Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mitihani ya utabibu yafutwa nchi nzima

Muktasari:

  • Hatimaye Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (Nacte), limeyafuta matokeo yote ya mitihani ya nadharia ya programu ya utabibu ngazi ya Diploma (NTA level 5) kwa vyuo vyote nchini baada ya kuthibitika mitihani hiyo ilivuja.


Moshi. Hatimaye Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (Nacte), limeyafuta matokeo yote ya mitihani ya nadharia ya programu ya utabibu ngazi ya Diploma (NTA level 5) kwa vyuo vyote nchini baada ya kuthibitika mitihani hiyo ilivuja.

Kutokana na kufutwa kwa matokeo hayo, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto inayosimamia vyuo vinavyokadiriwa kufika 147 nchi nzima, imeagiza kuandaliwa mitihani mingine ndani ya wiki sita.

Hata hivyo, Katibu Mtendaji wa Nacte, Dk Adolf Rutayuga alipoulizwa na Mwananchi kwa simu jana, alimtaka mwandishi awasiliane na Wizara ya Afya.

Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Profesa Abel Makubi alipopigiwa simu alimtaka mwandishi kumtumia ujumbe akisema yuko kwenye kikao na baada ya kutumiwa hakujibu ujumbe huo.

Kufutwa kwa mitihani

Hata hivyo, Wizara ya Afya kupitia barua yake ya jana yenye kumbukumbu LB.205/262/01A/11 iliyotumwa kwa wakuu wa vyuo vya Afya, ilisema Nacte imefuta matokeo hayo baada ya kupokea taarifa ya uchunguzi ya wizara.

Barua hiyo yenye kurasa mbili ilikuwa na vipengele vinne na kimojawapo ni kuwataarifu wakuu hao wa vyuo vya afya kuwa matokeo ya mitihani hiyo iliyofanyika kwa siku tatu Agosti mwaka huu kuwa yamefutwa.

Mitihani inayodaiwa kuvuja ni ya masomo ya RCH, Counselling, Internal Medicine, Pediatrics, Surgery na Obstetrics au Gynecology ambayo ilifanyika Agosti 16 hadi 18 na inaelezwa ilivuja katika kiwango cha kuvunja rekodi ya uvujaji mitihani.

“Baraza limekiri kupokea taarifa ya kamati ya uchunguzi iliyowasilishwa na WAMJW iliyohusu kuvuja na kusambaa kwa mitihani ya nadharia (theory examinations) ya programu ya utabibu ngazi ya tano, NTA level 5,” ilisema taarifa.

“Aidha baraza kupitia sheria ya Baraza, Sura 129 na kanuni za mitihani kifungu 33(1) (iii), ya 2004, limefuta matokeo ya mitihani ya kuandika kwa masomo yote ya programu ya utabibu ngazi ya tano, NTA level 5,” ilisisitiza barua hiyo.

Kupitia barua hiyo iliyotiwa saini na Fadhili Mussa Lyimo kwa niaba ya Katibu mkuu Wizara ya Afya, wizara imeagiza kuandaliwa kwa mitihani hiyo ndani ya wiki sita kuanzia Novemba 3, 2021.

“Mitihani hiyo itafanyika sambamba na mitihani ya marudio (supplementary examinations) kwa programu nyingine za afya nchi nzima,” ilisema barua hiyo.

“Napenda kuwajulisha kuwa WAMJW imepokea maelekezo ya Nacte na maandalizi ya mitihani hiyo yameanza. Ratiba ya mitihani itatolewa baada ya kukamilisha maandalizi,” ilisisitiza barua hiyo na kuongeza:

“Hivyo nawaelekeza (wakuu wa vyuo) kuwajulisha wanafunzi wote wa ngazi ya tano (NTA level 5) wa programu ya utabibu na wanafunzi wanaosubiri mitihani ya marudio kuanza kujiandaa kwa ajili ya mitihani hiyo.”

Katika barua hiyo, wizara pia ilisema ilikuwa imepokea barua ya Nacte ya Novemba 2, 2021 kwamba kikao cha 78 cha Baraza kilikuwa kimeridhia na kupitisha rasmi matokeo ya mitihani ya programu ya afya na sayansi shirikishi.

Mwananchi ndilo gazeti pekee lililokuwa la kwanza kuandika taarifa za kuvuja kwa mitihani hiyo ambayo inaelezwa kuwa baadhi ya wanafunzi walitumiana taarifa hizo kupitia mitandao ya Whatsapp na Telegram kabla ya mamlaka husika kuzuia matokeo hayo.

Wiki iliyopita, Waziri wa Afya, Dk Dorothy Gwajima ambaye wizara yake ilichukua hatua mapema baada ya kupokea taarifa za kuvuja kwa mitihani, aliahidi wizara yake ingetoa taarifa wiki hii baada ya uchunguzi kukamilika.

Kwa mujibu wa Waziri Gwajima, ambaye wadau wamepongeza hatua ya wizara yake kuchukua hatua za haraka, hadi sasa wizara imeshaunda kamati ambayo itaandaa ripoti na kuikabidhi kwake na yeye ataisoma kwa wananchi.

“Nasubiri taarifa ya kamati iliyoundwa tusome, tuikubali, tuijadili tuwaeleze wananchi kilichotokea na hatua zichukuliwe kwa sababu hilo ni jambo baya walilolifanya. Taarifa ya awali inaonyesha kweli huo mchezo umefanyika,” alisema.

“Kuna baadhi ya walioasisi (uvujishaji) wameshabainika, sasa kwa sababu ni suala la kisheria lazima waende wazame zaidi waletwe. Lakini kwa vyovyote vile kuna tatizo limetokea na matatizo yanafanywa na watu,” alisema na kuongeza:

“Watu wema wapo na wabaya wapo. Wamelifanya (tatizo la kuvuja mitihani) wamelitengeneza, sasa sisi tunasubiri taarifa hiyo (ya kamati) kwa hiyo tukabidhiwe sasa tuchukue hatua mubashara na wananchi wajue.

“Kwa taarifa nilizonazo sasa hivi kufikia Jumatatu ijayo (Novemba 1) tutakuwa tumeipata hiyo taarifa na tutaongea na vyombo vya habari.’’