Mfumo dume, mila potofu vyanzo mauaji ya wanawake

Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, Dk Anna Henga
Muktasari:
- Sababu kadhaa zinachangia mauaji ikiwepo mila potofu, mfumo dume na wanawake kuwa na uwezo wa kiuchumi.
Arusha. Wastani wa wanawake 492 wanauawa kila mwaka kuanzia mwaka 2018 hadi mwaka 2022 ikiwa ni wastani wa vifo vya wanawake 43 kila mwezi.
Utafiti wa mauaji hayo, umezinduliwa jana Oktoba 26, 2023 na Kituo cha Sheria na Haki za Binaadamu (LHRC) katika maadhimisho ya wiki ya Asasi za Kiraia nchini, ambayo inaendelea katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano Arusha (AICC).
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa ripoti, Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, Dk Anna Henga amesema utafiti huo, umefanyika ndani ya miaka mitano katika taarifa zilizokusanywa kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi nchini.
“Ripoti hii tumeizindua leo na tunaimani itapatikana kwa asasi ambazo zinahitaji lakini pia kwa wadau wengine wa masuala ya haki za wanawake,”amesema.
Akielezea ripoti hiyo, Ofisa Miradi Kitengo cha Wanawake, Watoto na Watu wenye ulemavu wa LHRC, Wakili Getrude Dyabene, amesema katika utafiti huo, kwa kipindi cha miaka mitano mwaka 2018 hadi 2022 wanawake 2,438 waliripotiwa polisi kuuawa.
Amesema kuanzia Septemba mwaka jana hadi Septemba mwaka huu, wanawake 472 wameripotiwa kuuawa ambao ni sawa na wanawake 53 kila mwezi ikiwa ni ongezeko la wanawake 10 kila mwezi kutoka takwimu za miaka mitano iliyopita.
Wakili Dyabene amesema utafiti umebaini vyanzo vya mauaji hayo, ni imani potofu za ushirikiana, mila na desturi, dini, tabia, wanawake kukubali kufanyiwa ukatili hadi kufikia kuuawa, mifumo dume, elimu na wanawake kuwa na uhuru wa kiuchumi na jinsi matukio ya ukatili yanavyoripotiwa kwenye vyombo vya habari.
“Baadhi ya wanaume ambao wamezidiwa vipato na wake, zao wamekuwa wakiona wamekosa mamlaka kwenye familia na hivyo kuamua kuwaua wenza wao,”amesema.
Amesema utafiti wa vyanzo vya vifo hivyo, ulifanywa katika mikoa ambayo ilikuwa inaongoza kwa mauaji ya wanawake ambayo ni Mwanza Geita, Shinyanga, Dar es Salam na Kilimanjaro.
Wakili Dyabene amesema mauaji ya makusudi ya wanawake yanaongezeka kwa sababu hakuna sheria maalumu ya ukatili wa kijinsia kuhusiana na mauaji ya makusudi ya wanawake na hivyo mauaji hayo kuonekana na kuripotiwa kama mauaji ya aina nyingine.
Akizungumza katika uzinduzi huo, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), Ofisi ya Mkurugenzi wa Upelelezi, Tulibake Mwasongwa amesema tatizo la mauaji ya wanawake ni bado kubwa nchini.
Hata hivyo amesema polisi inaendelea kushughulikia ambapo tayari limeunda madawati 420 ya jinsia katika vituo mbali mbali vya polisi nchi nzima.
Amesema katika taarifa za polisi kuanzia Januari hadi Juni mwaka huu, wanawake 298 wameuawa katika matukio tofauti.
Amesema Idadi katika kipindi hicho cha Januari hadi June mwaka 2022 wanawake 308 waliuawa kikatili na taarifa zao kuripotiwa polisi.
“Haya ni matukio machache tu ambayo yaliripotiwa polisi lakini kuna matukio mengine ambayo hayajaripotiwa”amesema.
Akizungumza katika mkutano huo, Mchungaji Richard Hananja amesema ongezeko la vifo vya wanawake linachangiwa pia na kukosekana malezi bora katika jamii lakini pia familia na taasisi za dini kushindwa kutoa mafunzo ya maisha kwa watoto.
“Lakini pia mila na desturi zetu zimejaa usiri, hatuwambii ukweli watoto,hatuwafundishi dini, katika makanisa na misikiti wanakaa muda mfupi ambao hautoshi kufundishwa kila kitu”amesema