Mganga wa jadi jela kwa kosa la kumuua mwenzake wakigombea mwanamke

Mganga wa jadi jela kwa kosa la kumuua mwenzake wakigombea mwanamke

Dar es Salaam. Mganga wa kienyeji, Ismail Ramadhani (27) amehukumiwa kifungo cha mwaka mmoja jela, baada ya kupatikana na hatia ya kumuua mwanaume mwenzake bila kukusudia, wakiwa wanagombania mwanamke.

Ramadhani ambaye ni mkazi wa Vingunguti jijini Dar es Salaam, amehukimiwa kifungo hicho leo Jumanne, Septemba 6, 29022 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkuu, wakati kesi yake ya mauaji ilipokuja kwa ajili ya usikilizwaji wa upande wa mashtaka.

Hukumu hiyo imetolewa na Hakimu Mkazi Mkuu, Joyce Minde, baada ya mshtakiwa kukiri shtaka lake mbele ya mahakama.

Awali, kabla ya kuanza na usikilizwaji wa shauri hilo, upande wa mashitaka waliomba kumkumbusha Ramadhani kosa lake na  baada ya kukumbushwa alikiri kosa la kuua bila kukusudia.

Wakili wa Serikali, Mosie Kaima alidai mshtakwia anadaiwa kutenda kosa hilo, Novemba 13, 2015, maeneo ya Vingunguti mji mpya, iliyopo wilaya ya Ilala, alimuua Mohamed Kamogela bila kukusudia.

Kaima alidai siku hiyo ya tukio saa 2 usiku, mshitakiwa walikuwa wanagombania mwanamke aliyetajwa kwa jina moja la Ester ambaye alikuwa na mahusiano wa kimapenzi naye kwa muda tofauti.

"Ugomvi huo uliibuka baada ya Kamogela kumtuhumu kuwa anaendelea na uhusiano na mwanamke huyo huku mshitakiwa akimueleza kwamba hana tena mahusiano wa kimapenzi na huyo mwanamke," alidai wakili Kaima.

Wakili huyo aliendelea kudai wakati wa mabishano hayo marehemu alikuwa ameambatana na watu wanne wakiwa na mapanga ambapo walianza kumpiga mshitakiwa kwa bapa na mapanga hayo.

Wakili Mosie alidai wakati tukio hilo linaendelea kuna mtu ambaye alijulikana kwa jina la Ally rafiki na mshitakiwa akiwa eneo hilo alimrushia kisu ili aweze kujiokoa.

"Baada ya kudaka kisu hicho mshitakiwa alikitumia kisu hicho kumchoma katika mkono wa kushoto ambapo marehemu alikimbia na kuangukia katika varanda ya nyumba ambayo ilikuwa karibu na eneo hilo kisha kufariki dunia," alidai wakili Kaima

Aliendelea kuieleza Mahakama marehemu baada ya kufariki askari polisi walipata taarifa ambapo mwili wa marehemu ulichukuliwa na kupelekwa hospitali ya Amana na kisha Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa ajili ya uchunguzi.

Hata hivyo, uchunguzi ulibaini marehemu alipoteza damu nyingi.

Alidai askari polisi walikwenda eneo la tukio kisha kuchora ramana na Novemba 16, 2015 mshitakkwa alikamatwa.

Baada ya maelezo hayo mshitakkwa alikiri kosa la kuua bila kukusudia na na ndipo mahakama ilipomtia hatiani kama alivyoshtakiwa.

Upande wa mashtaka uliomba  Mahakama itoe adhabu kwa mujibu wa sheria kwani mshitakiwa alitumia kisu kumchoma marehemu.

“Marehemu akiwa na wenzake kama walikuwa wanataka kumuua mshitakiwa wangemuua muda mfupi, hawakuwa na  nia ya kumuua, hivyo mshitakiwa apewe adhabu kwa mujibu wa sheria," alidai.

Naye wakili wa mshtakiwa, Yohana Kibinda, alidai mteja wake amekaa gerezani kwa kipindi cha miaka saba ni muda mrefu kwani wakati huo alikuwa na miaka 20

"Wakati ugomvi unatokea mteja wangu hakuwa na nia ya kusababisha kifo, hivyo naomba mahakama ampewe adhabu nafuu ili aweze kutumikia taifa lake kwani ana wazazi  na mtoto mdogo wanamtegemea, "alidai Wakili Kibinda.