Mirungi yatumika hadharani, DCEA yakiri tatizo ni kubwa
Muktasari:
- Yaeleza kuwa dawa hizo zinaingizwa kwa wingi kutoka nchi jirani huku wasafirishaji wakibuni mbinu mpya kila uchao, ikiwemo kuzisafirisha kwenye maboksi yenye barafu wakidai kuwa ni samaki wabichi.
Dar es Salaam. Wakati hatua mbalimbali zikiendelea kuchukuliwa kudhibiti matumizi ya dawa za kulevya aina ya mirungi, imebainika kuwa dawa hizo kwa sasa zinatumika hadharani kwenye sehemu za starehe, hali inayoibua wasiwasi wa kuongezeka kwa uraibu, matatizo ya afya ya akili na magonjwa ya moyo katika jamii.
Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), kemikali ya cathinone iliyopo kwenye mirungi ina sifa zinazofanana na zile za dawa za kusisimua mfumo wa fahamu aina ya amphetamine, hivyo matumizi yake yanaweza kusababisha athari za kiafya kwa mtumiaji.
Uchunguzi wa Mwananchi umebaini kuwa licha ya matumizi ya mirungi kupigwa marufuku kisheria, baadhi ya watumiaji wamekuwa wakitumia dawa hizo kwenye maeneo ya starehe, wakidai mazingira hayo huwapa uhuru wa kuitumia bila kuvutia macho ya watu wengi.
Baadhi ya maeneo yanayotajwa na watu wanaofahamu mwenendo huo ni Tabata, Sinza, Mabibo, Manzese na Kinondoni, ambako matumizi ya mirungi hudaiwa kuonekana kwenye baa nyakati za usiku.
Kwa mujibu wa baadhi ya watu wanaofahamu biashara hiyo, bei hutegemea ubora wa mirungi, ambapo kichana kimoja huuzwa kati ya Sh20,000, huku aina inayotajwa kuwa ya daraja la juu ikifikia hadi Sh40,000.
Mmoja wa watumiaji wa mirungi, ambaye Mwananchi limehifadhi jina lake, amesema hupendelea kuitumia akiwa kwenye baa kutokana na mazingira ya burudani.
"Muziki, mazingira ya baa na matumizi ya mirungi vinanifanya nijisikie tofauti. Tofauti na sigara, mirungi haina harufu kali, hivyo si rahisi watu kugundua mtu anaitumia," amesema.
Mtumiaji mwingine amesema hupendelea kuitafuna kwenye baa kwa madai kuwa hujihisi salama zaidi akiwa sehemu yenye watu wengi kuliko maeneo mengine.
"Nikiwa baa nahisi kuna usalama zaidi kwa sababu watu ni wengi na kila mtu anajali mambo yake," amesema.
Hata hivyo, amekiri kuwa vijana wengi huanza kutumia mirungi kwa majaribio, lakini baadaye hujikuta wakishindwa kuacha.
DCEA yakiri tatizo ni kubwa
Akizungumza na Mwananchi, Kamishna Jenerali wa DCEA, Aretas Lyimo, amekiri kuwa matumizi ya mirungi yameongezeka kwa kasi nchini, huku dawa hiyo ikichukua nafasi ya heroini, kokeni na skanka ambazo zimeanza kupatikana kwa shida kutokana na operesheni za kudhibiti biashara ya dawa za kulevya.
Amesema uchunguzi uliofanywa katika mikoa ya Dar es Salaam, Tanga, Kilimanjaro, Arusha, Dodoma na Manyara umebaini kuwa matumizi ya mirungi yamekuwa makubwa, huku watumiaji wengi wakiwa ni wale waliokuwa wakitumia dawa nyingine za kulevya.
Amesema ongezeko hilo linachangiwa na uzalishaji mkubwa wa zao la mirungi nchini Kenya, ambako ni halali kulimwa na kutumiwa, hali inayorahisisha kuingizwa kwake nchini kupitia njia zisizo rasmi.
Kwa mujibu wa Kamishna Jenerali, uchunguzi umebaini kuwepo kwa baa za vichochoroni katika maeneo mbalimbali ambako mirungi hutumiwa kwa kificho, huku baadhi ya baa kubwa zikiwa na vyumba maalumu vya VIP vinavyotumiwa na wateja maalumu.
Amesema baadhi ya maeneo yaliyobainika kuwa na matumizi makubwa ni Magomeni, Kinondoni, Sinza na Ubungo jijini Dar es Salaam, huku mkoa wa Arusha ukitajwa kuwa miongoni mwa maeneo yenye idadi kubwa ya sehemu hizo.
"Kuna baa nyingi zenye vyumba vya VIP ambako watu maalumu huingia, wakati mwingine zikiwa na walinzi wanaozuia wasiokuwa wahusika. Hata baadhi ya watumishi wa Serikali wamebainika kuwa miongoni mwa wanaotumia mirungi katika maeneo hayo," amesema.
Lyimo amesema DCEA imeimarisha operesheni katika mipaka baada ya kubaini kuwa wafanyabiashara wamekuwa wakibuni mbinu mpya za kuingiza mirungi kutoka Kenya.
Amesema mbali na kutumia pikipiki kupita kwenye njia za panya mpakani, baadhi ya wasafirishaji sasa hutumia boti zinazobeba mizigo kutoka Kenya na kuisimamisha katikati ya bahari kabla ya kuchukuliwa na vyombo vidogo usiku na kuingizwa nchini.
