Mnyika asema hawajui Mbowe alipo

Wednesday July 21 2021
mnyika pic
By Elizabeth Edward

Dar es Salaam. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimesema hakijui alipo mwenyekiti wa chama hicho Taifa, Freeman Mbowe hivyo kimemtaka Rais Samia Suluhu Hassan kuvielekeza vyombo vya ulinzi na usalama kumtafuta mwenyekiti wa chama hicho aliyetoweka katika mazingira ya kutatanisha akiwa hotelini jijini Mwanza.

Mbowe aliyekuwa jijini humo tayari kwa ajili ya kongamano la kudai Katiba Mpya lililoandaliwa na chama hicho.

SOMA: Polisi wazingira hoteli kongamano la Chadema

Akizungumza na wanahabari leo Jumatano Julai 21, 2021, Katibu Mkuu wa cha hicho, John Mnyika amemtaka Rais Samia kuingilia kati na kutoa maelekezo ya kurejeshwa kwa kiongozi huyo wa chama sambamba na kuachiwa huru kwa wanachama 11 wa Chadema waliokamatwa.

Sanjari na hilo Mnyika ameeleza kuwa kamati kuu ya chama itakutana kesho kujadili kuhusu tukio la kutoweka kwa mwenyekiti wao aliyechukuliwa na watu waliojitambulisha kuwa ni polisi

SOMA: Ukumbi kongamano la Chadema wasalia mtupu

Advertisement

Mnyika pia ameelekeza wanachama wa chama hicho kokote nchini kuanza hatua za kumtafuta mwenyekiti huyo katika njia watakazoona zinafaa.

“Popote alipo mwanachama au kiongozi wa Chadema ashiriki kudai mwenyekiti apatikane, hadi sasa hatujui alipo hivyo tusisite kuhoji, kudai na kushinikiza aachiwe alipo,” amesema Mnyika.

Advertisement