Mgomo wa daladala wawagawa wananchi Mbeya, viongozi wajifungia

Abiria wakiwa kwenye stendi ya daladala ya Kabwe jijini Mbeya kufuatia mgomo wa magari leo, Oktoba 17.

Muktasari:

  • Wakati viongozi wa serikali na wamiliki wa magari yanayofanya shughuli zake jijini Mbeya wajifungia kujadili hatima ya mgomo wa daladala, wananchi wametofautiana mtazamo juu ya changamoto hiyo.

Mbeya. Wakati daladala jijini Mbeya zikigoma kufanya kazi, wananchi wametofautiana mtazamo kuhusu kupanda kwa nauli, huku baadhi wakisema iongezeke na wengine wakipinga kwa sababu tofauti.

 Leo Oktoba 16,2023 mabasi yanayofanya shughuli zake jijini hapa yameweka mgomo ikielezwa kushinikiza kupanda kwa nauli kutokana na bi ei ya mafuta kuwa juu.

Mmoja wa madereva ambaye hakutaka kutajwa majina yake amesema gharama za mafuta ziko juu, hivyo nauli ya Sh500 inakuwa changamoto kwao katika kupata malipo.

“Bosi ukimpelekea hesabu ambayo hamjakubaliana hawezi kukuelewa, tumeamua leo tusifanye kazi, wakati matajiri wetu wakilifanyia kazi,” amesema.

Mariam Mwantona mkazi wa Kabwe jijini humo, amesema ni bora nauli ipande lakini wapate huduma ya usafiri kwani leo wameshindwa kuhudhuria mazishi ya mpendwa wao.

“Kwanza shughuli za uzalishaji zimekwama, wanafunzi nao lazima watachelewa masomo yao, bora nauli ipande kuliko hii changamoto inayotupata, tumeshindwa kwenda kuzika,” amesema Mariam.


Kwa upande wake Faustine Gile amesema maisha ya wananchi siyo mazuri akieleza kuwa kupandisha nauli itakuwa mzigo mzito mwingine kwao akiomba serikali kuingilia kati.

“Wanaoumia ni sisi wananchi wa kipato cha chini, leo Bajaji nauli yake imepanda tofauti na siku nyingine, ilianza kuwa Sh 500, ikaja Sh800 leo Sh1,000,”amesema Gile.

Mwananchi ilifika eneo la stendi ya daladala Kabwe jijini hapo na kushuhudia abilia wakiwa wamekaa na wengine kusimama wasijue la kufanya, huku bajaji zikiwa ndizo zinaendelea na shughuli.

Imeelezwa kuwa hadi sasa mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Beno Malisa amejifungia na viongozi wengine wakiwamo Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (Latra), wamiliki wa daladala na baadhi ya madereva wakijadili hali hiyo.