Mjadala kauli ya Shabiby wananchi kukatwa Sh2,000 kwenye laini za simu

Muktasari:

  • Alipochangia mjadala wa bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa mwaka wa fedha 2024/2025, bungeni jijini Dodoma, Aprili 5, 2024, Shabiby alishauri kila mwenye simu akatwe Sh2,000 kila mwezi, wabunge, wafanyabiashara na wafanyakazi wa-katwe Sh10,000 kuchangia uanzishaji wa bima ya afya kwa wote.

Dar es Salaam. Wazo la Mbunge wa Gairo, Ahmed Shabiby la kutaka wananchi wachangie uanzishaji wa bima ya afya kwa wote kwa kuchangia Sh2,000 kila mwezi kupitia laini zao za simu limeibua mjadala wenye maoni tofauti.

Alipochangia mjadala wa bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa mwaka wa fedha 2024/2025, bungeni jijini Dodoma, Aprili 5, 2024, Shabiby alishauri kila mwenye simu akatwe Sh2,000 kila mwezi, wabunge, wafanyabiashara na wafanyakazi wakatwe Sh10,000 kuchangia uanzishaji wa bima ya afya kwa wote.

“Kuna wamiliki wa laini za simu nchini wapo milioni 72 makato yao kwa mwaka yataingiza Sh1.7 trilioni na zikijumlishwa Sh10,000 kwa mwezi za wabunge, wafanyabiashara na wafanyakazi Serikali itapata kwa mwaka Sh2 trilioni, zitasaidia kuwa chanzo cha mapato ya uhakika kwa Bima ya Afya kwa wote,” amesema Shabiby.

Novemba 2, 2023 Bunge lilipitisha Muswada wa Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote, ambao Rais Samia Suluhu Hassan aliusaini na kutangazwa kwenye Gazeti la Serikali Desemba mosi, 2023 kuwa sheria kamili.

Masikini hawataweza kulipia

Kufuatia pendekezo hilo, Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), John Heche kupitia mtandao wa kijamii wa X (zamani twitter) amepingana na wazo hilo akisema Tanzania ina mamilioni ya watu wanamiliki laini za simu lakini hawawezi kuweka hata Sh1, 000 kwa mwezi.

“Wanashindwa kuweka fedha kwa sababu ya umasikini mkubwa, lakini tatizo la nchi yetu si mapato, isipokuwa kuna ugumu katika usimamizi na matumizi ya fedha zinazokusanywa na ubadhilifu,” amesema.

Heche amesema Serikali kila mwaka inatumia bajeti kubwa kununua magari ya kifahari akitaja ni zaidi ya Sh600 bilioni, lakini hata uendeshaji wake unatumia gharama kubwa ikiwemo kununua vipuri na mafuta.

“Wamekuwa wakifanya safari nyingi ambazo hazina msingi na magari yanatumika ndani ya miaka mitatu, likiharibika kipuri kimoja wanapaki baada ya muda wanaliuza bei kidogo,” alidai Heche.

Si Heche tu anayepingana na wazo hilo, hata Dk Elizabeth Sanga, waziri wivuli wa Afya kutoka ACT-Wazalendo, amesema kuweka tozo kwa watu kupitia laini za simu haifai na si suluhisho.

“Msimamo wetu kama chama, Serikali iboreshe mifuko ya hifadhi ya jamii ili ivutie watu wa sekta binafsi wakawekeze kwa wingi ili waweze kuchangia kadri ya uwezo wao kwa sababu ilivyo sasa, wananchi wengi hawana uwezo na hawakopesheki,” amesema.

Amesema tatizo hilo lipo kwa watu waliojiajiri, kutengenezwe mfumo utakaowawezesha wananchi kujiunga kwa hiyari ili wapate bima ya afya kama fao.

“Lazima kuwe na njia ya watu kujiunga na mifuko ya hifadhi ya jamii kwa sababu kuna matatizo ya kugharimia huduma za afya, watu hawana pensheni na hawakopesheki,” amesema.

Hii haiwezekani

Akitoa mawazo yake kuhusu hilo, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Bima ya Sanlam Tanzania, Khamis Suleiman amesema haiwezekani kuanzisha mfuko wowote wa bima kwa kuwakata watu wengine ili wanufaike wengine na hakuna nchi inayoendesha mfuko wa bima ya afya kwa utaratibu huo.

Amesema wafanyakazi hata wakikatwa shilingi ngapi katika mishahara yao, kama usimamizi si mzuri mfuko utafilisika.

“Usimamizi ni jambo muhimu kuliko vingine vyote, kuna baadhi ya wafanyakazi wanaumia, mathalani mimi ni mwalimu na mke wangu ni mwalimu, watu tunaowahudumia ni haohao watoto, wa mke wangu ni wangu pia, lakini yeye anachangia asilimia tatu na mimi nachangia kiasi hicho, ilitakiwa mmoja kufutiwa achangie mtu mmoja tu,” amesema.

Suleiman amesema hiyo inatakiwa kuboreshwa ili wafanyakazi wasichangie mara mbili akieleza bima inavyofanya kazi inazingatia vitu viwili kama bei yako haiko sawa utapata tu hasara hata uchangie kiasi gani.

