Shabiby ataka fedha za bima kwa wote zikatwe kwenye laini za simu

Muktasari:

  • Ashauri vituo vya kutolea huduma – hospitali, zahanati na vituo vya afya – vinavyomilikiwa na Serikali vibinafsishwe Serikali ibaki na hospitali za rufaa yakee.

Dodoma. Mbunge wa Gairo (CCM), Ahmed Shabiby ameishauri Serikali kukata Sh2,000 kila mwezi kwenye laini za simu huku wabunge, wafanyabiashara na wafanyakazi wakikatwa Sh10,000 ili fedha hizo ziwe chanzo cha mapato kwa Bima ya Afya kwa wote.

Amesema kuna wamiliki wa laini za simu milioni 72 nchini ambao makato yao kwa mwaka yataingiza Sh1.72 trilioni na zikijumlishwa za Sh10,000 kwa mwezi za wabunge, wafanyabiashara na wafanyakazi, Serikali itapata kwa mwaka takribani Sh2 trilioni.

Shabiby amesema hayo leo wakati akichangia mapendekezo ya bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa mwaka wa fedha 2024/2025.

Pia, ameshauri vituo vya kutolea huduma – hospitali, zahanati na vituo vya afya – vinavyomilikiwa na Serikali vibinafsishwe kama ilivyo Abu Dhabi na Korea Kusini.

Ameshauri madaktari na wauguzi waliopo nchini wajiunge na kubinafsishiwa hospitali badala ya kuwa chini ya Serikali.

Shabiby alisema maana ya kutaka laini za simu zitumike kama chanzo cha mapato ni kutokana na anavyoona baada ya Bunge kupitisha muswada wa Bima ya Afya kwa wote na kusainiwa na Rais Samia Suluhu Hassan kuwa sheria, kuna hatari bima hiyo ikachangisha wananchi ambao awali walishindwa kuchangia hata Sh10,000 na Sh30,000 za mfuko wa CHF.

Kwa mujibu wa Shabiby, wanufaika wa bima katika Watanzania 100 ni watu wanane ambao wanalipa bima.

“Hasa ukiichukulia hii hatuna chanzo maalumu cha kupata pesa ambazo zinaweza zikasaidia wananchi wa vijijini na watu masikini pamoja na wananchi wa mijini, hata mijini wapo masikini wengi tu, tena hata zaidi ya hao wa vijijini,” amesema na kuongeza:

“Nimeona tulizungumzie bila woga, najua kuna mawazo tutatoa na watu watatukana kwenye mtandao, lakini acha watukane. Hii bima ya afya, ushauri ninaotoa tupende tusipende lazima tuingize chanzo cha muhimu ambacho tutakipata kwa urahisi,” amesema.

Amesema fedha hizo zinaweza kusaidia wananchi hasa wa vijijini ambao kipato ni kidogo kwa kutowawekea ukomo wa matibabu, kwamba wenye fedha ndogo na matibabu yao yanakuwa hayahusu magonjwa mengine makubwa.

Shabiby alishauri baada ya vyanzo hivyo, Serikali ihamie kwenye vyanzo vingine kama mazao kwa kutoza kila kilo moja Sh1 au Sh2.

“Kama mtu hana laini ya simu ina maana huyo masikini wa kutupwa, huyo hafai hata kuchukuliwa Sh200, atatibiwa kutokana na mifuko,” amesema.

“Sasa hiki kinachokuja, najua wengi mtanishangaa lakini ndio ukweli. Hizi hospitali, zahanati na vituo vya afya vijijini vifikie hatua ya kubinafsishwa. Huo ndiyo ukweli, tuige habari ya Korea Kusini, tusiwe wavivu, nendeni mkaangalie Korea Kusini wanafanya nini Abu Dhabi wanafanya nini,” amesema.

“Korea Kusini hakuna hospitali ya kijijini ambayo ni ya Serikali, hakuna kituo cha afya ambacho ni cha Serikali, zahanati zote zimeingizwa kwenye mfumo mmoja, vituo vya afya vyote vimo kwenye mfumo mmoja,” alisema.

“Lipo jengo kubwa wamejenga watu wa intaneti wapo hapo, ripoti zote zinakwenda kule mtu mwenye zahanati akitaka kulipwa na bima, wale lazima wanakague ile zahanati ilimtibu nini X hapa, kwamba nilimpiga x-ray, lakini nikaona nimtibu malaria nikampa Kwinini (Quinine), wale hawatalipa gharama za x-ray kwa sababu ni utapeli na watalipa gharama za matibabu ya malaria pekee,” alisema.

Alishauri Serikali iwe na mfumo wa aina hiyo utakaobaini wenye vitendo vya utapeli kwenye hospitali na zahanati.

Shabiby alisema hospitali zinazopaswa kubaki chini ya Serikali ni zile za rufaa kama Hosptali ya Taifa ya Muhimbili.

Alisema utaratibu huo pia utaondoa tabia ya baadhi ya madaktari wa hospitali za Serikali na ambao wanafanya kwenye hospitali binafsi kuwa madalali wa kupeleka wagonjwa kwenye hospitali binafsi kwa kuziponda za Serikali kwamba hazina vifaa vya kutosha.

Mipango iliyopo ya Serikali ni kuwezesha huduma za bima kwa wote kwa mapato yatokanayo na ushuru wa bidhaa kwenye vinywaji vyenye kaboni, vinywaji vikali, bidhaa za vipodozi, michezo ya kubahatisha, ada ya vyombo vya moto, na mapato yatokanayo na ushuru wa miamala ya kielektroniki kwa kadri itakavyopendekezwa.