Mnyika: Walioapishwa walijiteua, hawakuteuliwa na Chadema

Wednesday November 25 2020
chadema pic
By Herieth Makwetta

Dar es Salaam. Katibu mkuu wa Chadema, John Mnyika amesema wanachama 19 wa chama hicho walioapishwa kuwa wabunge wa viti maalum  hawakuteuliwa na chama hicho, “hawana baraka za chama wala uongozi. Kundi hilo la wabunge wa viti maalum limejiteua lenyewe.”

 Mnyika ameeleza hayo leo Jumatano Oktoba 25, 2020 katika mkutano na waandishi wa habari wakati akieleza tukio la wanachama 19 wa Chadema wakiongozwa na mwenyekiti wa Baraza la Wanawake la chama hicho (Bawacha), Halima Mdee kuapishwa jana Jumanne na Spika Job Ndugai kuwa wabunge wa Viti Maalum.

Katibu mkuu huyo amesema kulikuwa na mawasiliano ya mara kwa mara kati ya chama hicho na  Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kupitia mkurugenzi wake, Dk Wilson Mahera na mawasiliano ya mwisho yalifanyika Novemba 11, 2020.

Amesema mawasiliano hayo ilikuwa barua kutoka Chadema kwenda NEC ikikana kuteua majina ya wabunge 19 wa viti maalum ambayo yalidaiwa kuwa yameshawasilishwa bungeni.

“Kwa mujibu wa utaratibu wa kikatiba wa mchakato wa viti maalum unaopatikana kwenye ibara ya 78 ibara ya tatu wanaopelekwa wanatakiwa kuwa wamekidhi vigezo kwa kujaza fomu maalum kuomba nafasi hiyo, na si viongozi kupeleka mtu bali fomu namba 8 D.”

“Tume ilituletea fomu hizi ili tutakaowateua tupeleke orodha ya majina 113 mimi kama katibu mkuu hakuna fomu ya mtu yoyote niliyowahi kuijaza popote  kuthibitisha uteuzi wa yeyote. Mchakato huo wote haujafanyika bali ni mchakato wa kughushi uliohusisha hao waliokwenda kuapa bila ridhaa ya chama wala mamlaka halali,” amesema Mnyika.

Advertisement

Mnyika amesema vyombo vya habari vinapaswa kuwauliza NEC kujua majina hayo yametolewa na nani, “mpaka ninavyozungumza na ninyi sijaletewa ushahidi na yeyote juu ya uhusika na mtu yeyote ndani ya  ofisi ya katibu mkuu kushirikiana na mfumo kufanya jambo hili, jambo ambalo nina uhakika na hao watu 19 waliokwenda kuapa walishiriki katika huu ubatili na wana fahamu hilo nina uhakika bila shaka yoyote.”

Advertisement