Mganga wa jadi kunyongwa kwa kuua watoto wawili Rukwa

Muktasari:

  • Mahakama Kuu Kanda ya Sumbawanga imemhukumu mganga wa jadi, James Kapyela (57) kunyongwa hadi kufa, baada ya kumtia hatiani kwa kosa la kuwaua kwa makusudi watoto Nicholaus Mwambage (7) na Emmanuel Juma (4).

Rukwa. Mahakama Kuu Kanda ya Sumbawanga imemhukumu mganga wa jadi, James Kapyela (57) kunyongwa hadi kufa, baada ya kumtia hatiani kwa kosa la kuwaua kwa makusudi watoto Nicholaus Mwambage (7) na Emmanuel Juma (4).

Ilidaiwa kuwa mganga huyo aliwalawiti watoto hao kabla ya kuwaua na kutupa miili yao kwenye pagala liliopo nyumbani kwake Machi 23, 2019 katika Mtaa wa Vuta, Kitongoji cha Kizwite, Sumbawanga Mjini.

Jaji Thadeo Mwenempazi alisema wakati akisoma hukumu hiyo jana Jumanne Oktoba 26, 2022 kuwa mahakama imeridhika kuwa mashahidi 11 wa Jamhuri wamethibitisha mashtaka dhidi ya mganga huyo.

Jamhuri iliwakilishwa na mawakili Marieta Maguta waliosaidiana na wakili Saimon Peres.


Watoto wapotea

Kabla ya kuthibitika kuuawa, watoto hao walitoweka nyumbani kwao na kuwafanya wazazi na majirani kuanzisha juhudi za pamoja kuwatafuta huku wakitoa taarifa katika Kituo cha Polisi, Sumbawanga Mjini.

Ilidaiwa kuwa siku iliyofuata binti mmoja aliyekuwa amekwenda mtoni kuteka maji alidai kumwona mmoja wa watoto walipotea na kutoa taarifa kwa wazazi wa watoto hao.

Aliwaeleza alikokuwa na kuwaacha wenzake. Katika jitihada za kuwatafuta, wazazi hao waliamua kuambatana naye hadi alikokuwa ili asaidie kupatikana watoto hao.

Mahakama ilielezwa kuwa walipofika kwenye nyumba ya mtuhumiwa, wazazi hao walikuta gari bovu lililokuwa limeegeshwa nje na walipo fungua mlango wa gari hilo walikuta kinyesi cha binaadamu na harufu kali huku nzi wengi wakirandaranda eneo hilo.

Baada ya kushuhudia hayo, wazazi hao hawakuishia hapo bali waliamua kwenda kwenye pagala lililopo karibu na nyumba ya mganga huyo na kukuta miili ya watoto hao ikiwa imetupwa hovyo.

Walilawitiwa

Uchunguzi wa kitabibu ulionesha kuwa watoto hao walilawitiwa kabla ya kunyongwa.

Baada ya Kapyela kutiwa hatiani, mawakili wa Serikali waliiomba mahakama itoe adhabu kali ili iwe fundisho na zuio kwa weingine wanaotamami kufanya vitendo kama hivyo. 

Aidha, upande wa utetezi uliongozwa na Wakili Deogratias Sanga huku mtuhumiwa akiwa hana mashaidi isipokuwa alikua peke yake ambapo alipewa nafasi ya kujitetea kabla ya mahakama kutoa hukumu hiyo.

Mshtakiwa huyo aliyekuwa akitetewa na wakili Deogratias Sanga alipewa nafasi ya kujitetea dhidhi ya adhabu hiyo na kuiomba mahakama impunguzie adhabu akidai kuwa kosa hilo ni la kwanza kwake na kwamba ana familia inayomtegemea.

Jaji Mwenempazi alisema mikono yake ilikuwa imefungwa kwani kifungu cha 196 had 197 cha Kanuni ya Adhabu kinatoa adhamu moja tu ya kunyongwa hadi kufa kwa mtu aliyepatikana na hatia ya kuua kwa makusudi.