Mnara mpya wa mawasiliano baharini kujengwa Mtwara

Muktasari:
- Tasac imejipanga kujenga mnara wa mawasiliano ya baharini mkoani Mtwara ili kuboresha huduma za kimawasiliano na usiri wa taarifa.
Mtwara. Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (Tasac), Kapteni Mussa Mandia amesema wakala huo utahakikisha ujenzi wa mnara mpya wa mawasiliano baharini mkoani hapa unakuwa wa viwango na wenye ubora.
Akizungumza wakati wa ziara yake ya siku tatu mkoni hapa jana Jumanne Novemba 7, 2023 ambapo walitembelea bandarini mkoani hapa amesema kuwa wameona mapungufu makubwa ya kimawasiliano hivyo suluhu yake ni ujenzi wa mnara wa kisasa.
“Tumeona mapungufu ambayo inabidi yafanyiwe kazi ambapo tuna taarifa kuwa mnara mpya unatengenezwa mkubwa na sisi kama wadhibiti tutahakikisha unajengwa kwa vigezo vinavyotakiwa kwakuwa eneo letu ni kubwa zaidi ya kilomita 1,224 kutokea nchini Kenya na kuteremka mpaka maingilio ya mto Ruvuma.
“Kutokana na umbali huo mpaka Dar es salaam tumeona kituo kimoja hakitoshi kuwa na mnara mmoja tunategemea kuwa na mnara mwingine hapa Mtwara ili kuboresha usalama wa safari za baharini,” amesema Mandia
Katika hatua nyingine wametembelea bandari ya mtwara na kuridhishwa na maandalizi ya ujenzi wa bandari ya mizigo michafu katika eneo la Kisiwa Mgao.
“Kiasili bandari hii imejengwa kwa ajili ya mizigo misafi kwenye kontena na makaa ya mawe inakuja katika kichele ikiwa na mavumbi mengi hiyo ni changamtoo lakini tunaona jitihada zinafanyika na bandari kujenga bandari maalum ya kuhudumia mizigo michafu na tumejiridhisha kama bodi na wadhibiti” amesema Kepten Mandia
kwa upande wake Mkurugenzi wa udhibiti wa ulinzi usalama wa vyombo vya maji baharini pamoja na utunzaji wa mazingira ya bahari TASAC, Leticia Mutaki amesema kuwa wamekuwa wakikagua shughuli mbalimbali za udhibiti, usalama wa vyombo na ulinzi wa bahari na uchafuzi wa mazingira unaotokana na meli.
“Vipo vyombo vikubwa tunavipa usajili na vidogo ambavyo tunavipa leseni ambapo kabla tunavikagua ili kujiridhisha vina ubora na usalama wa uhakika wa kuweza kutoa huduma ili kuweza kuepukana na majanga yanayoweza kutokea baharini,”amesema.