Mmoja afariki katika ajali iliyohusisha gari tatu Tanga
Muktasari:
- Ajali iliyohusisha magari mitatu jijini Tanga yaondoa maisha ya mtu, huku madereva wametakiwa kuchukua tahadhari wawapo barabarani ili kupunguza ajali barabarani na hivyo kuokoa maisha na nguvu kazi ambayo ambayo ni msingi wa maendeleo katika taifa.
Tanga. Mtu mmoja aliyefahamika kwa jina la Bakari Salim (25), amefariki dunia na wengine kadhaa kujeruhiwa katika ajali iliyohusisha magari mitatu mkoani Tanga.
Akithibitisha Kutokea kwa ajali hiyo Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Camachius Mchunguzi amesema, ajali hiyo iliyotokea katika Barabara ya Tanga – Muheza.
Kwa mujibu wa Kamanda huyo, Lori aina ya Scania lililokuwa likitokea Tanga mjini kuelekea Muheza, iligonga gari dogo mbili likianza na Toyota Ractis, kisha kugonga gari nyingine Suzuki ambapo gari hizi (Ractis na Suzuki) zilikuwa zikitokea Tanga mjini kuelekea Muheza.
Kamanda Mchunguzi amesema kuwa katika ajali hiyo, dereva wa Toyota Ractis amefariki, na imeelezwa kuwa chanzo cha ajali hiyo ni dereva huyo wa Toyota Ractis, kutaka kupita gari ambayo ilikuwa mbele yake bila kuchukua tahadhari.
Kamanda Mchunguzi amesema bado idadi ya majeruhi haijaweza kufahamika lakini wanaendelea na matibabu katika Hospitali ya Rufaa Bombo ambapo pia amewaonya vikali madereva wa vyombo vya usafiri ambao wamekuwa hawachukui tahadhari, wanapotumia barabara.
Baadhi ya watu walioshuhudia ajali hiyo, ambayo kwa mujibu wa Kamanda Muchunguzi imetokea jana Jumamosi Desemba 01, 2023; saa 5:50 usiku, wamelaumu kile walichokiita “uzembewa dereva” aliyekuwa akijaribu kulipita gari lililokuwa mbele yake bila kuchukua tahadhari.