Miaka 60 ya mapinduzi; tulikotoka, tulipo na tunakokwenda

Muktasari:

  • Usiku wa Jumamosi kuamkia Jumapili, Januari 12, 1964, kulitokea mapinduzi yaliyouondoa madarakani utawala wa Kisultani katika visiwa vya Zanzibar. Ndipo ikaundwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ).

Zanzibar imeadhimisha miaka 60 ya Mapinduzi huku ikiwa imepiga hatua mbalimbali za kimaendeleo na utoaji wa huduma bora za kijamii.

Usiku wa Jumamosi kuamkia Jumapili, Januari 12, 1964, kulitokea mapinduzi yaliyouondoa madarakani utawala wa Kisultani katika visiwa vya Zanzibar. Ndipo ikaundwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ).

Mapinduzi ya Zanzibar ni miongoni mwa mlolongo wa mambo yaliyosababisha maasi ya Jeshi la Tanganyika yaliyofanyika juma moja tu baada ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Maasi ya Tanganyika, ambayo yalianzia kwenye Kambi ya Jeshi ya Colito—sasa Lugalo—usiku wa Jumamosi kuamkia Jumapili ya Januari 19, 1964. Matukio hayo mawili yaliyofuatana—Mapinduzi ya Zanzibar na maasi ya kijeshi ya Tanganyika—yalitoa mchango mkubwa kwa Tanganyika kuungana na Zanzibar siku 100 baadaye.

Hata hivyo, Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ambao ulizaa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni miongoni mwa mambo muhimu sana ambayo ni uzao wa Mapinduzi ya Zanzibar.

 Ingelikuwa vigumu kuwapo kwa Jamhuri ya Muungano iwapo kusingekuwa na Mapinduzi ya Zanzibar.

Kwa hakika kulikuwa na hatua mbalimbali za maendeleo zilizochukuliwa tangu siku za mwanzo za mapinduzi, hasa na Serikali ya awamu ya kwanza chini ya Sheikh Abeid Amani Karume, kama vile katika ardhi, sera ya makazi, elimu na huduma za matibabu bure.

Baada ya Mapinduzi, elimu ilitangazwa kuwa bure kwa Wazanzibari wote bila ya kujali rangi, imani au jinsia.

Kwa zaidi ya miaka 300 ya utawala wa ukoloni katika visiwa vya Zanzibar hadi kufikia mwaka 1964, watoto wa wanyonge walikuwa hawapati nafasi ya kusoma.

Septemba 23, 1964, Mzee Karume alitangaza kuwa elimu itatolewa bure kwa watu wote wa Unguja na Pemba. Pia, mwaka Machi, mwaka huo alitangaza afya kuwa bure. Lakini mambo mengi yamebadilika ndani ya miaka 60 ya Mapinduzi hayo.

Mwaka 1991, Serikali ilitoa Sera ya Elimu ya Zanzibar ambayo iliainisha malengo na shabaha muhimu za kisekta.

Sera hiyo ilifanyiwa marekebisho mwaka 1995 ili kuingiza idadi ya malengo yaliyotamkwa katika mikataba na matamko muhimu ya kimataifa.

Maarufu miongoni mwa matamko na mikataba hiyo ni Azimio la Dunia la Jomtien la mwaka 1990 kuhusu Elimu kwa Wote (EFA), Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Mtoto (CRC) na Mkataba wa Kutokomeza Ubaguzi Dhidi ya Wanawake (CEDAW).

Ili kutekeleza Sera ya mwaka 1995 iliyofanyiwa marekebisho, wizara yenye dhamana ya elimu ilitoa Mpango Mkuu wa Elimu (ZEMAP) mwaka 1996 unaobainisha malengo mipango ya utekelezaji kwa miaka kumi.

Kwa upande wa uchumi, katika miaka ya 1960 baada ya Mapinduzi na mwanzoni mwa miaka ya 1970, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ilianza baadhi ya miradi ya maendeleo.

Mingi ya miradi hiyo ilianzishwa na Karume na baada ya kifo chake, iliendelezwa na Jumbe. Baadhi ya miradi hiyo ni pamoja na ujenzi wa makazi ya umma Zanzibar mjini, ujenzi wa hoteli za kitalii ikiwamo hoteli ya kimataifa ya Bwawani, ujenzi wa uwanja wa Amani Unguja na baadaye Uwanja wa Gombani Pemba.

Miradi mingine ni ujenzi wa mfumo wa barabara, na ununuzi wa meli za abiria, MV Mapinduzi na MV Maendeleo na meli ya mizigo ya MV Uhuru, ili kupunguza adha ya usafiri.