"Mpaka wa Tanzania na Kenya ni mrefu sana na wanaingia kupitia vipenyo mbalimbali. Lakini tumegundua pia mbinu mpya ambapo boti hukaa katikati ya bahari na watu huenda kuchukua mirungi kidogo kidogo usiku," amesema.
Aidha, amesema uchunguzi umebaini mbinu nyingine inayotumiwa kusafirisha mirungi kupitia mabasi ya abiria kwa kuificha kwenye maboksi yenye barafu na kudai kuwa ni samaki.
"Sasa wanachukua maboksi makubwa, wanaweka barafu nyingi halafu wanaficha mirungi ndani na kudai wanasafirisha samaki. Tumeshakamata mabasi yakiwa na mizigo ya aina hii. Tumewakamata wengi wanaotumia mbinu hiyo na kesi zao zinaendelea," amesema.
Amesema DCEA imekamata watu wengi pamoja na pikipiki zilizokuwa zikitumika kusafirisha mirungi, huku ikieleza kuwa taarifa kamili za operesheni hizo zitatolewa baada ya kukamilika kwa hatua za kisheria.
Zipi athari za mirungi?
Wataalamu wa afya wamesema mmea huo unaotafunwa na baadhi ya watu kwa lengo la kuongeza uchangamfu na kupunguza uchovu unaweza kuwa na madhara makubwa kwa afya ya akili, moyo na mfumo mzima wa mwili.
Wanasema ingawa baadhi ya watumiaji huona mirungi kama kichocheo cha kufanya kazi kwa muda mrefu au kuongeza umakini, matumizi ya mara kwa mara yanaweza kusababisha utegemezi wa kisaikolojia na kuongeza hatari ya magonjwa yasiyoambukiza pamoja na matatizo ya afya ya akili.
Mtaalamu wa magonjwa ya akili, Dk Emmanuel Nkya, amesema kemikali zilizopo kwenye mirungi, hususan cathinone na cathine, huchochea mfumo wa fahamu na kutoa hisia za uchangamfu kwa muda mfupi, lakini baadaye huacha athari zinazoweza kuwa kubwa.
"Mtumiaji anaweza kujisikia mwenye nguvu, mchangamfu na asiyehitaji usingizi kwa muda. Hata hivyo, matumizi ya muda mrefu yanaweza kuhusishwa na wasiwasi, kukosa usingizi, msongo wa mawazo na wakati mwingine matatizo makubwa ya afya ya akili kama psychosis," amesema.
Amesema baadhi ya watumiaji huanza kuona au kusikia vitu ambavyo havipo, huku wengine wakipoteza uwezo wa kufanya maamuzi sahihi kutokana na matumizi ya muda mrefu.
Kwa upande wake, daktari wa magonjwa ya moyo, Raphaela Lupogo, amesema mirungi huongeza mapigo ya moyo na shinikizo la damu, hali inayoweza kuwa hatari kwa watu wenye magonjwa ya moyo au walio katika hatari ya kupata magonjwa hayo.
"Tunawaona baadhi ya wagonjwa wenye shinikizo la damu ambalo linakuwa gumu kudhibiti kutokana na matumizi ya vichocheo mbalimbali, ikiwemo mirungi. Matumizi ya muda mrefu yanaweza kuongeza hatari ya kupata mshtuko wa moyo au kiharusi," amesema.
Mbali na moyo, wataalamu wanasema mirungi huathiri pia mfumo wa mmeng'enyo wa chakula kwa kupunguza hamu ya kula, kusababisha kufunga choo na wakati mwingine maumivu ya tumbo.
Mtaalamu wa lishe, Dk Salumu Mwinyi, amesema mirungi ina kemikali za asili za cathinone na cathine, ambazo huchochea mfumo wa fahamu na kumfanya mtumiaji ajisikie mwenye nguvu na uchangamfu kwa muda mfupi.
"Kadri mtu anavyoendelea kutumia, mwili na ubongo huzoea kemikali hizo na kumfanya ashindwe kuziacha kirahisi," amesema.
Amesema matumizi ya muda mrefu yanaweza kupunguza hamu ya kula na kusababisha utapiamlo, kupungua uzito na kudhoofika kwa afya.
Mbali na hilo, amesema mirungi inaweza kuongeza mapigo ya moyo na shinikizo la damu, hivyo kuongeza hatari ya magonjwa ya moyo na kiharusi, hasa kwa watu wenye vihatarishi vingine vya kiafya.
"Pia, inaweza kuathiri mfumo wa mmeng'enyo wa chakula na kusababisha matatizo kama kufunga choo kutokana na kemikali za tannins zilizopo kwenye majani hayo," amesema.
Kuhusu afya ya uzazi, Dk Mwinyi amesema tafiti mbalimbali zinaonyesha matumizi ya muda mrefu yanaweza kupunguza ubora wa mbegu za kiume.
Kwa wanawake wajawazito, amesema matumizi ya mirungi yanaweza kuongeza hatari ya mtoto kuzaliwa na uzito mdogo pamoja na changamoto nyingine za ujauzito.
Mwanasaikolojia Modesta Kimonga amesema pamoja na madhara ya kiafya, matumizi ya mirungi yanaweza kuathiri mahusiano ya kifamilia na uzalishaji kazini kutokana na utegemezi unaojengeka kwa baadhi ya watumiaji.
"Baadhi ya watu hufikia hatua ya kuamini hawawezi kufanya kazi au kuendelea na shughuli zao za kila siku bila kutafuna mirungi. Hapo ndipo utegemezi wa kisaikolojia unapoanza kujitokeza," amesema.