Mradi wa uchimbaji visima 20 Dar wasua

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Amos Makala akiutazama mtambo unaotumika kuchima visima vya maji kigamboni ukiwahaufanyi kazi.

Muktasari:

  • Mkuu wa mkoa wa Dar es salaam Amos Makalla ameipa siku saba Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (Dawasa) kuwasilisha ofisini kwake mpango waliouandaa kwa ajili ya kukabiliana na dharura ya maji nyakati za ukame kwenye mkoa huo,hii ni baada ya kubaini kusimama kwa mradi wa ufufuaji wa visima 20 wilayani Kigamboni.

Dar es Salaam. Mradi wa uchimbaji wa visima 20 unaotekelezwa na Mamlaka ya Maji safi na Usafi wa Mazingira (Dawasa) kwa ajili ya kutatua tatizo la maji hasa kipindi cha ukame mkoani Dar es Salaam, umesimama.

Kusimama kwa mradi huo kumeibua wasiwasi kwa Mkuu wa mkoa huo Amos Makalla ambaye amehoji kama kuna uhakika wa Dar es Salaam kutoingia kwenye kadhia ya kukosa maji kipindi cha ukame mwishoni mwa mwaka huu.

Akizungumza leo Mei 9, 2023 katika ziara ya kukagua utekelezaji wa mradi huo wa uchimbaji wa visima 20 Kigamboni, Makala amesema kwa miaka miwili mfululizo Dar es Salaam imekuwa na adha ya maji.

Kutokana na hali hiyo Makala ameitaka Dawasa ndani ya siku saba iwasilishe ofisini kwake mpango waliouandaa kumaliza tatizo la maji endapo kutatokea dharura kwenye mkoa wake.

Mpaka sasa kati ya visima 20 ambavyo vilipaswa kuchimbwa ni visima saba pekee ndivyo vimefanyiwa kazi na Kampuni ya Serengeti ambayo inatekeleza miradi, japo mkandarasi hakuonekana eneo la mradi kwa kile kilichoelezwa kuwa mitambo imeharibika.

"Nimekuja kuhakikisha kwamba mradi umefika mwisho, ulianza tangu mwaka 2014 na Rais Samia Suluhu Hassan amekwisha kutoa fedha, ni mara ya pili tunawaambia Dawasa wajipange kwa miradi ya maji kunapotokea dharura naelekeza mkandarasi arudi kutekeleza miradi huu,” amesema.

Pia aliongeza kusema: “Nawapa siku saba Dawasa, nataka nipate mpango wa visima vilivyosafishwa vinaanzaje kupata fedha.”

Kwa upande wake, Kaimu Mtendaji Mkuu wa Dawasa Shaban Mkwanywe amesema tayari wameshaandaa mpango wa kutatua changamoto ya maji Dar es Salam na wamewasilisha wizara ya maji lakini mwingine watauwasilisha kwa mkuu wa mkoa huyo.

Kuhusu kusimama kwa mradi huo wa visima amesema ni wiki moja sasa kutokana na hitilafu ya mitambo akiahidi kuandaa namna bora ya kumsimamia mkandarasi huyo.