Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Miradi ya tozo za simu, Uviko-19 sasa yazua balaa

Muktasari:

Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, Sahili Geraruma amewata wasimamizi wa miradi iliyojengwa chini ya kiwango kujitathimini na kujipima kama wanamudu nafasi hizo, vinginevyo wapishe.

Dar es Salaam. Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, Sahili Geraruma amewata wasimamizi wa miradi iliyojengwa chini ya kiwango kujitathimini na kujipima kama wanamudu nafasi hizo, vinginevyo wapishe.

Pia, ametoa wiki mbili kufanyiwa kazi dosari zilizojitokeza huku akitoa maelekezo kwa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kufanya ufuatiliaji.

Geraruma alitoa maelekezo hayo juzi, baada ya kusitisha uzinduzi wa miradi miwili katika Halmashauri ya Temeke, ukiwamo wa vyumba saba vya madarasa ya shule ya sekondari Karibuni, uliotekelezwa kupitia mpango wa maendeleo kwa ustawi wa Taifa na mapambano dhidi ya Uviko-19.

Mradi mwingine uliokataliwa kati ya miradi mitano ni majengo mawili ya upasuaji na lingine la kujifungulia watoto katika Hospitali ya Kilakala iliyojengwa kwa fedha za miamala ya simu.

“Kujengwa chini ya kiwango ni moja ya sababu zinazonifanya nisizindue miradi hii, lakini viongozi wa wilaya wanapaswa kujitathimini kama wanazitendea haki nafasi walizopewa,” alisema Geraruma.

“Mradi umejengwa chini ya kiwango, ukiangalia madirisha yamepinda, lakini baadhi ya majengo yana nyufa vilevile, hata marumaru zimetofautiana size, jambo ambalo ni tofauti na makubaliano yaliyoingiwa na mkandarasi,” alisema.

Kuhusu ujenzi wa majengo mawili katika Hospitali ya Kilakala, kiongozi huyo alibaini mkanganyiko wa nyaraka za kiwango cha fedha, huku akibainisha saizi ndogo tofauti na makubaliano ya mkataba.

Hata hivyo, Geraruma alikubali kuzindua mradi wa greda wenye thamani Sh776 milioni, katika halmashauri hiyo kwa sharti la kutokuanza kufanya kazi hadi dereva wa gari hilo apewe mkataba.

“Tunakubali kuzindua greda hili, lakini tunawataka lisianze kufanya kazi hadi mtakapotekeleza matakwa ya kisheria, kwa kuhakikisha dereva anakuwa na mkataba wa ajira, lolote linaweza kutokea,” alisema Geraruma.


Miradi ya halmashauri iliyokataliwa

Katika halmashauri za Ubungo, Kinondoni na Ilala kiongozi huyo aligoma kuzindua miradi mbalimbali kwa madai ya kasoro, huku akiitaka Takukuru kufanya uchunguzi.

Wilaya ya Kinondoni, Mwenge huo ulitembelea miradi mitatu yenye thamani ya Sh3.9 bilioni, ukiwamo wa Shule ya Sekondari ya Daniel Chongolo, Klabu ya Wapinga Rushwa katika Shule ya Sekondari Bunju A na Kikundi cha Vijana cha Fancing Wire Bunju B, kilichokuwa kimepata mkopo wa asilimia kumi kutoka katika halmashauri hiyo.

Miradi mingine ni Barabara ya Mkwajuni – Mbweni kwa kiwango cha lami yenye urefu wa kilomita saba, Shule ya Msingi ya Michaeli Urio iliyoko Kunduchi, wodi ya wazazi na maabara katika Zahanati ya Kawe.

“Mradi wa wodi ya wazazi na maabara katika Zahanati ya Kawe, naagiza Takukuru kufanya uchunguzi kutokana na kasoro zilizopo kwenye nyaraka za ununuzi,” alisema Geraruma.

Katika Wilaya ya Ubungo, mbio hizo zilikagua na kutembelea miradi yenye thamani ya Sh2.8 bilioni, huku akikataa kuzindua mradi wa Kikundi cha Vijana Wanaoendesha Bajaji wenye thamani ya zaidi ya Sh800 milioni kutokana na kasoro zilizobainika.

Miradi iliyokaguliwa katika wilaya hiyo ni Kituo cha Afya Goba, Kituo cha DMI Spring of Hope kinacholea wasichana waathirika wa matukio ya biashara haramu na unyanyasaji, Kibamba pamoja na barabara ya Msuguri – Bwawani Kata ya Msigani na ujenzi wa madarasa katika shule ya Sekondari Mashujaa Sinza.

Wilayani Ilala Mwenge huo ulitembelea na kukagua miradi saba yenye thamani ya Sh6.6 bilioni, iliyohusisha ujenzi wa madarasa 12 na matundu 10 ya vyoo katika Shule ya Sekondari Bungulo, ujenzi wa Daraja la Ulongoni A, mradi wa kijamii Kinyelezi Park na Kikundi cha Vijana Banana Vingunguti.

Miradi mingine ni kiwanda kidogo cha vijana cha kusaga unga wa lishe cha Long Life 1, Kitunda na ujenzi wa kituo cha afya Kipunguni.

Hata hivyo, alikataa kuzindua mradi wa Shule ya Sekondari Bangulo na kuiagiza Takukuru kufanya uchunguzi kutokana na kasoro, zikiwemo nyaraka za malipo ya fedha kinyume na utaratibu.