Vita ya ubakaji, uhalifu yahamia nyumba za ibada

Mkuu wa Dawati la Jinsia na Watoto Jeshi l Polisi Wilaya ya Mtwara, Inspekta Salma Iringo akizungumza na waumini wa Kanisa KatolikiParokia ya Yesu Kristo Mkombozi lililopo Mtaa wa Magomeni, wilayani Mtwara Mei 2022. Picha na mtandao
Dar es Salaam. Jeshi la Polisi linatekeleza mkakati maalumu wa kuwafikia waamini katika nyumba za ibada kwa lengo la kuwashirikisha katika vita dhidi ya uhalifu, hususan ubakaji na ulawiti.
Askari wa vyeo mbalimbali wakisaidiana na wale wa madawati ya jinsia wamekuwa wakitembelea makanisa na misikiti jijini Dar es Salaam kuomba ushiriki wa waamini katika kupambana na uhalifu, wakiweka msisitizo katika vitendo vya ubakaji na ulawiti wanavyodai vimeongezeka kwa kiasi cha kutisha.
“Na haya matukio (ubakaji na ulawiti) yamekuwa mengi mpaka nadhani ninyi mnashangaa kwa nini tuko hapa kanisani. Kutokana na kazi niliyoichagua sikutegemea hata siku moja nitasimama hapa kwenye altare kusema chochote,” alisema askari aliyejitambulisha kwa jina la Inspekta Mariam alipopewa nafasi ya kuzungumza na waumini katika kanisa moja baada ya misa.
Alisema ukatili dhidi ya wanawake na watoto unachukua sehemu kubwa ya idadi ya matukio yanayoripotiwa katika vituo vya polisi.
“Mpaka tumekuja hapa tumeona kuwa kupambana kwa kutumia sheria peke yake ni vigumu, tumeona labda tupate msaada wa kiroho kwa sababu wanaofanya haya ni miongoni mwa jamii na wengine ni waumini, kwa hiyo tumekuja ili kiroho muwasaidie wanaofanya hivyo vitendo,” alisema Inspekta Mariam.
Msemaji wa Jeshi la Polisi, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP), David Misime amefafanua uwepo wa mkakati huo, akisema unalenga kuyafikia makundi yote ya jamii na kuyashirikisha katika kupambana na uhalifu.
“Ni mkakati maalumu wa kuishirikisha jamii katika kupambana na uhalifu. Tumeamua kuyafikia makundi yote kuanzia watoto wa chekechea hadi watu wazima. Hii ni programu maalumu ya kufikia watu wote tukiamini kila mtu atashiriki kwa namna yake katika suala la ulinzi na usalama,” alisema Misime.
Kwa mujibu wa Misime, mkakati huo umeongezewa nguvu kubvwa na Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP) Camillius Wambura, ambaye anatajwa kutaka kujenga Jeshi la Polisi la kisasa na linalozingatia weledi zaidi.
“Baada ya IGP Wambura kuingia ameona kuwa nguvu ya uelewa wa pamoja ndiyo approach (njia) bora zaidi inayoweza kuzuia na kupambana na uhalifu nchini.
“Mfano siku hizi kuna matukio mengi ya watu wanaouana ndani ya nyumba, ukifuatilia unakuta walikuwa ni wapenzi. Sasa katika hali kama hii hata ukiweka doria kiasi gani haiwezi kusaidia. Watu wako ndani ya nyumba na wana mgogoro wamejifungia milango unajuaje?” alisema.
Tangu mwaka 2006, Jeshi la Polisi limekuwa likitekeleza mpango wa marekebisho wenye lengo la kulifanya jeshi hilo la kisasa zaidi, lenye askari wenye weledi na linaloshirikiana na jamii katika kubaini, kuzuia na kupambana na uhalifu.
Ndani ya mpango huo uliundwa utaratibu wa polisi jamii ambamo ndani yake kuna kipengele cha ushirikishwaji jamii.
“Uhalifu ni zao la jamii. Majambazi na wahalifu wengine wanatoka kwenye jamii zetu, wengine tunawapata makanisani na misikitini. Kwa hiyo tumeamua kufanya kazi na viongozi wa dini. Sisi tunafanya patrol (doria) za nje lakini wao (viongozi wa dini) wanafanya spiritual patrol (doria za kiroho),” alisema Misime.
