Mimea vamizi sasa yatishia malisho, migogoro ya ardhi

Arusha. Mimea vamizi inayosababishwa na mabadiliko ya tabia nchi imevamia zaidi ya ekari 7,000 katika Wilaya za Ngorongoro, Monduli na Longido.

Mimea hiyo inatajwa kuathiri malisho ya wanyamapori na mifugo katika wilaya hizo, kwani licha ya kutoliwa na wanyama, inazuia uoto wa majani ya asili ambayo ni chakula cha wanyama hao.

Taarifa zilizopo zinaonyesha kuwa mimea hiyo imeanza kuathiri maeneo ya kilimo kutokana kusambaa kwa kasi katika mashamba.

Wakizungumza na Mwananchi, baadhi ya watafiti, wafugaji na wahifadhi walieleza kuwa kama hatua za haraka zisipochukuliwa kudhibiti mimea hiyo, athari zake zitakuwa kubwa zaidi siku zijazo.

Mtafiti wa Taasisi ya utafiti wa Misitu (TAFORI), Dk Richard John alisema kumekuwepo na ongezeko la mimea vamizi katika misitu na maeneo ya nyanda za malisho.

Dk John alisema maeneo katika Wilaya ya Monduli yamevamiwa na miti aina ya Mrashia ambayo licha ya kuathiri malisho, inatumia kiasi kikubwa cha maji.

Mkurugenzi wa Jumuiko la Maliasili Tanzania (TNRF), Faustine Zakaria alisema changamoto ya mimea vamizi ni kubwa, lakini kuna mradi umeanzishwa kushughulikia hilo ambao unashirikisha Mamlaka ya Usimamizi Wanyamapori (TAWA), Taasisi ya Utafiti wa Misitu (TAFORI) na Taasisi ya utafiti na Maendeleo ya Jamii (CORDS).

Mkurugenzi wa shirika la CORDS, Lilian Looloital alisema maeneo yaliyoathirika kwa uvamizi wa mimea katika Wilaya ya Longido ni Entuimet WMA, Wosi-wosi maeneo ya Lake Natron.

Alisema Wilaya ya Monduli ni Selela, Mto wa Mbu, Engaruka na mipaka ya Lake Natron na Wilaya ya Ngorongoro - Pinyinyi, Enkaresero na maeneo mengine ya pembezoni.

Mwenyekiti wa kitongoji Cha Kigongoi, Wilaya ya Monduli Philemon Laizer, alisema mimea vamizi imekuwa changamoto na inamaliza malisho ya mifugo.

Ofisa mabadiliko ya tabianchi katika Wilaya ya Longido, Nestory Daqaro alisema zaidi ya ekari 1,000 katika wilaya hiyo zimevaniwa na mimea vamizi.

"Ili kukabiliana na hali hii tumeanza kung'oa mimea hii vamizi, lakini pia kuanza kuandaa maeneo mbadala ya malisho ya mifugo," alisema.

Mwenyekiti wa bodi ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), Venance Mabeyo alitaka kufanyika kwa utafiti wa kuondoa mimea vamizi ndani ya eneo la Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro.
Katika hifadhi hiyo eneo kubwa, hasa katika bonde limevamiwa na mimea vamizi ambayo si malisho ya wanyamapori.

Migogoro
Katika hatua nyingine ilielezwa kuwa baadhi ya migogoro ya ardhi iliyoleta athari za kiuchumi na kijamii kwa watu, inachangiwa na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Mwaka 2022 ukame uliathiri maeneo mengi ya nchi, wafugaji walijikuta wanaingiza mifugo yao katika mashamba ya wakulima kwa ajili ya kutafuta malisho.

Vijiji vinavyopakana vya Elerai kilichopo Kata ya Ormolog wilayani Longido Mkoa wa Arusha na kijiji cha Ngarenairobi kilichopo Wilaya ya Siha (Kilimanjaro), vimetumbukia katika migogoro ya wakulima na wafugaji.

Migogoro hiyo ilitokana na kugombania maeneo ya kulima na kufuga baada ya kukosekana kwa mvua muda mrefu, ikiwa ni matokeo ya mabadiliko ya tabianchi.

Mwenyekiti wa kijiji cha Elerai, Simon Ole Nasalei (51) aliliambia Mwananchi kuwa chanzo cha mgogoro kati ya wakulima na wafugaji ni ukame uliokumba kijiji hicho na maeneo mengine nchini.

Alisema ukame ulisababisha wafugaji kuingia katika Wilaya ya Siha kutafuta malisho kwenye mashamba ya wakulima na kusababisha mgogoro, jambo lililosababisha ng'ombe 400, mbuzi na kondoo 1,300 wa wafugaji kijijini hapo kutaifishwa.

"Baada ya mifugo kutaifishwa Agosti mwaka 2022, wafugaji walipata hasara kubwa kwa kuwa waliitegemea mifugo hiyo kwa shughuli za uchumi. Wanawake kutoka kijijini kwetu walikuwa wanaenda kwenye mashamba ya wakulima kwa ajili ya vibarua na wanarudi na chakula kama viazi, lakini baada ya mgogoro haikuwa hivyo tena," alisema Nasalei.

Wakulima wa kijiji cha Ngarenairobi (Siha), wanasema elimu ya mabadiliko ya tabianchi imewasaidia katika maisha yao na kupanga mambo kulingana na uhalisia.

Donald Ilomo (51), baba wa watoto watano na mkulima wa maharage, ngano, alizeti na viazi alisema mabadiliko ya tabianchi yamesababisha athari kubwa na kuchangia mgogoro kati ya wafugaji na wakulima.

Ester Laizer (22), mkazi wa kijiji cha Elerai anayejishughulisha na ufugaji wa kuku, ng'ombe na mbuzi aliliambia Mwananchi kuwa afadhali hivi sasa hali imetulia baada ya kusuluhishwa.

"Kabla ya mgogoro jamii hizi mbili tulikuwa tunashirikiana katika mambo ya kiuchumi kama kwenda kwenye masoko na kwenda kulima kwenye mashamba yao na kwa sasa hali hiyo imerejea kutokana na hatua za usuluhishi zinazoendelea kati ya jamii zetu," alisema.

Kwa kutambua umuhimu wa kupambana na mabadiliko ya tabianchi, Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL) kwa kushirikiana na Taasisi ya Bill and Melinda Gates, Taasisi ya CarbonTanzania na Clouds Media Group wameandaa mdahalo wa kujadili kwa kina juu ya hali hiyo inayoutesa ulimwengu.

Mwananchi imeandaa mdahalo huo kupitia chapa yake ya Jukwaa la Fikra inayolenga kutafuta suluhisho la masuala mbalimbali yanayoikabili jamii, hususani yale yanayohitaji fikra na suluhu ya pamoja.

Mada katika mdahalo huo ni Mabadiliko ya tabianchi ‘kutambua mwitikio na suluhisho kwa Watanzania’ na mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Makamu wa Rais wa Tanzania, Dk Philip Mpango ambaye ofisi yake ndiyo inasimamia masuala ya mazingira nchini.

Mdahalo utafanyika Juni mosi katika hoteli ya Serena, jijini Dar es Salaam kuanzia saa 10 jioni hadi saa tatu usiku na utakuwa ukirushwa mubashara kupitia Clouds Tv.