Mnyika: Safu ya Chadema sasa imekamilika

Muktasari:

  • Katibu Mkuu wa Chadema John Mnyika amesema anaona faraja kuona safu nzima ya chama hicho umekamilika.

Dar es Salaam. Katibu Mkuu wa Chadema John Mnyika amesema anaona faraja kuona safu nzima ya chama hicho umekamilika.

Mnyika ametoa kauli hiyo leo Jumatano, Januari 25, 2023, katika uwanja wa Bulyaga uliopo Temeke jijini Dar es Salaam wakati wa mkutano wa hadhara wa kumpokea Makamu Mwenyekiti wa chama hicho Tundu Lissu aliyekuwa uhamishoni nchini Ubelgiji.

Amesema wakati mwingi amekuwa akijikuta yuko mwenyewe na wakati mwingine amekuwa na Mwenyekiti wa chama hicho Freeman Mbowe kutokana na mazingira yaliyokuwapo hapa nchini.

"Baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2023 kumalizika ambao wewe (Lissu) ulikuwa mgombea urais ulipomalizika wewe uliondoka na Mwenyekiti Mbowe akaondoka baadae alirudi na kuanza kudai Katiba mpya lakini alikamatwa na kufunguliwa kesi,"amesema Mnyika

"Leo hii nina furaha Makamu Mwenyekiti umerejea na safu yote imekamilika naamini tutaendeleza mapambano kuelekea Uchaguzi Mkuu mwaka 2025 kushika dola,"

Mnyika amemwambia Lissu amesikia malalamiko ya wananchi juu ya bei za bidhaa kuwa juu hivyo anaamini atamfikishia Rais Samia Suluhu Hassan taarifa.


Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu (Zanzibar), Salum Mwalimu amesema nafasi ya urais ameikaimu kwa miaka miwili hivyo anamkabidhi Lissu nafasi hiyo.

Mwalimu alikuwa mgombea mwenza katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020.

"Ni miaka miwili sasa naona furaha kumkabidhi Lissu nafasi yake ya urais kwa furaha na unyenyekevu mkubwa"amesema Mwalimu.