Njia zinazoenda hotelini pia zafungwa

Muktasari:

Askari Polisi waliojihami kwa silaha za moto na mabomu ya kutoa machozi wamezingira na kufunga njia za kuingia na kutoka hoteli ya Tourist (zamani Tai Five) eneo la Kitangiri ambako kongamano la Katiba Mpya lililoandaliwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) lilitarajiwa kufanyika leo Julai 21.

Mwanza. Askari Polisi waliojihami kwa silaha za moto na mabomu ya kutoa machozi wamezingira na kufunga njia za kuingia na kutoka hoteli ya Tourist (zamani Tai Five) eneo la Kitangiri ambako kongamano la Katiba Mpya lililoandaliwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) lilitarajiwa kufanyika leo Julai 21.

Pamoja na uwepo wa askari polisi, njia ya kuingia eneo la hoteli hiyo pia umefungwa utepe maalum kuzuia watu kuingia huku barabara kutoka Kona ya Bwiru kwenda Kitangiri iliko hoteli ya Tourist nayo ikiwa imefungwa kwa kutumia magari ya polisi.

Kila anayepita njia hiyo uhojiwa kabla ya kuruhusiwa kupita au kuzuiwa kwa kutakiwa kupita njia nyingine.

Waandishi wa Mwananchi wamefika katika hoteli hiyo na kushuhudia magari matano ya polisi likiwemo la kubeba watuhumiwa na wafungwa maarufu kama karandinga yakiwa yameegeshwa nje na ndani ya uzio wa hoteli.

Kitendo cha askari Polisi kuzingira hoteli na kufunga njia inayoenda hotelini hapo kunakuja huku kukiwa na taarifa zinazosambaa kupitia mitandao ya kijamii zikidai kuwa Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Freeman Mbowe na viongozi wengine 10 wa chama hicho kushikiliwa na polisi.

Alipotafutwa na Mwananchi kwa njia ya simu leo Julai 21, Kamanda wa Polisi mkoa wa Mwanza, Ramadhani Ng’anzi kuhusu taarifa hizo alisema kuwa yuko msikitini hivyo hawezi kuzungumzia hilo kwa sasa.

“Nani wewe? Aaahaaa…..hebu subiri kwanza niko msikitini siwezi kuzungumzia hilo kwa sasa,” amesema Kamanda Ng’anzi na kukata simu

Ujumbe mfupi wa maneno aliotumiwa Kamanda Ng’anzi kutaka kupata uthibitisho wa taarifa hizo pia haukujibiwa.

Imeandikwa na Peter Saramba, Saada Amir na Mgongo Kaitira


Fuatilia mitandao ya Mwananchi kwa taarifa zaidi