VIDEO: Ukumbi kongamano la Chadema wasalia mtupu

Ukumbi kongamano la Chadema wasalia mtupu

Muktasari:

Hadi saa 5:50 asubuhi ya Jumatano Julai 21, ukumbi wa mikutano wa hoteli ya Tourist (zamani Tai Five) ulilopo eneo la Kitangiri jijini Mwanza uliotarajiwa kutumika kwa ajili ya kongamano la Katiba Mpya lililoandaliwa na Chadema ulilikuwa tupu baada ya washiriki kushindwa kuingia kutokana na hiteli hiyo kuzingirwa na askari wa Jeshi la Polisi.

Mwanza. Hadi saa 5:50 asubuhi ya Jumatano Julai 21, ukumbi wa mikutano wa hoteli ya Tourist (zamani Tai Five) ulilopo eneo la Kitangiri jijini Mwanza uliotarajiwa kutumika kwa ajili ya kongamano la Katiba Mpya lililoandaliwa na Chadema ulilikuwa tupu baada ya washiriki kushindwa kuingia kutokana na hiteli hiyo kuzingirwa na askari wa Jeshi la Polisi.

Ukumbi wa Tourist Hoteli eneo la Kitangiri jijini Mwanza uliotarajiwa kutumika kwa ajili ya kongamano la Katiba Mpya lililoandaliwa na Chadema ukiwa mtupu saa 5:50 asubuhi. Kongamano hilo lilipangwa kuanza saa 2:00 asubuhi. Picha na Mgongo Kaitira

Mwananchi Digital imeshuhudia ukumbi huo uliojaa viti ukiwa umepambwa kwa vitambaa vyenye nembo na rangi za Chadema ikiashiria uwepo wa shughuli za kisiasa za chama hicho Kikuu cha upinzani nchini.

Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na Chadema jana Jumanne Julai 20 ilionyesha kuwa kongamano hilo lililotarajiwa kushirikisha makundi mbalimbali ya kijamii lingeanza saa 2:00 asubuhi.

Njia za kuingia na kutoka hotelini hapo zimefungwa utepe maalum wa polisi kuzuia watu kuvuka ambapo wachache wakiwemo waandishi wa habari huruhusiwa baada ya kujieleza kwa askari walioweka doria na ulinzi ukiwemo wa kikosi cha mbwa.

Ndani na nje ya uzio wa hoteli hiyo kumeegeshwa magari ya polisi likiwemo lenye maji ya kuwasha maarufu kama washawasha.

Njia zote zinazoenda eneo la Kitangiri ilipo Tourist Hotel zimefungwa kwa utepe na magari ya polisi kuanzia Kona ya Bwiru ambapo ni watu wachache wanaotoa maelezo yanayowaridhisha askari polisi ndio huruhusiwa kupita.

Imeandikwa na Peter Saramba, Mgongo Kaitira na Saada Amir.