Sh760 milioni kuchimba visima vijiji 14 Chunya

Mbunge wa  Lupa ,Masache Kasaka akifungua bomba la maji kuashiria kukamilika kwa mradi wa uliofadhiliwa na Shirika la CRS wenye thamani ya Sh 880 milioni utakaozalisha  lita 150,000 kwa siku na kuhudumia wakazi 2,000 wa kata ya Ifumbo wilayani Chunya mkoani Mbeya. Picha na Hawa Mathias.

Muktasari:

  • Mradi wa uchimbaji wa visima vya maji safi utaelekezwa kwenye vijiji vya pembezoni ambako kuna hadha kubwa ya maji na mwingiliano mkubwa wa shughuli za kijamii ikiwepo uchimbaji wa madini ya dhahabu.

Mbeya. Serikali imetoa zaidi ya Sh760 milioni kwa ajili ya utekelezaji wa mradi wa kuchimba visima virefu vya maji katika vijiji 14 Wilaya ya Chunya Mkoa wa Mbeya kwa lengo la kutatua changamoto ya maji katika maeneo ya pembezoni.

Meneja wa Wakala wa usambazaji Maji vijijini (Ruwasa) Wilaya ya Chunya, Mhandisi Ismail Nassoro ameliambia Mwananchi leo Jumatano Aprili 12, 2023 wakati Mbunge wa Lupa Masache Kasaka alipotembelea mradi wa maji wilayani humo.

Mradi huo uliofadhiliwa na shirika la Catholic Relief Service (CRS) kwa gharama ya Sh880 milioni na kuhudumia wakazi 2,000 katika Kata ya Ifumbo.

Mhandisi Nassoro amesema mradi wa uchimbaji wa visima tayari utekelezaji wake umeanza mara baada ya Wizara ya Maji kupeleka gari na vifaa maalum vya utekelezaji wa miradi hiyo.

“Kama unavyojua jiografia ya Wilaya ya Chunya kuna changamoto kubwa ya maji ambapo kati ya vijiji 14 tayari vijiji viwili cha Itumbi na Matondo mradi umekamilika na wakati wowote wananchi wanaanza kupata huduma ya maji safi na salama ya bomba,” amesema.

Kwa upande wake Mbunge wa Lupa, Masache Kasaka amesema kuwa kitendo cha Serikali kuelekeza miradi ya maji wilayani humo imekuwa na mchango mkubwa kwani uwepo wa mradi wa maji Ifumbo wenye uwezo wa kuzalisha lita 150,000 kwa siku utakuwa mkombozi mkubwa.

“Mradi huu utakuwa mwarobaini kwa Chunya kupata huduma ya maji katika Kata ya Ifumbo ambapo wananchi zaidi 2,000 watanufaika ikiwepo ujenzi wa visima katika vijiji 14 yote hiyo ni matunda ya Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan,” amesema.

Kasaka amefafanua kuwa kuna miradi minne mikubwa iliyoelekezwa na Serikali ambayo imekamilika ni wa Makongolosi uliozinduliwa na Rais Samia Suluhu Hassan, Matundasi na Sangambi uliozinduliwa na mbio za mwenge wa uhuru mapema mwaka jana.