Mgogoro wa meya, mkurugenzi Mwanza unavyowatesa madiwani

Meya wa Jiji la Mwanza, James Bwire akiomba miadi ya kukutana na Rais John Magufuli kwa kuwa ana mambo ya kumueleza na asingeweza kuongea hadharani katika eneo la Igogo jijini Mwanza hivi karibuni. Picha na Michael Jamson

Mwanza. Wakati Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella akitangaza kuingilia kati kutatua mgogoro kati ya meya James Bwire na mkurugenzi wa jiji, Kiomoni Kibamba kutekeleza agizo la Rais John Magufuli, mgogoro huo umeendelea kuwapasua vichwa viongozi.

Hii ni baada ya mwendelezo wa vikao vya baraza la madiwani kushindikana kutokana na shinikizo la madiwani kumtaka meya huyo ajiuzulu wakidai kutokuwa na imani naye. Akizungumza na Mwananchi ofisini kwake jana, Mongella alisema Serikali haiwezi kuvumilia kuona mgogoro huo ukikwamisha vikao vya baraza na maendeleo ya wananchi. “Vikao vya baraza la madiwani na kamati zinazoongozwa na meya vimekwama tangu mwezi Agosti. Hatuwezi kuvumilia hali hii, ofisi yangu itaingilia kati,” alisema Mongella.

Kikao kingine chavunjika

Licha ya agizo la Rais John Magufuli la kuwataka viongozi wa Mwanza kumaliza mgogoro huo kwa njia ya mazungumzo, kikao cha baraza la madiwani kilichoitishwa Novemba 2, hakikufanyika kutokana na shinikizo la baadhi ya madiwani la kumkataa meya huyo.

Hiki ni kikao cha pili kushindikana kwa sababu hiyohiyo baada ya kile cha Agosti 16.

Kabla ya kuahirisha kikao hicho kabla ya Meya Bwire kuwasili ukumbini, mkurugenzi wa jiji, Kiomoni Kibamba aliyegoma kujibu maswali wala kutoa ufafanuzi kwa waandishi wa habari, aliwaambia wajumbe kuwa watajulishwa siku ya kufanyika kikao kingine.

Muda mfupi baada ya Kibamba kuahirisha kikao na madiwani wanaotokana na CCM kutoka ukumbini, Meya Bwire aliingia ukumbini na kuwatangazia madiwani wanaotokana na Chadema ambao walikuwamo ikumbini kuwa kikao hicho kitaitishwa siku nyingine.

Kama ilivyokuwa kwa Kibamba, Bwire naye alikataa kujibu maswali wala kutoa ufafanuzi kwa waandishi wa habari sababu za kikao kutofanyika.

Agizo la Rais Magufuli

Akihutubia wananchi katika mkutano wa hadhara eneo la Nyakato Oktoba 30, Rais Magufuli aliwaagiza viongozi wa wilaya na Mkoa wa Mwanza kutumia njia ya majadiliano kutatua tofauti miongoni mwao badala ya kufikishana polisi.

“Meya ni wa CCM (Chama Cha Mapinduzi) na viongozi wote wa jiji, wilaya na mkoa pia ni wa CCM, tumieni vikao kumaliza tofauti zenu,” aliagiza Rais Magufuli

Mkuu huyo wa nchi alitoa agizo hilo akijibu moja ya mabango ya wakazi wa Kata ya Mahina kuhusu tukio la kukamatwa na kuswekwa mahabusu Meya Bwire kwa kile kilichodaiwa ni kumzuia kuwasilisha mbele ya Rais suala la mgogoro kati yake na viongozi wenzake.

Chadema wawashutumu CCM

Akizungumzia kukwama kwa vikao vya baraza kwa mara ya pili mfululizo, diwani wa Butimba, John Pambulu (Chadema), aliwatupia lawama wenzake wa CCM kwa kutumia mgogoro kati ya meya na mkurugenzi kukwamisha vikao na shughuli za maendeleo ya wananchi. “Ni vyema wenzetu wa CCM watumie vikao vyao kumaliza migogoro yao badala ya kukwamisha vikao vya baraza na hivyo kukwamisha maendeleo ya wananchi zaidi ya 300,000 wa Jiji la Mwanza,” alisema Pambulu.

