Watu tisa mbaroni kwa tuhuma za kumuua mlinzi

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Njombe Mahamoud Banga.

Muktasari:

Mwenyekiti wa Mtaa wa Uzunguni, Yusto Kiyeyeu amesema tukio hilo la mauaji ni la ajabu kwa kuwa halijawahi kutokea kwenye mtaa huo

Njombe. Jeshi la Polisi Mkoa wa Njombe linawashikilia watu tisa kwa tuhuma za kuhusika na mauaji ya mlinzi, Samweli Nofola (28), mkazi wa Kijiji cha Mtewele kilichopo Wilaya ya Wanging'ombe mkoani Njombe.

Hayo yamethibitishwa leo Aprili 14, 2024 na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Njombe, Mahamoud Banga wakati akizungumza na Mwananchi Digital.

Amesema tukio hilo la mauaji limetokea katika Mtaa wa Uzunguni, Kata ya Maguvani, usiku wa kuamkia April 13, 2024, saa 8:30 usiku.

Kamanda Banga amesema marehemu alikuwa mlinzi wa kampuni ya ulinzi iliyopo mjini Makambako na siku ya tukio, watu wasiojulikana walimuua mlinzi huyo na kuvunja maduka manne na kuiba vitu mbalimbali.

Amesema vitu vilivyoibwa kwenye duka hilo ni mafuta ya kula lita sita na nusu, vocha, sabuni na pafyumu.

“Kuna mfanyabiashara mmoja ambaye ni mwalimu, alidai ndani ya duka lake kulikuwa na Sh300,000, hakuzikuta lakini kuna mwingine Sh2,000 za chenji naye hakuzikuta. Ukitafuta jumla ya fedha za watu zilizochukuliwa, ni kama Sh300,000 ukichanganya na vitu vilivyochukuliwa, unapata Sh500,000, lakini utaona uhai wa mtu umetolewa,” amesema Banga.

 “Kama lengo lilikuwa kuiba mali zenye thamani ndogo kiasi hicho, kipi kimewafanya watuhumiwa hao kutoa uhai wa mtu? Jambo linaloonekana hapa, pengine kulikuwa na suala la kisasi.”

Kamanda Banga amesema marehemu alikuwa akiishi Wanging'ombe lakini jioni huwa anakwenda kufanya kazi zake Makambako alikoajiriwa na kurudi tena nyumbani kwake.

Amesema hadi sasa, watu tisa wanashikiliwa na jeshi hilo wakituhumiwa kuhusika katika tukio hilo na wanaendelea na mahojiano huku uchunguzi zaidi ukiendelea.

Ametoa wito kwa wafanyabiashara na kampuni za ulinzi kuacha kuweka mlinzi mmoja ambaye atalinda maduka mengi kwenye eneo kubwa la namna hiyo kwa kuwa ni vigumu kuhimili endapo kutatokea changamoto kama iliyojitokeza.

Mwenyekiti wa Mtaa wa Uzunguni, Yusto Kiyeyeu amesema tukio hilo la mauaji ni la ajabu kwa kuwa halijawahi kutokea kwenye mtaa huo tukio linalohusisha mauaji ya mlinzi.

“Sasa hivi kumekuwa na vibaka ndani ya mtaa wangu na wengine wanashirikiana kutoka mitaa mingine,” amesema Kiyeyeu.

Baadhi ya wafanyabiashara ambao wamevunjiwa maduka yao na kuibiwa fedha na bidhaa, wakiwemo Christina Kilindila na Martin Nzalalila wamesema maduka yao  yamevunjwa na kuuawa mlinzi waliyemuajiri kulinda  mali zao.

"Tukio linasikitisha kwa kweli, unaiba vitu halafu unaua mlinzi! Kwa kweli dunia inaelekea kubaya,” amesema Kilindila.

Mkazi wa eneo hilo, Raphael Msumba ameiomba Serikali kupitia Jeshi la Polisi kurejesha utaratibu wa kuwa na sungusungu watakaokuwa na jukumu la kulinda mitaa yao ili kukabiliana na vitendo vya uhalifu hasa wizi wa mali unaozidi kuongezeka.