Mkapa alivyochuana na mawakili wa Serikali akimtetea Mahalu (4)

Muktasari:

  • Katika sehemu ya tatu ya mapitio ya kesi ya aliyekuwa balozi wa Tanzania nchini Italia, Profesa Ricky Costa Mahalu, tuliona jinsi Rais wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa alivyomtetea Profesa Mahalu dhidi ya tuhuma za wizi zilizokuwa zikimkabili.

Katika sehemu ya tatu ya mapitio ya kesi ya aliyekuwa balozi wa Tanzania nchini Italia, Profesa Ricky Costa Mahalu, tuliona jinsi Rais wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa alivyomtetea Profesa Mahalu dhidi ya tuhuma za wizi zilizokuwa zikimkabili.

Rais Mkapa aliieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa alikuwa akipata taarifa zote kuhusu mchakato wa ununuzi wa jengo la ubalozi wa Tanzania nchini Italia na Serikali yake iliridhia bei na utaratibu wa ulipaji wa fedha hizo.

Profesa Mahalu pamoja na aliyekuwa Ofisa Utawala wa ubalozi huo, Grace Martin walishitakiwa mwaka 2007 kwa kula njama, kutumia nyaraka za ununuzi ya jengo la ubalozi kwa nia ya kumdanganya mwajiri wao (Serikali) na wizi wa Euro 2,065,827 (zaidi ya Sh2.5 bilioni).

Akiwa kizimbani, Mkapa alipambana vikali alipokuwa akihojiwa na upande wa mashtaka kuhusiana na ushahidi alioutoa.

 Endelea… Kama ulivyo utaratibu wa kisheria, upande kinzani katika kesi hupewa nafasi ya kumuuliza maswali kila shahidi anayesimama kizimbani kutoa ushahidi kuhusiana na ushahidi wake.

Hivyo, hata Mkapa baada ya kumaliza kutoa ushidi aliwekwa kikaangoni kwa kuulizwa maswali kutoka kwa waendesha mashtaka.

Ifuatayo ni sehemu ya mahojiano kati ya Mkapa na wakili wake, Alex Mgongolwa wakati akimuongoza kutoa ushahidi.

Mgongolwa: Shahidi, alikuja hapa shahidi wa kwanza wa mashtaka, Martin Lumbanga (aliyewahi kuwa Katibu Mkuu Kiongozi) akasema kuwa hakuwa na taarifa za idhini ya Serikali katika ununuzi wa jengo hilo, je, wewe unasemaje?

Mkapa: Ninashangaa kwa nini alisema hivyo.

Mgongolwa: Wewe ukiwa Rais ulijua na ukabariki, inawezekana yeye asingeweza kujua?

Mkapa: Ndio.

Mgongolwa: Kikatiba Rais hukabidhiwa ripoti ya CAG, je, una taarifa yoyote ya CAG kuhusu malalamiko juu ya ununuzi wa jengo hilo?

Mkapa: Sikuwahi kupata malalamiko hayo.

Mgongolwa: Nini ufahamu wako kama Rais mstaafu juu ya utumishi wa mshtakiwa ambaye ulimteua kuwa Balozi Italia?

Mkapa: Ninamfahamu kama msomi mzuri, mwadilifu na mfanyakazi mwaminifu na kiongozi wahaki. Mkapa aliongeza uzito katika jibu hilo kwa kutaja sifa na nafasi mbalimbali za uongozi wa Profesa Mahalu katika utumishi wake.

Baada ya Mkapa kumaliza kutoa ushahidi wake, ilifuata zamu ya mawakili wa Serikali, Vicent Haule na Wakili wa Serikali Mkuu, Ponsiano Lukosi, kumuuliza maswali kuhusiana na ununuzi wa jengo hilo.

 Haule: Mheshimiwa katika hansard (kielelezo namba 6 cha upande wa utetezi) uliyosoma imeandikwa jumla ya fedha zilizopelekwa kununua jengo hilo ni kiasi gani?

Mkapa: Sh29 bilioni.

Haule: Na zilizoandikwa kwenye hii risiti ambazo ulisema ulikuwa unazifahamu ni kiasi gani?

Mkapa: Nilichosema ni Euro 3 milioni, mimi sijui exchange rate wakati huo ilikuwa ni kiasi gani hiyo si kazi yangu.

Haule: Nani aliagiza upelelezi wa ununuzi wa jengo hilo?

Mkapa: Mimi sijui.

Haule: Uchunguzi wa malipo hayo ulifanyika lini, ukiwa bado madarakani au baada ya kutoka madarakani?

Mkapa: Mimi sijui, nilikuja kusikia tu kuwa balozi wako anashtakiwa.

Haule: Ulijua lini kuwa balozi wako uliyekuwa umemteua wewe anashtakiwa?

Mkapa: Siku alipofikishwa mahakamani ndipo nilipoambiwana kesho yake kweli nikamuona kwenye magazeti.

Haule: Ulisema ulipotaarifiwa kuhusu ununuzi huo ulibariki na hukuzuia, kwani ulipaswa kuzuia?

Mkapa: Ningeweza kuzuia na kuamuru hizo fedha zipelekwe kwingine kwa kuwa wakati huo tulikuwa na crisis (tatizo) ya fedha, lakini kwa kuwa niliona umuhimu wa ununuzi wa jengo hilo nikaagiza linunuliwe.

