Moshi watoa ‘vifurushi’ vya majeneza, mazishi

Muktasari:

  • Katika mpango huo, mteja akinunua jeneza mapema kabla ya kifo chake ana uhakika wa kupata punguzo la bei hadi asilimia 30 pamoja na ofa ya huduma ya matengenezo ya kaburi kama atakubaliana na watoa huduma.

Moshi. Kama ulidhani vifurushi vya muda wa maongezi na data vinatolewa na kampuni za simu za mkononi pekee, utakuwa unakosea; sasa kuna vifurushi vya majeneza.

Tena si tu vifurushi, bali sasa huduma ya mazishi, kaburi na shughuli nyingine za kuwalaza ndugu waliofariki katika nyumba zao za milele, zimerahisishwa.

Mteja akinunua jeneza mapema kabla ya kifo chake, ana uhakika wa kupata punguzo la bei la hadi asilimia 30, lakini pia atakuwa na uhakika wa huduma nyingine za matengenezo ya kaburi kama atakubaliana na watoa huduma.

“Unajua kila mtu lazima afe na ndiyo maana watu wanaandika wosia,” alisema Macmillan Siraki, mkurugenzi wa kampuni ya Godmark Funeral Directors ya mjini Moshi iliyoanzisha huduma ya vifurushi hivyo vya majeneza.

“Unapanga vitu vyako ukiwa hai. Ukishakufa watu watakupangia. Hawatapanga kama wewe unavyotaka

“Hata jeneza, hakuna atakayekununulia kama ulivyotaka wewe wakati ukiwa hai. Kuna baadhi ya watu hawathamini mtu akishakufa na pengine hata fedha ya jeneza ni ya kwake.

Alisema walipoanzisha huduma hiyo ya punguzo, watu wengi walijitokeza.

“Wapo walioonyesha interest (nia) na baadhi wameshatoa oda. Lakini makubaliano yetu ni kutunza siri hii hawataki iwe public (hadharani),” alisema Siraki.

“Walikuwa wanauliza tu maswali kama miundo inapobadilika inakuwaje lakini tumekubaliana kama ikitoka design (muundo) mpya akiwa hai, tutambadilishia labda kama atataka la gharama zaidi.

“Mara nyingi hatuongezi fedha. Kama mtu amekuachia fedha yake maana yake na wewe umeitumia kuzungusha kwenye biashara. Huna sababu ya kuongeza bei zaidi ya kumpa design nzuri iliyotokea.”

Siraki alikuwa akizungumza katika mahojiano maalumu na Mwananchi juzi na kusema mbali na punguzo hilo, kampuni hiyo ina mpango wa kujenga chumba cha kuhifadhia maiti na mteja atakayenunua kifurushi cha huduma kwao, atanufaika na huduma ya kuhifadhiwa bure maiti yake.

Alisema kampuni hiyo pia itatoa huduma mpya ya mazishi ambayo itaondoa kazi ya kuchanganya zege makaburini.

Majeneza mjini hapa huuzwa kati ya Sh390,000 na Sh1.5 milioni kulingana na ubora wake.

“Kama mteja atanunua jeneza lake akiwa hai, atapata punguzo la asilimia 30 ya bei,” alisema Siraki.

Mkurugenzi huyo alisema tangu watangaze ofa hiyo, wameshapata wateja saba ambao wameagiza watengenezewe majeneza na wameshalipia.

Aliwatoa hofu watu kutokana na dhana iliyojengeka kuwa ukinunua jeneza lako ukiwa hai, itakuwa ni kujitafutia balaa, akisema jeneza halina tofauti na kabati la vyombo nyumbani.

“Hii ni kutoelewa tu. Jeneza ni kama kabati tu isipokuwa tofauti yake ni kwamba jeneza linalazwa chini. Tuondokane na dhana hii tupange misiba yetu tukiwa hai. hata ukifa unakuwa unajua jeneza lako likoje,” alisema.

Akizungumzia changamoto katika utengenezaji wa majeneza, mkurugenzi huyo alisema kuna wakati inamlazimu kuingia ndani ya jeneza ili kuhakikisha kama vipimo vya marehemu viko sawa.

“Huwezi kumwambia mtu niletee maiti. Mafundi ni waoga. Wanadhani wakiingia humo watakufa. Unalala wewe, unamwambia hapa tunatakiwa tuongeze kipimo fulani,” alisema Siraki.

Hakuna kuchanganya zege

Mbali na majeneza ya kisasa, hivi sasa waombolezaji wengi hufunika makaburi kwa zege ambalo huchanganyiwa makaburini na hivyo shughuli hiyo kuchukua muda mrefu.

Lakini Siraji alisema wamebuni ‘bidhaa’ mpya ya vipande vyepesi vya zege.

“Sasa hivi tuna slab (vipande vya zege) ambavyo kaburi likishafunikwa, tunaweka tombstone ambayo ni mabble (marumaru) ambayo ina jina na taarifa nyingine za marehemu,” alisema.

“Hizi slab ni vipande kama vitano hivi huna haja tena ya kumwaga zege kwenye kaburi. Hivi vipande vinabebwa na watu wawili tu na kuunganishwa juu ya kaburi na baadaye tunakuwekea mabble.

“Hii ni aina mpya ambayo tumekuja nayo na inapunguza gharama, muda na nguvu kazi. Tunaangalia namna tunavyopunguza gharama sio watu wanasubiri mpaka zege ichanganywe, wajengee.”

Wakazi wa Kilimanjaro wanajulikana kwa kuweka uzito katika shughuli za mazishi na mara nyingi hupumzisha miili ya wapendwa wao katika maeneo yao ya makazi.

Itaendelea kesho