Moto ulioteketeza maduka ya vipodozi wazimwa
Muktasari:
- Chanzo cha moto huo kinahisiwa kuwa ni hitilafu ya umeme, huku Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda akisisitiza uchunguzi wa kina
Mwanza. Hatimaye moto ulioanza majira ya saa moja na nusu usiku wa kuamkia leo katika maduka ya vipodozi yaliyopo eneo la Lumumba, jijini Mwanza, umedhibitiwa na kuzimwa baada ya juhudi kufanywa na Jeshi la Zimamoto kwa zaidi ya saa tano.
Akizungumza katika eneo la tukio, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda amesema hadi kufikia saa sita usiku hakukuwa na taarifa ya madhara ya vifo wala majeruhi.
Amesema uharibifu mkubwa umehusisha maduka kadhaa pamoja na jengo moja lililoshika moto kwa kiwango kikubwa.
Gari la zimamoto wakati likiendelea na uzimaji moto katika maduka ya vipodozi yaliyoteketea jijini Mwanza. Picha na Saada Amir
Ameeleza kuwa hali ya usalama iliimarishwa tangu mwanzo wa tukio, huku vikosi vya Jeshi la Polisi na Jeshi la Wananchi vikihakikisha mali za wananchi zinalindwa na hakuna tukio la wizi lililoripotiwa.
Hata hivyo, amebainisha kuwa baadhi ya wananchi walihamisha mali zao kwa hofu licha ya kupewa tahadhari kuwa hakuna ulazima huo.
"Nilipigiwa simu na mwananchi akisema anaona moto na mimi ikabdi nipigie Zimamoto...waliwahi na kudhibiti moto usisambae," amesema Mtanda.
Gari la zimamoto likiendelwa kuzima moto ulioteketeza baadhi ya maduka ya vipodozi Mtaa wa Lumumba jijini Mwanza. Picha na Saada Amir
Amesema chanzo cha moto kinahisiwa kuwa ni hitilafu ya umeme, huku akisisitiza kuwa uchunguzi wa kina pamoja na tathmini ya hasara utaendelea kufanywa na vyombo husika vya Zimamoto na uokoaji kabla ya kutolewa taarifa rasmi.
Ameongeza kuwa huduma za dharura zimeimarishwa, ikiwamo uwepo wa magari ya wagonjwa kwa ajili ya kuwahudumia wananchi watakaopata madhara kama mshtuko au presha kutokana na tukio hilo, huku akiahidi kuwa Serikali itakutana na waathirika ili kujadili hatua zinazofuata.
Mbunge wa Nyamagana, John Nzilanyingi amesema tukio hilo limeonesha umuhimu wa uwekezaji katika vifaa vya kisasa vya Zimamoto, akisisitiza kuwa hali ingeweza kuwa mbaya zaidi bila uwepo wa vifaa hivyo.
Baadhi ya wafanyabiashara wa maduka ya vipodozi, mtaa wa Lumumba jijini Mwanza wakiokoa mali zao. Picha na Saada Amir
Amepongeza ushirikiano uliooneshwa na wananchi katika kukabiliana na moto huo, akieleza kuwa baadhi yao walishiriki moja kwa moja katika juhudi za uokoaji, ikiwemo kuvunja milango na kusaidia kuongoza maji.
Ametoa wito kwa wananchi na wafanyabiashara kuzingatia sheria za mipango miji wanapojenga, akibainisha kuwa uwepo wa njia za vichochoro umesababisha changamoto kwa magari ya Zimamoto kufika kwa urahisi katika baadhi ya maeneo.
Shuhuda wa tukio, Emmanuel Mushi amesema tukio hilo ni la kusikitisha na bila juhudi za vikosi vya ulinzi kushirikiana, hasara ingekuwa kubwa kwa kuwa vipodozi hususani pafyumu, vilikuwa vikilipuka kwa kasi.
"Kilichotokea leo ni jambo linaloumiza... hata hivyo tunalipongeza jeshi la uokoaji na Serikali ya mkoa, waendelee kutupigania majanga kama hayo yanapotokea," amesema.
Katika tukio hilo, zaidi ya magari manane yalishiriki yakiwamo kutoka Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, Jeshi la Polisi pamoja na Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), kwa pamoja yalifanikiwa kudhibiti moto huo na kuzuia madhara zaidi.