Mkono kuzikwa Mei 29 Butiama
Mbunge wa zamani wa Musoma Vijijini, Wakili Nimrod Mkono enzi za uhai wake.
Muktasari:
- Maziko ya Mbunge wa zamani, Nimrod Mkono yanatarajiwa kufanyika Mei 29, mwaka huu mkoani Mwanza.
Dar es Salaam. Mwili wa Mbunge wa zamani wa Musoma Vijijini, Wakili Nimrod Mkono unatarajiwa kuzikwa Mei 29, mwaka huu katika Kijiji cha Kigori mkoani Mara.
Wakili Mkono alifariki dunia Aprili 18, mwaka huu nchini Marekani alikokwenda tangu mwaka 2018 kwa matibabu ya ugonjwa wa kupoteza kumbukumbu.
Kulingana na taarifa ya maziko hayo, iliyotolewa leo Jumatano Mei 24, 2023 na kamati ya mazishi, mwili wa mwanasiasa huyo utapokelewa kutokea Marekani Mei 27, mwaka huu.
Kesho yake, Mei 28, mwaka huu waombolezaji watapata fursa ya kutoa heshima za mwisho kwa Wakili Mkono katika viwanja vya Karimjee jijini Dar es Salaam.
Baadaye, mwili huo utasafirishwa kwa njia ya anga kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere kuelekea Mara yaliko makazi yake ya asili.
Mkono alishinda ubunge wa Musoma Vijijini mwaka 2000 na kuongoza kwa vipindi vitatu hadi mwaka 2015.
Mwanasiasa huyo, alizaliwa Agosti 18, 1943 katika Kijiji cha Busegwe mkoani Mwanza.