MAONI YA MHARIRI: Watanzania tuna kila sababu ya kutochukua sheria mkononi

Gazeti hili toleo la jana kulikuwa na habari iliyoeleza kuwa jiji la Dar es Salaam linaongoza kwa mauaji ya kujichukulia sheria mkononi. Habari hiyo ilitokana na taarifa ya Mtafiti wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kuhusu hali ya haki za binadamu kwa kipindi cha nusu mwaka kuanzia Januari hadi Juni, mwaka huu.
Mtafiti huyo, Fundikira Wazambi alinukuu ripoti ya Polisi kuwa jumla ya watu 479 wameuawa nchini kutokana na watu kujichukulia sheria mkononi.
Taarifa ya Wazambi inaonyesha kuwa Mkoa wa Dar es Salaam unaongoza kwa matukio hayo kwa kuwa na vifo 117, ukifuatiwa na Mbeya (33), Mara (28) na Geita (26).
Pia, mkurugenzi wa LHRC, Dk Helen Kijo-Bisimba alisema kituo hicho kimepokea malalamiko kutoka kwa wananchi wakidai kuteswa na wengine wameuawa kwa tuhuma za mauaji yanayofanyika Kibiti, Mkuranga na Rufiji mkoani Pwani.
Ripoti ya LHRC ni mwendelezo wa taarifa za vitendo vya watu kujichukulia sheria mkononi ambavyo vimekuwa vikiripotiwa mara kwa mara na vyombo vya habari nchini.
Tunapinga tabia ya wananchi kujichukulia sheria mkononi, kwa sababu kuna watu ambao wanauawa kwa kuchomwa moto na wengine kupata majeraha makubwa hadi ulemavu wakati si wahalifu.
Mfano wa hili ni tukio lililowahi kutokea mkoani Geita ambako kijana mwenye umri wa miaka 22 aliuawa kwa kupigwa na wananchi kwa madai alikuwa mwizi, wakati ilibainika baadaye hakuwa na hatia.
Tunasisitiza wananchi kuacha kuchukua sheria mkononi, sababu si wote wanaoitwa wezi ni wahalifu, lakini hata kama mtu ni mhalifu kuna haja ya kujiuliza kosa alilolifanya linastahili adhabu ya kifo cha kikatili au kupewa ulemavu unaotokana na kipigo kinachotokana na kile kinachoelezwa kuwa ni hasira kali?
Rai yetu kwa Jeshi la Polisi lisiwaonee huruma watu wanaosababisha mauaji au ulemavu kwa watu ambao hawakustahili kufanyiwa hivyo, sheria zipo kwa ajili ya wanaozivunja, kwa maana hiyo wahalifu wote wafikishwe kwenye vyombo vya sheria.
Lakini, Jeshi la Polisi nalo lihakikishe kwamba linafuta dhana iliyojengeka kwamba wahalifu wanapofikishwa vituoni wanaachiwa kwa njia zisizoeleweka kwani hali hiyo wakati mwingine inaweza kuwa mojawapo ya mambo yanayowachochea wananchi kujichukulia sheria mkononi.
Iwapo Polisi watarejesha imani kwa wananchi kwamba hakuna mhalifu atakayeachiwa kwa mlango wa nyuma, na badala yake wote wakafikishwa mahakamani ili sheria ichukue mkondo wake, pengine hasira za wananchi zitapungua kwa kiasi kikubwa.
Tumeona ripoti ya LHRC ikililaumu jeshi hilo kwamba nao wamekuwa wakichukua sheria mkononi kwa kuwaadhibu watuhumiwa wanaowakamata.
Kazi ya polisi ni taaluma, askari wote walioko kwenye jeshi hilo wamepitia kwenye vyuo stahiki vinavyotoa mafunzo ya namna ya kupambana na wahalifu na si kuwaumiza au kuwaua bila kufuata utaratibu.
Tunaamini vitendo vinavyofanywa na baadhi yao vya kuwapiga au kuwaumiza watuhumiwa ni sawa na kujichukulia sheria mkononi. Nao tunawasihi kuwa mfano wa kuigwa kwanza kwa kuwakamata wananchi wenye vitendo vya kujichukulia sheria mkononi na wao kuacha vitendo hivyo.
Madhara yanayotokana na kupiga au kuua wahalifu ni makubwa kuliko inavyodhaniwa, tunaamini kwa kutumia vyombo vya sheria, tabia ya mtu inaweza kurekebishika na kuwa raia mwema katika jamii.
Rai yetu kwa polisi ni kuongeza nguvu ya kupambana na wananchi wenye kuendeleza tabia ya kuchukua sheria mkononi.