Vifo vya joto kali vyafikia 3,700 Ulaya, Tanzania yashuhudia baridi kali
Muktasari:
- Wakati joto kali likiua maelfu ya watu barani Ulaya, Tanzania inaendelea kushuhudia baridi katika baadhi ya mikoa, hali inayohusishwa na mabadiliko ya tabianchi.
Dar es Salaam. Wakati baadhi ya mikoa ya Tanzania ikiendelea kushuhudia hali ya baridi katika kipindi hiki cha msimu wa mwaka, mataifa ya Ulaya yanakabiliwa na athari mbaya za wimbi la joto kali lililosababisha vifo vya watu 3,700 ndani ya siku tisa.
Hata hivyo, wataalamu wa hali ya hewa wamesema kuwa idadi hiyo huenda ikaongezeka kadiri tathmini rasmi zinavyoendelea kukamilika.
Kwa mujibu wa taarifa zilizoripotiwa na vyombo mbalimbali vya habari vya kimataifa, zikirejea uchambuzi wa watafiti wa afya na tabianchi, mawimbi ya joto yaliyodumu kati ya Juni 20 na 28, 2026, yamesababisha halijoto kuzidi nyuzi joto 40 katika maeneo mengi ya Ulaya Magharibi, hususan nchini Ufaransa, Ubelgiji na Uholanzi.
Uchambuzi huo umebainisha kuwa watu 3,700 wamefariki dunia kutokana na athari zinazohusishwa na joto hilo kali, huku asilimia 80 ya vifo hivyo vikihusisha watu wenye umri wa miaka 65 na kuendelea.
Mamlaka ya Afya ya Umma ya Ufaransa imeeleza kuwa takwimu hizo ni za awali na huenda zikaongezeka baada ya uchambuzi wa kina kukamilika.
Katika taarifa yake, mamlaka hiyo imesema: "Idadi ya vifo itakuwa kubwa zaidi kuliko takwimu hizi za awali zinavyoonesha."
Nchini Ufaransa pekee, zaidi ya vifo 2,000 vimeripotiwa katika kipindi hicho, huku hospitali na vituo vya kulelea wazee vikishuhudia ongezeko kubwa la wagonjwa waliopata matatizo yanayohusiana na joto kali.
Serikali ya nchi hiyo imeongeza tahadhari za afya kwa makundi yaliyo hatarini, hususan wazee, watoto na watu wenye magonjwa sugu.
Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) limesema Ulaya ndiyo bara linaloongezeka joto kwa kasi zaidi duniani kutokana na mabadiliko ya tabianchi.
Mkuu wa Kitengo cha Huduma za Hali ya Hewa wa shirika hilo, John Kennedy, amesema mawimbi ya joto kama yanayoshuhudiwa sasa yanatarajiwa kutokea mara nyingi zaidi kadiri joto la dunia linavyoendelea kuongezeka, akisisitiza kuwa hali hiyo inaendana na utabiri wa kisayansi kuhusu athari za mabadiliko ya tabianchi.
Tanzania yashuhudia baridi kali
Wakati Ulaya ikikabiliwa na athari hiyo ya joto kali, Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imeendelea kutoa taarifa zikionesha kuwa baadhi ya mikoa, hususan ile ya Nyanda za Juu Kusini pamoja na maeneo mengine kadhaa, inaendelea kushuhudia hali ya baridi kali katika kipindi hiki.
Kwa mujibu wa TMA, mikoa inayotarajiwa kuendelea kuwa na baridi ni Mbeya, Songwe, Njombe, Iringa, Rukwa, Katavi, Ruvuma na baadhi ya maeneo ya mikoa ya Kilimanjaro, Arusha na Manyara, huku maeneo mengine yakitarajiwa kuwa na vipindi vya ukungu na upepo mkali na baridi nyakati za asubuhi na usiku.
Wataalamu wa tabianchi wanaeleza kuwa kuwepo kwa baridi katika baadhi ya maeneo ya Tanzania hakupingi ukweli wa ongezeko la joto duniani.
Badala yake, hali hiyo inaonesha namna ambavyo mabadiliko ya tabianchi yanavyobadilisha mifumo ya hali ya hewa duniani, ambapo baadhi ya maeneo hukumbwa na joto kali lisilo la kawaida na mengine yakishuhudia baridi kali au vipindi virefu vya hali ya hewa isiyo ya kawaida.
Huku idadi ya vifo Ulaya ikiendelea kufuatiliwa na mamlaka za afya, mashirika ya kimataifa yamezitaka serikali duniani kuimarisha mifumo ya tahadhari, kuwekeza katika mikakati ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kuwalinda zaidi wananchi walio katika makundi hatarishi ili kupunguza madhara yanayotokana na matukio makubwa ya hali ya hewa.
Waziri Mkuu wa Ufaransa shakani
Wakati huo huo, kutokana na athari za wimbi la joto, ambalo nchini Ufaransa limesababisha vifo vya zaidi ya watu 2,000, Waziri Mkuu wa nchi hiyo, Sebastian Lecornu, anakabiliwa na shinikizo la kutaka ajiuzulu kwa madai kwamba serikali yake ilishindwa kukabiliana na hali hiyo.
Wakiwasilisha hoja hiyo jana, wabunge wa Chama cha Green wanadai serikali haikuwa imejiandaa vya kutosha kukabiliana na mawimbi ya joto yaliyosababisha maelfu ya vifo, ingawa wachambuzi wengi nchini humo wanaona uwezekano wa serikali kuangushwa ni mdogo kwa kuwa upinzani bado hauna kura za kutosha bungeni.