Jiji la Mwanza lenye kata 18, lina madiwani 24, CCM inayoshikilia kata 14 ikiwa na madiwani 20 na Chadema inayoongoza kata tatu ikiwa na madiwani wanne.

CCM kuingilia kati

Akizungumzia suala hilo, mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Nyamagana, Athumani Zebedayo aliahidi kuwa chama hicho kitaingilia kati mgogoro huo kutokana na kuhusisha viongozi na madiwani wanaotoka chama hicho. “Inaumiza kuona viongozi na madiwani wa CCM ndio wanaokwamisha maendeleo ya wananchi kutokana na mivutano miongoni mwao, chama kitachukua hatua,” alisema Zebedayo.

Wakati hayo yakijiri, tayari madiwani 20 wamewasilisha hoja ya kutokuwa na imani na meya wakimtaka kuachia ngazi, huku kiongozi huyo akisisitiza msimamo wa kutojiuzulu akisema hakuna hoja wala tuhuma za msingi dhidi yake.

Madiwani washambuliwa

Katika hatua nyingine, madiwani, watendaji wa Jiji la Mwanza na waandishi wa habari waliokuwa kwenye ziara ya kukagua miradi ya maendeleo jijini humo, juzi walilazimika kutimua mbio kujinusuru kutoka mikononi mwa wakazi wa Kata ya Mahina inayoongozwa na Meya Bwire waliokuwa wakiwashambulia kwa mawe kuwazuia kukagua majengo ya zahanati ya kiongozi huyo yanayodaiwa kujengwa eneo la umma.

Kama si uhodari wa kutimua mbio, msafara huo uliokuwa na watu zaidi ya 30 wakitumia magari matatu, pengine yangetokea mambo makubwa kutokana na wananchi hao waliojigawa makundi matatu na kuuweka kati msafara huo.

Pia walibeba silaha za jadi ikiwamo mapanga, sime, marungu na fimbo.

Akizungumzia tukio hilo, mkuu wa msafara ambaye ni diwani wa Mkolani, Dismas Litte alisema suala hilo litajadiliwa na kuamuliwa kupitia vikao, huku akionya kuwa hatua kali za kisheria na kinidhamu lazima zichukuliwe dhidi ya watakaobainika kuwa nyuma ya mashambulizi hayo.

Waandishi wa habari waliokuwa wakipiga picha tukio hilo nao walilazimika kutimua mbio baada ya kundi lingine lililojificha kuibuka na kutaka kuwapora kamera zao.

DED, meya wanasemaje?

Akizungumzia mgogoro huo, Meya Bwire aliyetangaza mbele ya Rais Magufuli utayari wa kukaa na viongozi wenzake kumaliza tofauti miongoni mwao, alisema mgogoro wa kiungozi unaoendelea ndani ya jiji unatokana na msimamo wake wa kupiga vita ufisadi anaodai hauwafurahishi viongozi wenzake kuanzia ndani ya jiji, Wilaya ya Nyamagana na Mkoa wa Mwanza.

Meya huyo ambaye pia ni mkurugenzi mtendaji wa mtandao wa Taasisi ya Alliance inayomiliki shule, kituo cha kulea na kukuza vipaji na timu ya soka alitaja miradi ya dampo la Buhongwa na ule wa maji uliopo Fumagila kama mifano ya matumizi mabaya ya fedha za umma.

Mkurugenzi wa jiji, Kibamba alisema binafsi hana tatizo na Bwire zaidi ya kutekeleza wajibu na majukumu yake kisheria ikiwamo kuzuia viongozi wa kisiasa kutumia nafasi zao kuingilia masuala ya kiutendaji.

Kuhusu madai ya ufisadi kwenye ujenzi wa nyumba katika dampo la kisasa eneo la Buhongwa kwa gharama ya Sh400 milioni na mradi wa maji Fumagila uliogharimu Sh800 milioni, anakanusha huku akidai kuwa tayari ameiomba Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kuchunguza tuhuma hizo.

Habari hii imeandikwa na Peter Saramba, Ngollo John na Jesse Mikofu