Mnyika: Nitagombea tena ubunge Kibamba

Muktasari:

Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika amesema atagombea tena ubunge Kibamba katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba, 2020.

Dar es Salaam. Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika amesema atagombea tena ubunge Kibamba katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba, 2020.

Mnyika ambaye alichaguliwa kuwa katibu mkuu wa Chadema Desemba 20, 2019 ameeleza hayo leo Jumatano Januari 29, 2020 katika mahojiano maalum yaliyorusha moja kwa moja na Kituo cha Televisheni cha ITV.

Alipoulizwa kama atagombea tena ubunge katika jimbo hilo aliloliongoza tangu mwaka 2015,  Mnyika amewataka wananchi wajiandae kumchagua kuwa mwakilishi wao bungeni.

Amesema kwa kuwa wananchi walimchagua kuwa mbunge mwaka 2015 akiwa naibu katibu mkuu wa Chadema, pia watamchagua akiwa katibu mkuu wa chama hicho kikuu cha upinzani nchini.

“Nitagombea Kibamba nawaomba wananchi kwa unyenyekevu mkubwa ikifika wakati wa kampeni za uchaguzi wanipe ubunge mwaka 2020.”

“Kulikuwa na shida sana ya maji  Ubungo na Kibamba lakini kwa muda ambao nimewatumikia wananchi nimepigania sana na ajenda ya maji, na sehemu kubwa ya jimbo wamepata maji,” amesema Mnyika.

Mnyika alikuwa mbunge wa Ubungo mwaka 2010, mwaka 2015 aligombea ubunge Kibamba baada ya jimbo la Ubungo kugawanya na kuzaliwa jimbo jipya la Kibamba. Mbunge wa Ubungo ni Saed Kubenea (Chadema).