani Kelvin (2) .
Akizungumzia tukio hilo, Balozi wa mtaa huo, Elizabeth Thimos amesema leo asubuhi Saa 2 kasoro robo alifuatwa na mama anayejulikana kwa jina la mama Winner na kumueleza kuwa kuna mtu amekufa, akachukua hatua ya kumtafuta mwenyekiti wa kitongoji hicho lakini hakupatikana .
Balozi aliendelea kusema baada kutompata kiongozi mwenzake ndipo alipochukua hatua ya kutoa taarifa kituo cha Polisi cha Mjini kati ambao walifika na kuuchukua mwili kwa ajili ya uchunguzi zaidi pamoja na kuuhifadhi.
Hata hivyo, haijulikani kama marehemu alijinyonga mwenyewe ama amenyongwa.
Kamanda wa Polisi Mkoa Arusha, Jonathan Shana amethibitisha kupata taarifa za tukio hilo na uchunguzi wa tukio hilo unaendelea.