Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mitandao jamii yatajwa kuwa nguzo ya uchumi wa kidijitali vijijini

Mwenyekiti wa Kamati ya Programu Shule ya Mitandao Jamii Tanzania Dkt. Jabhera Matogoro akiongea katika kongamano la Tano la Shule ya Mitandao Jamii Tanzania lililofanyika mjini Tarime, mkoa wa Mara hivi karibuni.

Muktasari:

  • Matumizi bora ya teknolojia na majukwaa ya kidijitali yanaweza kuongeza kipato cha wananchi na kuimarisha uchumi wa jamii

Dar es Salaam. Wadau wa mawasiliano, teknolojia na maendeleo ya jamii wamekutana mjini Tarime, Mkoa wa Mara kujadili namna mitandao jamii inavyoweza kuchochea ukuaji wa uchumi wa kidijitali, kuongeza fursa za ajira na kuharakisha maendeleo ya kijamii katika maeneo ya vijijini nchini.

Mwenyekiti wa Kamati ya Programu ya Shule ya Mitandao Jamii Tanzania, Dk Jabhera Matogoro amesema kongamano la Tano la Shule ya Mitandao Jamii Tanzania (TSCN 2026) linawakutanisha washiriki zaidi ya 50 kutoka maeneo mbalimbali ya Tanzania na Kenya.

Amesema kongamano hilo limeandaliwa na Chuo cha Ufundi cha Tanzania cha Mitandao Jamii (TCNPC) kwa kushirikiana na Chama cha Ushirika cha Mawasiliano cha Tarime, likiongozwa na kaulimbiu isemayo:

“Kutoka kuunganishwa kwenye intaneti kwenda uzalishaji wa kiuchumi: Mitandao Jamii Inayochochea Uchumi wa Kidijitali Jumuishi kuelekea Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.”

Akizungumza katika kongamano hilo leo Jumapili Juni 7, 2026, Dk Matogoro amesema lengo ni kuhamasisha matumizi ya huduma za mawasiliano kama nyenzo ya uzalishaji, ubunifu, biashara, elimu na maendeleo ya kijamii, badala ya kutumika kwa mawasiliano pekee.

“Kongamano hili linaonesha namna intaneti na teknolojia za mawasiliano zinavyoweza kuwa kichocheo cha maendeleo ya kiuchumi na kijamii, hususan katika maeneo ya vijijini,” amesema.

Amesema washiriki wa kongamano hilo ni pamoja na wataalamu wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama), viongozi wa mitandao jamii, watunga sera, watafiti, wabunifu wa teknolojia, viongozi wa vyama vya ushirika, vijana, taasisi za umma na binafsi pamoja na wadau wa maendeleo.

Dk Matogoro amesema kongamano hilo pia linatoa fursa kwa washiriki kujifunza namna mitandao jamii inavyoweza kusaidia kupunguza pengo la kidijitali kwa jamii ambazo bado hazijafikiwa kikamilifu na huduma bora za mawasiliano na intaneti.

Aidha, amesema limeweka mkazo katika Maendeleo ya Elimu ya Sayansi, Teknolojia, Uhandisi na Hisabati (STEM) kama msingi wa kuwaandaa vijana kushiriki kikamilifu katika uchumi wa kisasa wa kidijitali.

“Kupitia Kituo cha STEM Dodoma kilichoanzishwa kwa ushirikiano kati ya TCNPC na STEMpower, wanafunzi na vijana wanapata mafunzo kwa vitendo kupitia maabara za kisasa, roboti na teknolojia nyingine zinazokuza ubunifu na ujuzi wa kidijitali,” amesema.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Masoko na Ushirikishwaji wa Umma wa Chuo cha Ufundi cha Tanzania cha Mitandao Jamii, Alhaji Sefu, amesisitiza umuhimu wa matumizi sahihi ya mitandao ya kijamii katika kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

Amesema majukwaa ya kidijitali hayapaswi kuonekana kama njia za mawasiliano pekee, bali ni nyenzo muhimu zinazoweza kutumika kujifunza, kubadilishana maarifa, kujenga mitandao ya kitaaluma na kutangaza fursa mbalimbali za maendeleo.

“Mitandao ya kijamii ina uwezo mkubwa wa kuwawezesha wananchi kupata taarifa, maarifa na fursa zinazoweza kuboresha maisha yao. Ni muhimu kuitumia kwa tija ili kuchangia maendeleo ya mtu mmoja mmoja na jamii kwa ujumla,” amesema Sefu.

Amesema vijana, wajasiriamali na viongozi wa jamii wanapaswa kutumia majukwaa ya kidijitali kukuza shughuli zao za kiuchumi kwa kutangaza bidhaa na huduma, kufikia masoko mapya na kuongeza thamani ya kazi zao.