Mganga anayetuhumiwa kumuua mlinzi wake mbaroni

Kamanda wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro akitoa taarifa ya tukio la  mauali yaliyotokea Aprili 21 maeneo ya Kigogo Fresh, Dar es Salaam.

Muktasari:

  • Tukio la mauaji hayo lilitokea Aprili 21, Mwaka huu eneo la Kigogo Fresh, Pugu Wilaya ya Ilala Dar es Salaam na chanzo cha mauaji hayo kinadaiwa ni wizi.

Dar es Salaam. Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam limethibitisha kumtia mbaroni Mganga wa kienyeji Tazani Nonyo kwa tuhumiwa za mauaji ya mlinzi wake Japhari Mwinyimvua (40).

Tukio la mauaji hayo lilitokea Aprili 21, Mwaka huu eneo la Kigogo Fresh, Pugu Wilaya ya Ilala Dar es Salaam na chanzo cha mauaji hayo kinadaiwa kuwa  ni baada ya Tazani kumshutumu mlinzi wake Mwinyimvua kumuibia baadhi ya mali zake alizokuwa akizilinda.

Hata hivyo, katika mtiririko wa mkasa huo, Richard Nonyo (65) ambaye ni baba mzazi wa Tazani aliuawa kwa kushambuliwa na kundi la wananchi wenye hasira kali wakimtuhumu mtoto wake kuhusiana na kifo cha mlinzi huyo.

Akizungumzia tukio hilo, leo Aprili 22, Kamanda wa kanda hiyo, Jumanne Muliro amesema mganga huyo tayari wamemkamata na wanaendelea na uchunguzi wa tukio hilo ili watuhumiwa wote waliohusika watiwe mbaroni.

"Tazani amekamatwa maeneo ya Chanika mchana wa (leo) akiwa kwenye harakati za kukimbia. Na bado Jeshi la linaendelea chunguza kwa haraka tukio hilo na wahusika wote wa tukio hilo watakamatwa na kufikishwa mahakamani kwa hatua zaidi za kisheria.," amesema

 Katika hatua nyingine, Kamanda Muliro amesema Jeshi hilo limewakamata Furaha Jacobo(32) mkazi wa Masaki na Mustafa Kihenga (28) Mkazi wa Mwenge TRA kwa tuhuma za uhalifu wa kimtandao kwa kusambaza picha chafu za mnato na video mjongeo za watu zisizokuwa na maadili.

Muliro amesema watuhumiwa hao walikuwa wanatelekeleza shughuli hiyo kwa lengo la kujipatia fedha kwa vitisho.

"Watuhumiwa hawa wanatarajiwa kufikishwa mahakamani leo kujibu tuhuma zinazowakabili," amesema Muliro. 

Kamanda Muliro ametoa wito kwa wananchi linapotokea tukio au jambo lolote,  watu wenye jukumu la kufanya uchunguzi wa masuala yote ya kijinai ni mamlaka zilizokabidhiwa kisheria.

"Tunataka wananchi waache mara moja tabia ya kufanya mambo kinyume na sheria ikiwa ni pamoja na suala la kujichukulia sheria mkononi. Jeshi halitasita kufuatilia kupata ushahidi na kuwakamata watu wanaotenda makosa huku wakijidai kwamba wana hasira kali," amesema.

Muliro amesema kufanya kosa kwa kisingizio cha hasira kali ni kosa kisheria huku akieleza mamlaka zilizopewa nguvu kisheria zitaendelea kufuatilia na kuwakamata wote kisha kuwafikisha mahakamani.

"Hakuna mtu yeyote mwenye mamlaka kuondoa uhai wa mtu yeyote kwa sababu zozote zile hiyo ni sheria ya jumla ambayo ni msingi wa haki ya kila mtu kuishi bila hata kuchambua kwenda kwa kina," amesema.