Mkandarasi akimbia, vibarua walia njaa
Muktasari:
- Mradi huo ambao utahudumia vijiji 11vya kata hiyo, utagharimu Sh 2.1bilioni na unatarajiwa kukamilika Septemba mwaka huu.
Moshi. Wakati ‘vibarua’ katika mradi wa maji wenye thamani ya Sh2.1 bilioni, Kata ya Marangu Magharibi, Wilaya ya Moshi, wakilalamika kutolipwa stahiki zao kwa muda mrefu, msimamizi wa mradi huo, Harison Mfangavo ajifungia kwenye gari kumkwepa mwandishi.
Vijana hao ambao wanatoka mikoa mbalimbali nchini, wamedai kuwa, wamekuwa wakifanya kazi kwa makubaliano ya kulipwa kila wiki, lakini mkandarasi huyo amekuwa hatimizi jukumu hilo kitu kinachosababisha wakiendelea kuishi maisha magumu.
Hata hivyo mwandishi wetu alipotaka kupata maoni ya mkadarasi huyo, hakuonyesha nia ya kutaka kuzungumza na badala yake aliingia na kujifungia kwenye gari.
Hata pale juhudi zilipofanywa kuwapata viongozi wa Makao Makuu ya kampuni hiyo yaliyoko Dar es Salaam, Kundaeli Mfwangavo ambaye ndiye mkandarasi wa mradi, alijitenga na malalamiko hayo huku akitupia mpira kwa aliyeko site ndiye ajibu.
"Hakuna malalamiko ni hearsay,” amesema Kundaeli akimaanisha ni taarifa ya kuambiwa na haina uhalisia wowote, na kuongeza kuwa: “Wahoji wale walioko kule kwenye mradi, mimi niko head office Dar es Salaam, malalamiko hayajanifikia mimi, ila ninachojua ni hearsay hakuna malalamiko.”
Awali wakizungumza kwa nyakati tofauti vijana hao ambao kila mmoja anadai kiasi chake cha fedha kulingana na siku alizofanya kazi, wamesema wamefanya kazi katika mradi huo ikiwemo kuchimba mtaro wa kulaza mabomba tangu kuanza kwa mradi huo na hawajalipwa stahiki zao.
Akizungumza Michael Samson kutoka Morogoro amesema kutolipwa fedha zao kumewasababishia changamoto kubwa hadi kwenye familia zao kutokana na kushindwa kutuma fedha za matumizi
"Hii imekuwa changamoto kubwa, kwa sasa naamua kuzima simu ili kuepuka usumbufu wa familia kwa kuwa nimeshindwa kutuma fedha za matumizi, naomba serikali itusaidie katika hili," amesema.
Kwa upande Samuel Sam, amemwambia mwandishi wa habari hizi kuwa makubaliano ni kupokea ujira wao kila wiki lakini sasa ni wiki ya tatu hawajalipwa na kwamba kila siku wanapewa tarehe, jambo ambalo limewasabibishia mgogoro na familia zao kutokana na kushindwa kutuma fedha za matumizi.
"Wengine tumeacha familia, watoto wanateseka kwa kushindwa kuzihudumia, inafika mahali unauhitaji kwa ajili ya kujikimu na familia yako, ukiuliza unapewa majibu yasiyoridhisha, ni bora mtu akupe majibu kuwa anashughulikia kwa wiki moja au mbili fedha mtazipata lakini anatuambia kesho na ikifika haeleweki," amesema na kuongeza;
"Tumefika mahali tukasitisha kufanya kazi na wanaotuzunguka ndiyo wanaotusaidia lakini wao hawakupaswa kubeba mzigo huu, familia sasa zinahisi tumeanzisha familia nyingine huku kwa kuwa hatutumi fedha za matumizi, vitu ambavyo sivyo, tunaomba jambo hili lishughulikiwe tupate muafaka kwani tumekuja hapa kwa ajili ya kutafuta riziki kama wao wanavyotafuta."
Bosco Lekule ambaye anadai Sh 300,000 amesema amefanya kazi zaidi ya siku 30 na hajalipwa fedha zake mpaka leo na kila siku anapomuuliza bosi wao amekuwa akiahidi kuwalipa bila mafanikio.
"Mimi nadai fedha kuanzia Aprili 29 mwaka huu na mpaka leo naendelea kufanya kazi kila siku na sijapewa hela zangu, nikimuuliza bosi anasema kesho kila siku, siku nyingine bosi haonekani anarudi usiku tukimuuliza anasema tukalale turudi asubuhi lakini asubuhi hayupo," amelalamika.
Mwenyekiti wa vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM) Wilaya ya Moshi Vijijini, Yuvenal Shirima ambaye alifika katika eneo hilo, amewataka vijana hao kuvuta subira na kuwa wavumilivu wakati wakiendelea kulifuatilia suala hilo.
"Niwape pole vijana wenzangu kwa haya mnayopitia, niwaombe mvute subira, mtuvumilie tulifuatilie hili na kila mmoja atapata haki yake kulingana na siku alizofanya kazi kama mlivyokubaliana," amewafariji Mwenyekiti huyo.
"Kila mmoja anatambua anadai shilingi ngapi, tayari nimeongea na Meneja wa Ruwasa Mkoa amesema analifuatilia, sasa niombe orodhesheni majina yenu kila mmoja na kiasi anachodai, ili tuweze kulifuatilia na kuhakikisha mnapata haki zenu, kwani mradi huu umekuja kwa ajili ya maendeleo na si kuwatesa wananchi,” aliongeza.
Diwani wa kata ya Marangu Magharibi ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Moshi, Filbert Shayo amesema hawana taarifa za malalamiko hayo na kwamba kama ni madai ni makubaliano yao na mkandarasi.
"Mradi huu umehujumiwa, kuna mabomba yamekatwa na vibao vinavyoelekeza kuanza na kumalizika kwa mradi navyo vimevunjwa, na kwa hisia za haraka huwenda wanaodai fedha ndio wamehujumu mradi ili walipwe, kwani tumefika hapa na kuona wanalalamika wanadai," amehoji Diwani huyo.
Amesema mradi huo ambao utahudumia vijiji 11vya kata hiyo, utagharimu Sh 2.1bilioni na unatarajiwa kukamilika Septemba mwaka huu.