Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Siri mitihani ya utabibu ilivyovuja

Siri mitihani ya utabibu ilivyovuja

Muktasari:

  • Wakati Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Dorothy Gwajima akitangaza kiama kwa watakaothibitika kuvujisha mitihani ya stashahada kwa matabibu wa afya, mbinu iliyotumika kuvujisha imebainika.


Moshi/Morogoro. Wakati Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Dorothy Gwajima akitangaza kiama kwa watakaothibitika kuvujisha mitihani ya stashahada kwa matabibu wa afya, mbinu iliyotumika kuvujisha imebainika.

Vyanzo mbalimbali vimedokeza mitihani hiyo ilipigwa picha kwa kutumia simu janja wakati inafungwa kusambazwa katika vyuo vya afya vinavyosimamiwa na wizara, na mitihani hiyo kusambaa kupitia mitandao ya Whatsapp na Telegram.

Gazeti hili limefanikiwa kupata nakala ya mitihani hiyo iliyovuja na miongozo ya usahihishaji ikionyesha waliopiga picha mitihani hiyo na kuisambaza, walifanya hivyo kabla ya kuiweka kwenye bahasha na kuifunga kwa lakiri.

“Ukitizama hizo picha za mitihani iliyovuja na kuifanyia tathmini na mazingira yenyewe utagundua jambo moja kwamba ndio ilikuwa inawekwa kwenye bahasha au iliwekwa wakaifungua kabla ya lakiri,” imedokezwa.

Mazingira ambayo mitihani hiyo ilipigwa picha kwa mujibu wa nakala ambazo gazeti hili linayo, yanaonyesha ni kwenye chumba au ofisi yenye meza ambapo mitihani hiyo kwa chini zinaonekana bahasha zilizotumika kuifungia.

Mitihani inayodaiwa kuvuja ni ya masomo ya RCH, Counselling, Internal Medicine, Pediatrics, Surgery na Obstetrics au Gynecology ambayo ilifanyika Agosti 16 hadi 18 na inaelezwa ilivuja katika kiwango cha kuvunja rekodi ya uvujaji mitihani.

Inadaiwa mitihani hiyo ilivuja katika kiwango ambacho baadhi ya wanafunzi walitumiana mitihani na mwongozo wa usahihishaji kwa njia ya Whatsapp, Telegram na barua pepe huku baadhi ya vyuo vikidaiwa kuinunua.

Tayari Wizara ya Afya inayosimamia vyuo vya afya 147 nchi nzima na ambayo ndio ilitunga mitihani kupitia Kurugenzi yake ya mafunzo, imeagiza kuzuiwa kutolewa kwa matokeo hayo ya mitihani ngazi ya NTA 5 ambayo ni Diploma.

Waziri Gwajima

Akizungumza akiwa mjini Morogoro jana, Waziri wa Afya, Dk Gwajima alisema hadi kufikia Novemba 1, mwaka huu atakuwa ameweka wazi watu wote waliohusika na udanganyifu wa mitihani hiyo ya utabibu nchi nzima.

Dk Gwajima alitoa kauli hiyo ya kwanza rasmi ya Serikali akihojiwa na mwandishi wa gazeti hili baada ya kuzindua Kituo cha Elimu ya Afya kwa njia ya masafa na kusema hatua kali za kisheria zitachukuliwa kwa wote watakaobainika kuhusika.

Waziri Gwajima alisema hadi sasa wameshaunda kamati itakayoandaa ripoti na kuikabidhi kwake na yeye ataisoma kwa wananchi.

“Kuna baadhi ya waliouasisi (uvujishaji) wameshabainika, sasa kwa sababu ni suala la kisheria lazima waende wazame zaidi, matatizo yanafanywa na watu,” alisema na kuongeza:

“Watu wema wapo na wabaya wapo, ni jambo baya, taaluma hii ni ya kuponya watu. Ni taaluma ya kutibu watu halafu mtu anakwenda kufanya mambo ya hovyo kama hayo. Haivumiliki na haikubaliki,” alisema.

Ingawa hakutaja idadi ya vyuo vyote vya afya nchini ingawa ni karibu 147, Dk Gwajima alisema vyuo hivyo ndio vinavyotarajiwa kutoa watumishi wa kada ya afya wanaokwenda kuwahudumia Watanzania hmaeneo mbalimbali nchini.

Akizungumzia kuhusu Kituo cha Elimu Masafa aliwataka viongozi wa kituo hicho kuhakikisha wanaboresha mifumo ya chuo ili waweze kuzalisha watumishi walio bora huku mkurugenzi wa Mafunzo, Dk Saitore Laizer akitaja faida za chuo.

Naye Mkuu wa kituo hicho, Ndementria Verman, alisema ujenzi wa kituo hicho umeongeza idadi ya watu kwenda kujifunza na kujiendeleza.