Wanaolalamikia walishasema huko nyuma mfuko huu hautadumu ifikapo 2025 utakuwa umefilisika. Walikuwa wameona kinachochangwa na kinachotumika haviendani,” amesema.

Amesema ili kufikia suluhu ya mfuko huo si wabunge kukaa na kupiga hesabu, wanaotakiwa kufanya hivyo ni wataalamu waliobobea katika sekta hiyo.

“Kuna watu wamekaa darasani miaka saba hadi 15 kazi yao ni hiyo,” amesema.

Mtaalamu mwingine wa masuala ya bima, Dk Anselmi Anselmi amesema huwezi kuweka kodi akatwe kila mtu ukapeleka kwenye mfuko unaohudumia watu asilimia nane ya Watanzania.

“Kabla ya kuweka ushuru uliotengwa kwenye bidhaa au huduma yoyote lazima kufanya utafiti za kiwango sahihi cha tozo kitaalamu, si makisio tu. Wanufaika wa tozo hiyo isiwe kundi dogo kwenye jamii,” amesema.

“Ikumbukwe tozo kwenye huduma za simu ilileta athari kubwa kipindi kifupi kilichopita, hivyo utafiti wa kutosha lazima wafanyike kabla ya kupendekeza tozo kwenye eneo ambalo tayari tul-ishaona athari mbaya kwenye manunuzi yake,” amesema.

“Tozo kwenye huduma za simu kwa ajili ya bima ya afya kwa wote inatumika nchi nyingine mfano Gabon. Lazima kufanya tathmini ya kina kabla ya kutekeleza jambo hilo,” amesema.

Dk Anselmi alishauri namna ya kuwezesha bima ya afya kwa wote ni kutumia kodi katika bidhaa haramu.

“Hizi ni kodi zinazowekwa kwenye bidhaa ambazo Serikali inalenga kupunguza matumizi yake au kama kuzitoza adhabu kwa athari zinazosababisha mfano sigara, pombe, vyakula vinavyoongeza hatari za magonjwa sugu kama kisukari na vitu vinavyoharibu mazingira kama matairi,” amesema.

Alishauri Serikali kutumia mifumo bunifu kama vile dhamana za kijamii, dhamana za utendaji kazi wa afya dhamana zilizounganishwa na bima bima iliyounganishwa na ustawi, dhamana za athari na makubaliano ya kodi ya watoa huduma.

“Wataalamu wahusishwe kuisaidia Serikali kuweka mifumo inayotekelezeka na yenye ufanisi katika kuhakikisha bima ya afya kwa wote inafanikiwa,” amesema.

Mipango iliyopo ya Serikali ni kuwezesha huduma za bima kwa wote kwa mapato yatokanayo na ushuru wa bidhaa kwenye vinywaji vyenye kaboni, vinywaji vikali, bidhaa za vipodozi, michezo ya kubahatisha, ada ya vyombo vya moto na mapato yatokanayo na ushuru wa miamala ya kielektroniki kwa kadri itakavyopendekezwa

Mbali na wataalamu wa bima, Oscar Mkude, mtaalamu wa uchumi naye amesema kodi kwenye laini za simu itakuwa na athari kwa watu wa maisha ya chini ambao ni wengi kwa sababu haiangalii kipato halisi cha wananchi.

“Kodi nzuri ni ile inayokatwa kwa kuzingatia kipato. Kwa namna alivyopendekeza (Mbunge) ni wazi wananchi wa kawaida wataumia inawezekana wazo ni zuri lakini utekelezaji wake unaweza kuwa changamoto,” amesema.

Amesema ili mpango huo uweze kutekelezeka ni lazimu kutengenezwe mfumo utakaosaidia kukata kodi hiyo kulingana na uwezo wa kipato cha mtu husika ili kujikita katika usawa.

“Laini za simu ziko milioni 70,  Watanzania tuko milioni 60, kwa kuzingatia anavyosema yeye maana yake kuna watu wana laini hadi tatu kwa hiyo watu watakuwa wanakatwa zaidi na haitakuwa sawa kodi nzuri ni ya kipato lakini simu si kipato,” amesema.

Mkude amesema jambo hilo linatakiwa kufanyiwa uchanganuzi wa kina kabla ya kutekelezwa kwa sababu wananchi wa kawaida ni kundi kubwa huwezi kulidharau na wanatumia simu kufanya mawasiliano katika mihangaiko yao.


Haki ya kila mtu

Dk Charles Sagoe Moses Mwakilishi wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Tanzania katika kuadhimisha siku ya afya duniani leo Aprili 7, 2024 amesema Tanzania inaendelea kujitahidi kufikia ajenda ya afya kwa wote ikizingatia haki za kila mtu na kuhakikisha zimejumuishwa katika sera na mikakati.

 “Ili kufikia maono ya afya kwa wote na kukuza haki za kila mtu kupata huduma za afya lazima tuongeze juhudi zetu katika kushughulikia mambo yanayoathiri afya ikiwa ni pamoja na umasikini kutokuwepo kwa usawa na miundombinu duni,” amesema.