Mjamzito ajifungulia nje ya zahanati usiku muuguzi akihofia usalama

Taswira ya mama mjamzito

Muktasari:

Tukio hilo limetokea Oktoba 16, 2023, baada ya mama mjamzito, Nyanzobhe Katale kufikishwa kwenye zahanati hiyo akiumwa uchungu wa kujifungua lakini akakosa msaada baada ya muuguzi anayeishi jirani kugoma kufungua mlango alipogongewa na waliomsindikiza mjamzito huyo usiku wa manane.

Tabora. Kukosekana kwa mlinzi katika Zahanati ya Kijiji cha Kidaru Wilaya ya Igunga mkoani Tabora kumesababisha mjamzito kujifungulia nje baada ya muuguzi kugoma kutoka nje usiku akihofia usalama wake.

Tukio hilo limetokea Oktoba 16, 2023, baada ya mama mjamzito, Nyanzobhe Katale kufikishwa kwenye zahanati hiyo akiumwa uchungu wa kujifungua lakini akakosa msaada baada ya muuguzi anayeishi jirani kugoma kufungua mlango alipogongewa na waliomsindikiza mjamzito huyo usiku wa manane.

‘’Nilipata uchungu wa kujifungua usiku wa Oktoba 16, 2023 nikaomba msaada kwa jirani yangu aliyenisindikiza zahanati kwa kutumia pikipiki lakini tukakuta zahanati imefungwa na hakuna mlinzi. Walionisindikiza wakaenda kumgongea muuguzi lakini hakufungua mlango,’’ amesema Nyanzobhe

Mandaru Charles, jiran aliyemsindikiza mjamzito huyo zahanati amesema baada ya jitihada za kumsawishi muuguzi kufungua mlango kushindikana, alimpigia simu Mtendaji wa Kijiji cha Kidaru, Jacobo Maganga ili afike eneo hilo kumthibitishia muuguzi huyo usalama wake lakini bahati mbaya mtendaji huyo alikuwa safarini.

Kauli ya muuguzi

Akizungumzia tukio hilo, muuguzi Agnes Shekitundu amekiri kukataa kufungua mlango na kutoka nje kwa sababu ya kuhofia usalama wake nyakati za usiku kutokana na matukio ya kihalifu.

“Zahanati yetu haina mlinzi na nilikuwa mwenyewe baada ya mtumizhi mwenzangu kuwa safarini mjini Igunga, hivyo nilihofia usalama na maisha yangu kwa sababu sikuwa na uhakika iwapo ule haukuwa mtego wa wahalifu,’’ amesema Agnes

Mlinzi afichua siri

Mlinzi wa zahanati hiyo, Daudi Nyama amekiri kutokuwepo eneo la lindo usiku huo akisema amelazimika kuacha kazi hiyo kutokana na kutolipwa malimbikizo ya mshahara kwa miezi minne fululizo.

‘’Naudai uongozi wa kijiji malimbikizo ya mshahara wa miezi minne kiasi cha Sh200, 000; nimeamua kuachana na kazi ya ulinzi na hivi sasa mimi ni mhudumu wa afya ngazi ya jamii. Hiyo ndio sasabu sikuwepo kwenye lindo siku ya tukio,’’ amesema Daudi

Viongozi watoa kauli

Akizungumzia tukio la mjamzito kujifungulia nje ya zahanati, Mganga Mkuu wa Wilaya ya Igunga, Dk Lucia Kafumu ameahidi kufuatilia kwa kina suala hilo kujua namna ya kulishughulikia.

‘’Kiutaratibu, uongozi wa kijiji unapaswa kuhakikisha zahanati inakuwa na mlinzi kwa ajili ya usalama wa watumishi na vifaa tiba; nitafuatilia kwa kina kujua kiini chatukio hilo na hatua za kuchukua kuhakikisha siyo tu usalama wa watumishi, bali pia uhakika wa huduma za dharura kwa wananchi,’’ amesema Dk Lucia

Ofisa Mtendaji wa Kata ya Isakamaliwa kilipo Kijiji cha Kidaru, Misambo Kanyelele ameahidi kwenda kijijini hapo kufuatilia suala hilo, ikiwemo la zahanati kuwa na mlinzi kwa ajili ya usalama wa watumishi, hasa nyakati za huduma za dharura usiku.