Mjadala kauli tata makada wa CCM

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), Justine Masejo

Muktasari:

  •  Kauli za makada wawili wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Jijini Arusha na Jijini Dar es Salaam zinazotafsiriwa ni za kuchochea uhalifu dhidi ya wafuasi wa vyama vingine vya siasa, zimeibua mijadala katika mitandao ya kijamii.

  

Moshi/Arusha. Kauli za makada wawili wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Jijini Arusha na Jijini Dar es Salaam zinazotafsiriwa ni za kuchochea uhalifu dhidi ya wafuasi wa vyama vingine vya siasa, zimeibua mijadala katika mitandao ya kijamii.

Moja ya kauli hizo ni ile inayodaiwa kutolewa na kijana wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) Jijini Arusha, Godlizen Kisila akitamba yeye alikuwa kiongozi wa kikosi cha chinjachinja.

Kauli ya Kisila ambaye video yake imesambaa kwa kasi katika mitandao ya kijamii hasa Twitter, Whatsapp, Telegram, Facebook na Instagram, inamuonyesha akizungumza mbele ya wajumbe akiomba kura na katika kuomba huko alisema;

“Ndugu zangu naitwa Godlizen Kisila. Niliwahi kuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM Wilaya ya Moshi mjini. Wakati mzee Massawe anashinda na mimi ndio nilishinda uenyekiti wa vijana, sare za CCM watu walikuwa hawavai.

“Kile kikosi cha chinjachinja mimi ndio nilikuwa nakiongoza. CCM hoyee. Ndugu zangu nisiwe msemaji sana naombeni kura zenu,” alisema Kisila, kauli ambayo baadhi ya wadau wa siasa wanaihusisha na utesaji uliokuwa ukitokea Jijini Arusha.

Hata hivyo, akizungumza na Mwananchi jana kuhusu hilo, alisema tafsiri ya video ile imepotoshwa na baadhi ya watu wasio na mapenzi mema na CCM, na kwamba chinjachinja alimaanisha kadi ya kupigia kura.

“Hiyo video inapotoshwa tu, mimi nilisema chinjachinja nikimaanisha kadi za kupigia kura ndiyo tulitumia kuchinjia wapinzani na CCM kuchukua dola, sikumaanisha eti mauaji bali kura pekee,” alisema kada huyo.

Mkazi wa jijini Arusha, Ernest Siku alisema Jeshi la Polisi linapaswa kuifanyia kazi video hiyo, akiihusisha na matukio ya watu waliokuwa wakichinjwa na kutupwa mitaroni katika uchaguzi wa 2020 hasa wilayani Arumeru.

“Katika mauaji yale, polisi walidai wanatafuta watuhumiwa waliotekeleza uhalifu huo, lakini hadi leo hakuna mafanikio, lakini uzuri huyu mjumbe wa CCM amekiri mbele ya umati wa watu yeye ndio alikuwa kiongozi wa hilo kundi.

“Tunaomba polisi wamkamate na kumhoji kwa kukiri kwake ili angalau kuweka amani mioyoni mwa wakazi wa Arusha walioumizwa na matukio ya ajabu ajabu, utesaji na umwagaji wa damu yaliyotokea siku za nyuma,” alisisitiza.

Mbali na video hiyo, katika mitandao ya kijamii pia kumesambaa video nyingine ikimuonyesha kijana wa UVCCM akitamba kuwa kazi ya vijana wa umoja huo ni kuharibu, halafu CCM chenyewe kitawajibika kutengeneza na kuomba radhi.

“Tunaelewana vizuri? Mimi kwa bahati mbaya natoaga kauli zangu mtu akizingua tunamwaga maji halafu tutarudi kuomba radhi. Mmenielewa vizuri hapo. Kazi ya UVCCM ni kuharibu na kazi ya chama ni kutuombea radhi,” anasikika akisema.

“Kazi ya UVCCM ni nini?” aliwauliza aliokuwa akizungumza nao na kujibiwa kuwa ni kuharibu na kazi ya chama ni kutengeneza na akafafanua kuwa wajibu wa kutengeneza ni wa Umoja wa Wazazi na Umoja wa Wanawake (UWT).

RPC, UVCCM Arusha wafunguka

Alipotafutwa kuzungumzia video ya kada wa CCM Jijini Arusha, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), Justine Masejo alisema hakuwa ameiona video hiyo, hivyo akaomba kupewa muda wa kuifanyia kazi.

“Hii video ndio kwanza nimeiona kwa sababu nilikuwa bize na ugeni wa mkutano wa kimataifa wa utalii. Naomba niulize wenzangu walionitangulia waliokuwepo enzi za chaguzi hizo na matukio yaliyotokea na endapo tukibaini ina mahusiano na mauaji ya watu basi tutamchukulia mhusika hatua kali za kisheria,” alisema.

Akizungumzia video hiyo, Katibu wa UVCCM mkoani Arusha, Ibrahim Kijanga alisema bado wanaitafakari kabla ya kutoa tamko rasmi, akisema matamshi hayo yasitafsiriwe kama ndiyo msimamo wa chama.

“Naomba isitafsiriwe kama ni msimamo wa chama, hatuhusiki na chochote, tunaitafakari ikibidi tutamuita mhusika kujua alikuwa anamaanisha nini hasa kusema hivyo, CCM haina tabia hizo,” alisema Kijanga.

Akilizungumzia hilo, Katibu wa Chadema mkoani Arusha, Reginald Massawe alidai kuwa kauli ya kada huyo inathibitisha malalamiko yao ya muda mrefu juu ya CCM kuhusika na matukio mbalimbali ya kihalifu, hasa yanayolenga kudhoofisha vyama vya upinzani.

“Tumekuwa na malalamiko kwa Serikali na hasa CCM kuendesha genge la vijana wanaoratibu matukio ya kihalifu bila shaka, sasa ushahidi tunao hasa wenye mawazo tofauti, siasa na demokrasia.

“Kwa ushahidi huu (video), warudi tu na wawe watu wema na kama wanatekeleza majukumu yao hawana haja ya kuwa na genge la chinjachinja,” alishauri.

Mwanasheria atoa neno

Akizungumzia kilichosemwa kwenye video hizo, Wakili wa Mahakama Kuu Tanzania, John Mallya alisema kisheria, mtu huyo ilipaswa awe amekamatwa na vyombo vya dola.

“Chadema wamekuwa na malalamiko ya muda mrefu ukizingatia wao ndio waathirika wakubwa wa matukio kama haya.

“Polisi wamekuwa wakidai wanatafuta wahalifu na upelelezi unaendelea. Huyu aliyejitokeza basi akamatwe na ahojiwe, inawezekana kuna anachokijua kuhusu matukio hayo,” alisema wakili Mallya.