Anasema jeshi limeona kuwa kuwashirikisha wananchi katika masuala ya ulinzi na usalama ndiyo njia ya uhakika ya kupambana na uhalifu wa aina zote.
“Ukiangalia trend (mwelekeo) ya dunia utaona tunalofanya ndilo upolisi wa kisasa unavyotaka na si upolisi wa maguvu.
“Mtu akiwa na uelewa mzuri kuhusu uhalifu, athari zake na jinsi ya kuuzuia atatoa elimu kwa wengine na hapo jamii itakuwa salama na mmomonyoko wa maadili utapungua ndani ya Taifa,” alisema.
Ubakaji, ulawiti tishio
Akizungumzia ongezeko la ubakaji na ulawiti, Inspekta Mariam aliwaomba waamini kuripoti matukio hayo katika madawati ya jinsia katika vituo vya polisi kwa kuwa huko watakutana na askari waliofundishwa kushughulika na masuala hayo na wanaofikika kirahisi.
“Hivi vitu vinafanyika huko mitaani na vingine majumbani. Kwa hiyo tunawaomba muwe mnaviripoti ili kusaidia, kwa sababu watoto wanaofanyiwa ukatili, watoto wanaolawitiwa baadaye wanakuwa na ile tabia na wanaipeleka mpaka shuleni, sasa tunatengeneza kizazi gani baadaye?
“Tutakuwa na Taifa la watu wakatili kwa sababu ukifanyiwa ukatili unakuwa katili zaidi ya yule aliyekufanyia,” alisema.
Mkuu wa Ushirikishwaji Jamii Wilaya ya Kinondoni, Kamishna Msaidizi wa Polisi, Ally Wendo aliungana na Misime kuwa IGP Wambura ameamua kuiongezea nguvu kamisheni ya ushirikishwaji wa jamii.
“Sasa hivi kila kata ina askari wa cheo cha nyota moja, kazi kubwa ya huyo mkaguzi ni kushirikiana na viongozi wa kata pamoja na wananchi katika kupambana na uhalifu. Mfano, mkoa wetu wa Kinondoni una kata 35 na kila kata ina mkaguzi kata ambaye anatusaidia,” alisema.
Bakwata, TEC wanena
Mwenyekiti wa Halmashauri Kuu ya Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata), Sheikh Khamis Mataka ameupongeza mkakati huo wa polisi, akisema ni stratejia rafiki itakayoleta matokeo chanya kuliko ile ya matumizi ya nguvu.
“Ni jambo jema kwa sababu kadiri dunia inavyoendelea wahalifu wanatumia akili zaidi, yaani uhalifu ni suala la mentality (tabia) ya watu, kwa hiyo kinachochezewa hapa ni akili ya binadamu. Kwa hiyo matumizi ya nguvu yanakuwa hayana matokeo chanya sana. Akili huwa haiogopi nguvu. Akili iliyochezewa hupata msaada mkubwa zaidi ikielimishwa. Kwa hiyo polisi kwenda ndani ya nyumba za ibada ni sahihi,” anasema.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Padri Charles Kitima alisema jambo hilo ni jema, huku akitoa angalizo kuwa ili mkakati huo uwe endelevu na ufanikiwe, uelewa huo ungeanza kutolewa kwa viongozi wa dini kwanza ili nao wawashirikishe vizuri zaidi waumini wanaowaongoza.
“Ni jambo zuri kwa kuleta awareness (uelewa) kubwa lakini ni vema uwashirikishe viongozi wa dini kwanza. Fikiria ukiwaelimisha mapadri, makatekista, wenyeviti wa jumuiya ndogo ndogo utakuta ndani ya mwezi mmoja uelewa utakuwa umefika nchi nzima.
“Tuna ibada 20,000 kila Jumapili, tuna jumuiya ndogo ndogo 67,000, sasa utapata wapi askari wa kwenda kote huko. Kwa hiyo utaona wangewakusanya waendesha ibada ili nao wawafikishie ujumbe waamini,” alisema.
Aliongeza kuwa ni haki kwa wasimamizi wa sheria kutumia majukwaa ya kanisa na hata jumuiya ndogo ndogo, ukiwajengea uwezo viongozi wanaoendesha ibada unakuwa na uhakika zaidi wa ujumbe kuwafikia watu wengi kwa wakati mmoja na inaleta sustainability (uendelevu),” alisema Kitima.