Mkutano wa CCM, Chadema waibua hisia tofauti

Rais Samia Suluhu Hassan akiongoza kikao cha majadiliano kilichohusisha viongozi wa CCM, Chadema na Serikali Ikulu Chamwino Jijini Dodoma, juzi. Picha na Ikulu

Muktasari:

Siku moja baada ya viongozi wa Chama cha Mapinduzi (CCM), wakiongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kuonana na ujumbe wa viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), baadhi ya wasomi wameeleza faida na hasara ya mkutano huo.

Dar es Salaam. Siku moja baada ya viongozi wa Chama cha Mapinduzi (CCM), wakiongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kuonana na ujumbe wa viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), baadhi ya wasomi wameeleza faida na hasara ya mkutano huo.

Rais Samia akiambatana na viongozi waandamizi wa CCM na Serikali walikutana na ujumbe wa viongozi wa Chadema, ulioongozwa na mwenyekiti wao, Freeman Mbowe, Ikulu ya Chamwino mkoani Dodoma na kufanya mazungumzo ambayo bado hayajawekwa wazi na pande hizo mbili.

Mazungumzo baina na Rais Samia na viongozi hao wa chama kikuu cha upinzani ni mwendelezo wa kiongozi huyo mkuu wa nchi wa kukutana na makundi mbalimbali ya wadau wa demokrasia ili kuleta utengamano wa Taifa.

Wasomi hao walieleza hayo jana kwa nyakati tofauti, wakati wakizungumza na Mwananchi na kuongeza kuwa hatua ya viongozi wa CCM kukaa meza moja na Chadema inaashiria huenda Taifa likashuhudia siasa safi kwa siku zijazo.

Mchambuzi wa masuala ya siasa, Dk Faraja Kristomus alisema kikao cha uongozi wa juu wa Chadema na CCM chini ya Rais Samia kinatoa picha mbili tofauti.

Alisema upande mmoja unatoa taswira ya matumaini ya maridhiano ya kisiasa kutokana na mvutano ambao umekuwapo kwa muda mrefu kati ya pande hizo mbili.

“Kama viongozi wa ngazi ya juu wanakutana inaleta matumaini kuwa hali ya kisiasa itatengemaa kwa siku zijazo. Huenda kutakuwa na mazingira mazuri ya kufanya siasa na madai ya muda mrefu ya Chadema yatafanyiwa kazi.

“Lakini upande wa pili, baadhi ya wafuasi wa vyama vingine vya upinzani watawachukulia hawa viongozi wa Chadema kama wabinafsi. Watachukuliwa kama watu wenye kutanguliza masilahi binafsi na siyo ya kisiasa nchini kwa sababu kwa nyakati tofauti wamekuwa wakisusia vikao vya pamoja na vyama vingine,” alisema Dk Kristomus.

Hata hivyo, Dk Kristomus ambaye ni mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), alisema viongozi wa Chadema watakuwa na kazi kubwa ya kuwatuliza wafuasi wao vijana wanaharakati watakaoweza kuhisi kuwa viongozi wao wanaanza kukaa meza moja na CCM waliokuwa wakiamini hawawezi kuwatakia mema.

Mchambuzi mwingine, Said Msonga, alisema “ni hatua nzuri ingawa imekuja kwa kuchelewa, ilitakiwa ifanyike mapema, ni kikao chenye nia safi cha mwendelezo wa Rais Samia kutafuta njia bora kufanya siasa bila watu au viongozi kutukana. Kwa hatua hii huenda viongozi wa Chadema wakashiriki katika kikosi kazi.

“Ingawa mwanzoni Chadema walijiweka kando kutokana na msimamo wao, kwa mazingira ya sasa wameamua hakuna jinsi ya kujitenga ili kuweka siasa safi. Chadema ndio chama kikuu cha upinzani chenye wafuasi wengi, ndiyo maana hatua ya kuonana na Rais imekuwa gumzo.”

Hata hivyo, Msonga alisema kitendo cha viongozi wakuu wa Chadema kuonana na Rais Samia, kimepokewa kwa hisia tofauti kwa wanachama na viongozi wa chama hicho, baadhi waliunga mkono huku wengine wakipinga hatua hiyo, wakidai licha ya kufanya mazungumzo, madai yao hayasikilizwi.

Msonga ambaye pia ni mchambuzi siasa za kimataifa alisisitiza kwa mazingira ya sasa hakukuwa na namna ya chama hicho kikuu cha upinzani kuendelea kujitenga na kwamba uamuzi wao utaisaidia Chadema kutoa mchango wao wa kuhakikisha siasa za Tanzania zinakwenda kuleta mabadiliko.

Mchambuzi mwingine, Profesa Mohamed Bakari alisema, “ingawa hatujui walichokizungumza, lakini muda utaongea wa kujua walichojadiliana na makubaliano yao.

“Hatua ya viongozi wa Chadema kukutana na Rais Samia inasaidia kuondoa minong’ono na kuweka uhalali wa mazungumzo yao, tofauti angekuwa na kiongozi mmoja.”

Profesa Mohamed ambaye ni mhadhiri wa UDSM, alisema Chadema ndio chama kikuu cha upinzani na mazungumzo yao na Rais Samia, viongozi wa Serikali pamoja na CCM yalikuwa yakiangaliwa kwa uzito mkubwa.