Miili saba ya watoto waliokufa maji Arusha yatambuliwa
Muktasari:
- Jeshi la Zimamoto mkoani Arusha limetaja majina ya wanafunzi saba waliofariki baada ya gari walilokuwa wakisafiria kwenda shule kutumbukia kwenye Korongo lililojaa maji eneo la Dampo mkoani Arusha.
Arusha. Miili saba ya wanafunzi wa Shule ya Msingi Ghati Memorial waliofariki dunia baada ya gari walilokuwemo kusombwa na maji jana, imetambuliwa.
Ajali hiyo iliyoua watu wanane wakiwemo wanafunzi saba kati ya 11 waliokuwepo na muokoaji mmoja, ilitokea jana Aprili 12, 2024 saa 12:40 asubuhi kwenye Korongo lililojaa maji eneo la Dampo mkoani Arusha.
Shughuli za uokozi ziliyochukua saa 11, zikiongozwa na wananchi na vyombo vya ulinzi na usalama, ilifanikisha kupatikana miili saba ya wanafunzi na mtu mzima mmoja, huku mwanafunzi mmoja akiwa bado hajulikani alipo.
Kamanda wa Jeshi la Zimamoto Mkoa wa Arusha Osward Mwanjejele amesema leo Aprili 13, 2024 kuwa miili iliyotambuliwa ni ya Shedrak William, Noel Jonas na Dolan Jeremiah, Winfrida Emmanuel, Atrichan Emmanuel, Morgan Emmanuel, Abigail Peter na Abiabol Peter."
Amesema kikosi cha uokoaji kimerudi kazini kwa ajili ya kusaka mtoto mmoja ambaye hajulikani alipo baada ya miili kubainika kuwa saba badala ya nane ili kukamilisha idadi ya wanafunzi 11 waliokuwemo kwenye gari wakati ajali hiyo inatokea.
"Tulipata idadi ya wanafunzi waliokuwepo ni 11 na dereva pamoja na Matron, lakini jana katika uokozi tulipata miili saba na walionusurika watatu, maana yake hesabu bado inakataa, inamaanisha kuna mwanafunzi mmoja hajaonekana" amesema Mwanjejele.
Amesema kikosi cha uokoaji kutoka Jeshi la Zimamoto pamoja na Polisi wakishirikiana na wananchi wamerudi eneo la tukio kufuata mkondo huo wa maji hadi unapomwaga maji eneo la Olokii, zaidi ya kilomita 35.
Ametumia nafasi hiyo kuwataka wananchi kuchukua tahadhari kwenye mvua zinazoendelea kunyesha akizitaka shule zenye magari ya kubeba wanafunzi kuongeza umakini.
Mwili wa msamaria
Kamanda Mwanjejele ametoa wito kwa wananchi: "Wakazi wa eneo lile wajitokeze kuutambua mwili wa mtu mmoja ambaye alikuwa anasaidia shughuli za uokoaji, uliopatikana jana."