Idadi ya shule na vituo vya afya ziliongezeka, lakini mradi mkubwa zaidi ulikuwa ni ule wa kujenga nyumba za umma, yalikuwa maarufu kama Maghorofa ya Michenzani ambayo yalianza kujengwa kwa ajili ya makazi bora ya wananchi wa Zanzibar wakati wa uongozi wa Sheikh Karume.

Serikali, kwa mfano, ilipanga kujenga maghorofa katika Mji wa Unguja, Chakechake, Wete na Mkoani Pemba. Michenzani pekee, Serikali ilipanga kujenga maghorofa ambayo yangekaliwa na watu 35,000 kwa gharama ya pauni milioni 20 za Uingereza.

Hii ni baadhi ya miradi mikuu ya maendeleo ambayo sasa inathaminiwa na serikali kuwa ni mafanikio ya Mapinduzi.

Katika kuhakikisha kuwa uchumi wa Zanzibar unaimarika, SMZ imeweka vipaumbele vitano katika sera ya uchumi wa buluu ili kuimarisha uchumi na kuboresha maisha ya wananchi.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi Zanzibar, Dk Aboud Jumbe, alitaja vipaumbele hivyo kuwa ni utalii, uvuvi, usafiri wa baharini, nishati na usimamizi wa bahari.

Sasa utalii umekuwa si kwa Zanzibar pekee bali kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, lakini kwa Zanzibar utalii wa pwani umekuwa ukiongeza mapato ya nchi.

Eneo jingine la kuimarisha uchumi ni uvuvi na mazao ya baharini kwa kuwa asilimia kubwa ya wananchi mmoja mmoja wa Zanzibar wanaguswa na sekta mbili muhimu za uvuvi mdogomdogo na mazao ya baharini.

Kipaumbele kingine ni usafiri wa baharini ambapo kuna bandari, miundombinu ya usafiri wa baharini, vyombo vya usafiri wa baharini, mchango wa kibiashara, mchango wa huduma wa usafiri wa baharini lakini pia usalama wa baharini.

Zanzibar kuna nishati na uchimbaji wa mafuta na gesi.

Sera ya uchumi wa buluu imelenga katika jitihada za Serikali za kuleta mageuzi katika uchimbaji wa mafuta na gesi kwa sababu ulimwenguni kote asilimia 30 ya uchimbaji wa mafuta na gesi unafanyika baharini.

Katika kuendeleza uchumi wa Zanzibar, Rais Hussein Mwinyi anasema bado nchi yake ina mahitaji makubwa ya uwekezaji kwenye sekta ya uchumi wa buluu kupitia utalii, uvuvi na ufugaji wa vifaranga vya samaki, na hivyo anawataka mabalozi wanaoiwakilisha Tanzania katika mataifa ya nje kutangaza maeneo hayo.

Kuelekea mwishoni mwa mwaka jana, Zanzibar imevutia uwekezaji wa karibu Dola za Marekani 3.73 bilioni (Sh9.4 trilioni) kupitia miradi iliyosajiliwa na Mamlaka ya Uwekezaji na Vitega Uchumi Zanzibar (ZIPA).

Kutokana na mikakati iliyowekwa na serikali yake, Dk Mwinyi sasa anawahakikishia wananchi wake mwaka 2024 wenye mafanikio zaidi, na kusema Zanzibar iko mbioni kufikia malengo yake ya maendeleo.

“Tunaelekea kwenye mustakabali mwema,” Dk Mwinyi alisema katika ujumbe wake wa Krismasi mwaka jana.

Zanzibar inahitaji utaratibu uliounganishwa vizuri unaojengwa kwa kufuata taratibu zinazohitajika ili kufikia malengo haya na kusaidia michakato hii.

Siyo wengi wanaoiona Zanzibar kama kitovu cha ukuaji wa uchumi. Visiwa hivyo vimefaidika na vivutio vyake vya asili na maisha tulivu kwa kuunda sekta ya utalii inayoingiza mamilioni ya dola ambayo inawavutia watalii.

Hata hivyo, bado kuna mengi zaidi yanaweza, au yanapaswa, kufanywa ikiwa Zanzibar itaongeza ukuaji wake wa uchumi na viwango bora vya maisha kwa wananchi wake.

Rais Mwinyi hawezi kufanya kazi hiyo peke yake, lakini kwa hakika anaweza kuweka mikakati zaidi ya kuimarisha uchumi zaidi.