watatu wa familia moja wadaiwa kumuua Mwenyekiti wa kitongoji Same

Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Kilimanjaro, Simon Maigwa.

Muktasari:

  • Mwenyekiti wa kitongoji cha Sinangoa A, kata ya Ndungu, Wilaya ya Same, Mkoani Kilimanjaro, Charles Mkuruto anadaiwa kuuawa na wananchi katika kitongoji cha Kampimbi, wilayani humo kisa mgogoro wa ardhi.

Same.Watu watatu wa familia moja, katika kitongoji cha Kampimbi, Kijiji cha Ndungu, Wilaya ya Same, Mkoani Kilimanjaro wanadaiwa kumshambulia na kumuua kwa kumkata sehemu za  kichwa na begani na kitu kinachodhaniwa kuwa na ncha kali,  Mwenyekiti wa kitongoji cha Sinangoa A, Charles Mkuruto na kumsababishia kifo chake.

Mwenyekiti huyo ambaye pia ni Mjumbe wa Baraza la ardhi kata ya Ndungu, aliuawa jana Aprili 26, mwaka huu baada ya ndugu hao kudaiwa  kumvamia na kumshambulia na kisha kutokomea kusikojulikana.

Inadaiwa kuwa mauaji hayo yanatokana na uwepo wa mgogoro wa ardhi unaobishaniwa na wanafamilia hao katika Kijiji hicho kwa muda mrefu ambao tayari upo katika Baraza la ardhi la kata.

Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo, Mkuu wa Wilaya hiyo, Kasilda Mgeni amesema tukio hilo limetokea   jana, Aprili 26,  saa 5:30 asubuhi maeneo ya kitongoji cha Kampimbi kata ya Ndungu na baada ya tukio hilo kufanyika watuhumiwa wa mauaji hayo walitoroka.

DC Mgeni amelaani vikali mauaji hayo ya kinyama ya watu kujichukulia sheria mkononi na kuliagiza Jeshi la polisi wilayani humo kuwasaka watuhumiwa hao na kuhakikisha wanakamatwa na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.

"Naliagiza Jeshi la polisi kufanya msako na  kuhakikisha wanawakamata watu watatu ambao ni  wa familia moja ambao ndio wanaotuhumiwa na maua ya nwenyekiti ili sheria ichukue mkondo wake,"amesema DC Kasilda

Awali mkuu huyo wa Wilaya amesema sababu za mauaji hayo zinatokana na mgogoro wa ardhi unaowahusisha watuhumiwa hao na serikali ya kijiji.

"Sababu za mauaji hayo ni mgogoro wa ardhi unaowahusisha watuhumiwa hawa wa familia moja, leo(jana) Baraza la ardhi lilienda eneo la mashamba yanayobishaniwa ndipo watuhumiwa walipomvamia marehemu na kumkata kata na kitu chenye ncha kali na kisha kukimbia,"amesema DC Kasilda

Alipotafutwa Kamanda wa polisi mkoani humo kuhusiana na mauaji hayo, Simon Maigwa amesema tayari wanamshikilia mtuhumiwa mmoja kwa kuhusika na mauaji hayo na kwamba wanaendelea kuwatafuta watuhumiwa wengine wawili.

"Ni kweli kulitokea mauaji haya ya Mwenyekiti wa kitongoji na tayari tunamshikilia mtuhumiwa mmoja na wengine wawili tunaendelea kuwatafuta ili tuwafikishe kwenye vyombo vya sheria,"amesema Kamanda Maigwa