Haule: Umuhimu upi, wa kulipa kupitia akaunti mbili au upi

Mkapa: Kupata Chancellery (Ofisi ya ubalozi).

Haule: Baada ya kutoa maagizo hayo (kwa Profesa Mahalu), ni nani mwingine katika wizara (Mambo ya Nje) uliyemwarifu kuhusu malipo hayo kwa akaunti mbili?

Mkapa: Kwani hiyo inahusiana na nini? Maagizo yangu mimi nilishatoa kwa balozi jengo linunuliwe, kama Rais nilikuwa ninaagiza tu.

Haule: Mheshimiwa, nakuuliza tena, na nisingependa nawe uniulize swali. Ni kweli au si kweli kwamba hakuna mtu mwingine wizarani ambaye ulimpa taarifa hizo? Mkapa: Sikumbuki mimi.

Wakili Lukosi: Mheshimiwa, Lumbanga akiwa Katibu Mkuu Kiongozi ulikuwa ukimwamini?

Mkapa: Ndio.

Lukosi: Ni kwa kiasi gani ulimshirikisha katika ununuzi wa jengo hilo?

Mkapa: Specifically (mahususi) katika hilo sikumbuki, lakini ki-principle (kimsingi) nilishatoa maagizo kuwa mkipata chancellery nunueni na yeye alikuwa akijua. Tulifanya hivyo India, Marekani na Uingereza.

Lukosi: Sasa Lumbanga alisema hajui ununuzi wa hili, je, wewe unaona ni kitu cha kawaida?

Mkapa: Ndio maana nimesema nashangaa, maana haingewezekana kwamba mimi nika-communicate (nikafanya mawasiliano) na wizara moja tu na Lumbanga asijue.

Lukosi: Ulipata kujua au kuuliza ni kwa nini muuzaji alitaka alipwe kupitia katika akaunti mbili tofauti? Mkapa: Sikuuliza, mimi nilichokuwa nataka ni chancellery.

Lukosu: Unakumbuka kuna jengo lingine la ubalozi ambalo muuzaji alitaka alipwe kwa utaratibu huu wa kupitia akaunti mbili tofauti?

Mkapa: Siwezi kusema, nakumbuka lakini siwezi kusema kwa sababu mambo mengine ukiyasema yanaweza kuharibu uhusiano na nchi husika. Jibu hilo lilimfanya Hakimu Mugeta naye aingilie kati kwa kumuuliza Mkapa swali la nyongeza, kisha akamwacha wakili Lukosi akaendelea. Hakimu Mugeta: Kwa hiyo hayo mazingira huwa yapo?

Mkapa: Ndio. Lukosi: Unawakumbuka watu wengine uliowahi kuwateua ambao wako mahakamani na yuko mwingine alishakuja kukuomba umtetee?

Mkapa: Ni lazima nilijibu hili? Alihoji Mkapa, huku akicheka na kuwafanya wasikilizaji nao wacheke. Lukosi: Kwa hiyo hii ni kesi ya kwanza kwako kuombwa kuja kutoa ushahidi?

Mkapa: Ndio.

Lukosi: Nikikwambia lengo la mwenye jengo kutaka mchakato wa uuzwaji kuwepo na mikataba miwili lilikuwa ni kukwepa kodi kwa Serikali yake utasemaje?

Mkapa: Hilo ni tatizo lake na nchi yake, mimi nilikuwa nataka nyumba na nimepata nyumba, nasema Alhamdulillah. (Alisema Mkapa huku akicheka tena na kuwafanya wasikilizaji nao wavunjike mbavu).

Lukosi: Nikikwambia hizo fedha kulipwa kwa instalment (kwa awamu), Profesa Mahalu alikuwa anataka azitumie kwa maslahi yake utasemaje?

Mkapa: Mimi nitashangaa sana, hasa nitakushangaa wewe, maana Profesa mimi namuamini. (Alijibu Mkapa na kuwachekesha wasikilizaji kwa mara nyingine). Baada ya maswali ya mawakili hao wa Serikali, wakili mwingine wa utetezi, Mabere Marando alimuuliza maswali machache katika kusawazisha mashimo yaliyotokana na maswali aliyoulizwa na mawakili wa Serikali, kwa kutoa ufafanuzi, kama ifuatavyo:

Marando: Shahidi, umewahi kupata malalamiko yoyote kutoka wizarani kuwa kulikuwapo makosa katika ununuzi wa jengo la ubalozi Italia?

Mkapa: Sijawahi. Marando: Ama kutoka kwa Katibu Mkuu Kiongozi, Martin Lumbanga, ama kwa Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje, ama wa Wizara ya Fedha, ama Hazina kwamba Balozi Mahalu alifanya kosa kwenda kufanya malipo katika akaunti mbili za muuzaji?

Mkapa: Yeyote kati ya hao hakuna.

Marando: Mpaka unaalikwa kwenda kuzindua jengo hilo, uliwahi kupata ushauri kutoka ofisi ya DPP (Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka) ama kwa AG (Mwanasheria Mkuu wa Serikali) kwamba usiende katika uzinduzi wa jengo hilo kuna uchafu?

Mkapa: Sikuwahi kushauriwa. Itaendelea kesho


Kwa maoni na ushauri kuhusu habari hii tuandikie kupitia 0765864917