Mke, mume wafa ajalini ikiua sita Kiteto

Wanandoa ambao ni miongoni mwa watu sita walifariki dunia katika ajali gari iliyotokea eneo la Pori namba moja Kata ya Partimbo wilayani Kiteto Mkoani Manyara.

Muktasari:

  • Ajali hiyo imetokea eneo la Pori namba moja Kata ya Partimbo wilayani Kiteto Mkoani Manyara baada ya gari la wagonjwa kugongana kugongana uso kwa uso na gari dogo.

Kiteto. Watumishi sita wa Serikali, Wilaya ya Kiteto mkoani Manyara, wakiwamo mke na mume, wamefariki dunia na wengine watano wamejeruhiwa baada ya kupata ajali ya gari eneo la Pori wilayani humo.

  

Watumishi hao kati yao watano wanatoka Idara ya Afya na mmoja Idara ya Elimu, kwa pamoja wamepoteza maisha baada ya gari lao walilokuwa wamepanda kugongana uso kwa uso na gari lingine aina ya Prado.


Tukio hilo limetokea jioni ya jana Jumatatu Novemba 07, 2022 eneo la Pori namba moja Kata ya Partimbo wilayani Kiteto na kupelekwa hospitali ya Mkoa wa Dodoma kwa matibabu zaidi.

Mkuu wa Wilaya ya Kiteto Mbaraka Batenga, akiwa hospitali ya Kiteto amethibitika kutokea ajali hiyo.


Alisema ajali hiyo imehusisha gari la wagongwa la Kituo cha Afya Sunya lililokuwa limepeleka mgonjwa Hospitali ya Wilaya ya Kiteto kwa ajili ya matibabu na wakati likirudi likiwa limebeba watumishi kurejea eneo la kazi Sunya liligongana uso kwa uso na gari dogo aina ya Prado likitokea barabara ya Kilindi Tanga kwenda Kiteto.

"Ajali hii imehusisha gari letu la afya ‘ambulance’, Kituo cha Afya Sunya ambalo limegongana uso kwa na gari lingine dogo aina ya Prado na kusababisha vifo vya watu sita na majeruhi watano wamepelekwa hospitali ya Dodoma, wangine wawili wanaendelea na matibabu hospitali ya Wilaya ya Kiteto" alisema Batenga.

Taarifa zinasema kati ya waliofariki ni mume na mke ambao wameacha mtoto wa miezi nane.

Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Kiteto, Pascal Mbota akizungumza na Mwananchi Digital alisema amepokea miili ya watu wawili waliopoteza maisha na majeruhi kumi na moja.


Kati ya majeruhi hao wanne wamefariki katika harakati za kuokoa maisha yao, watano wamesafirishwa kwenda Hospitali ya Dodoma kwa matibabu na wawili wanaendelea kutibiwa katika hospitali ya Kiteto.


Kamanda wa Polisi Mkoa wa Manyara RPC George Katabazi, alithibitisha ajali hiyo akisema atatoa taarifa kamili baadaye.