Mkenda atoa angalizo ubora wa elimu ya juu

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda

Dar es Salaam.  Waziri wa Elimu, Profesa Adolf Mkenda amewataka wadhibiti ubora wa elimu barani Afrika kutoshawishika kushusha viwango vya ufaulu ili vyuo vipate wanafunzi wengi.

Amesema wanafunzi wanatakiwa wakidhi viwango vya kimataifa hivyo wasiokuwa na sifa stahiki watafutiwe namna nyingine ya kusaidiwa ili wafikie vigezo husika na si kwa kushusha viwango vya ufaulu.

Wito huo ameutoa leo Jumanne, Novemba 28, 2023  wakati wa mkutano wa Mtandao wa wathibiti ubora wa elimu ya juu barani Afrika (AfriQAN) uliolenga kujadili mchango wa wathibiti ubora wa elimu ya juu katika dunia ya kidijitali. 

Profesa Mkenda amesema wanataaluma hao wana jukumu kubwa la kuhakikisha suala la ubora wa elimu linapewa kipaumbele kwa kuangalia masilahi mapana ya bara la Afrika lengo likiwa kutengeneza watalaamu siyo wahitimu.

“Wadhibiti ubora mna kila sababu ya kuendelea kusimamia suala la ubora wa elimu, kwa namna yoyote msikubali kuangukia kwenye shinikizo la kushusha ubora. Shinikizo hili linaweza kuwepo kwa sababu ya kuongezeka kwa idadi ya vyuo vikuu ikizingatiwa kwamba uendeshaji wa vyuo hivi ni biashara yenye ushindani. 

“Katika ufundishaji wa vyuo vikuu kazi kubwa ni kuhakikisha mwanafunzi anafanya vizuri, inaposhindikana basi huyo mwanafunzi aondoke lakini siyo kushusha viwango ili kukidhi hali yake. Sasa katika ushindani isije ikatokea ili mradi mwanafunzi ana ada basi aendelee tu au kutoa ufaulu mkubwa kwa lengo la kuvutia,” amesema Profesa Mkenda. 

Kuhusu kuongeza idadi wanafunzi katika vyuo vikuu amesema sula hilo nalo linapaswa kumulika ili ongezeko hilo lisiwe kikwazo cha utoaji elimu bora na kuzuia wahadhiri kufanya tafiti zinazolenga kupata maarifa mapya. 

“Tuangalie azma njema ya kuongeza idadi ya wanafunzi katika vyuo vikuu vyetu isiwe chanzo cha kupunguza ubora wa elimu, wahadhiri ni lazima wapate muda wa kufanya tafiti” amesema

Waziri huyo pia aligusia suala la kuajiri wahadhiri akieleza nalo linapaswa kuangaliwa kwa umakini mkubwa kuhakikisha watu wanaopewa dhamana ya kufundisha kwenye vyuo vikuu wanakidhi viwango stahiki vinavyotambulika kimataifa,” amesema.

Akizungumza kwenye kongamano hilo Mkurugenzi wa Tafiti wa Shirikisho la Vyuo Vikuu Afrika (AAU), Profesa Fredrick Ato Armah ameweka msisitizo kwenye ushirikiano wa vyuo vikuu na kuitumia teknolojia kama nyenzo ya kufikia malengo waliyojiwekea.

“Teknolojia imeturahisishia sasa hivi mhadhiri wa chuo katika nchi moja anaweza kuwafundisha wanafunzi wa chuo kingine, kinachotakiwa kufanyika ni uwekezaji katika hii miundombinu ya teknolojia.  

“Suala jingine tunapaswa kutambua kuwa katika ulimwengu huu wa kidijitali teknolojia haikwepeki, muhimu kwetu ni kujitahidi tuendane na maendeleo ya teknolojia,” amesema Profesa Armah. 

Katibu Mtendaji wa Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU), Profesa Charles Kihampa amesema ushirikiano wa taasisi hizo za udhibiti ubora barani Afrika unalenga kuhakikisha viwango vya elimu ya juu katika nchi wanachama vinawiana. 

“Mtandao unatuwezesha kushirikina na wathibiti ubora kutoka nchi mbalimbali katika kutimiza jukumu la kudhibiti ubora wa elimu tukiandaa taratibu mbalimbali za uendeshaji taasisi za elimu ya kuu.

“Hii ina maana kwamba elimu hasa ya elimu ya juu inapaswa kumtengeneza mhitimu anayeweza kufanya kazi si tu ndani ya nchi yake bali hata katika nchi nyingine, kupitia mtandao huu kuna vigezo vya uthibiti ubora ambavyo tunavitumia kuhakikisha wanafunzi wetu wanahitimu wakiwa na viwango,” amesema Profesa Kihampa. 

Amesema mkutano huo unafanyika nchini kwa mara ya kwanza tangu kuanzishwa kwa mtandao huo miaka 14 iliyopita na mwaka huu Tanzania imepata fursa ya kuwa mwenyeji. 

Mkutano huo umehusisha washiriki kutoka nchi 22 za Afrika zikiwemo Tanzania, Kenya, Rwanda, Malawi, Lesotho, Uganda, Eswatini, Ghana, Zambia, Niger, Nigeria, Senegal, Zimbabwe, DRC, Cape Verde, Mali, Namibia, Angola, Ivory Coast na Misri.