Moto wa kikokotoo wazidi kuwaka bungeni, Gambo akikomalia

New Content Item (1)

Muktasari:

  • Mbunge Mrisho Gambo ameliomba Bunge liunde kamati kushughulikia kikokotoo cha mafao ya wastaafu, hoja yaungwa mkono na Mbunge Florent Kyombo.

Dodoma. Suala la kikokotoo cha mafao ya wastaafu limeendelea kuwa mjadala safari hii Mbunge wa Arusha Mjini (CCM), Mrisho Gambo ameingia bungeni na vielelezo vinavyoonyesha wastaafu wanavyopunjwa mafao.

Mbali na hayo, Gambo pia ameshauri Bunge liunde kamati maalumu kwa ajili ya kushughulikia changamoto ya kikokotoo na ametaka wafanyakazi waliokutwa na sheria ya  kikokotoo waendelee na ukokotoaji wa sheria ya kabla ya Julai 2014, pia kikokotoo cha sasa kinawapunja wafanyakazi hadi Sh54 milioni.

Hoja hiyo imeungwa mkono na Mbunge wa Jimbo la Nkenge, Florent Kyombo ambaye amesema; “Kwa kweli wabunge tukianza kufikiri jambo hili ni la watu wa upinzani si kweli, jambo hili ni letu tulipitisha sisi wenyewe hapa tukiwa Bunge lenye wabunge wengi wa CCM na jambo hili linatuhitaji sisi turudie upya tujadili jambo hili upya na lije mbele yetu.”

Kikokotoo  ambacho ni matokeo ya makubaliano ya pamoja kati ya Serikali, Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (Tucta) na Chama cha Waajiri Tanzania (ATE) ambacho kilianza kutumika Julai 1, 2022 ni mwendelezo wa hoja zilizoanza  wiki iliyopita likiibuliwa na Ester Bulaya,  Jane Jerry na  Kasalali Mageni.

Gambo na Kyombo kama ilivyokuwa wiki iliyopita kwa Bulaya, Jerry na Mageni, wamesema hayo wakati wakichangia hotuba ya Ofisi ya Waziri Mkuu ya makadirio ya mapato na matumizi ya Ofisi yake na ofisi ya Bunge kwa mwaka  2024/2025, leo Jumatatu, Aprili 8, 2024.

Gambo ameanza kwa kusema; “Nitajitahidi leo angalau kwa asilimia zisizopungua 90 nichangie kikokotoo, kama muda utabaki ndio nitaangalia masuala mengine.”

Mbunge huyo amesema nchi ina bahati kwa kuwa Rais Samia  mara kadhaa alipokuwa anazungumza na jamii amekuwa anaonyesha nia ya kutaka kikokotoo kifanyiwe kazi kwa masilahi mapana ya wafanyakazi.

Gambo alimnukuu Rais Samia kwenye hotuba yake ya Mei mosi 2020 alipozungumza kwenye sherehe za wafanyakazi zilizofanyika Dodoma kwamba.

“Kwenye ukurasa wa 18, sambamba na suala la malipo ya mafao limetajwa pia suala la kupanda kikokotoo kitakachotoa faraja kwa wastaafu, nashukuru Tucta wametaja mpaka kiwango kwa muda mrefu tumekuwa tukivutana kutoka 25 (aslimia 25) kwenda 50 (asilimia 50), lakini Tucta wamesema tukutane katikati.

“Sasa Serikali tutakwenda kukaa katika utatu wetu au sisi na Tucta kuangalia tunavyoweza kufanya, lakini wazo mliokuja nalo si baya,” Gambo alinukuu kauli ya Rais Samia kutoka kwenye yake ya siku ya Wafanyakazi duniani.

Gambo amesema hiyo ni ishara kwamba Rais yuko tayari kwenye suala la kikokotoo na amenukuu tena hotuba ya Rais Samia ya Septemba 3, 2023 alipozungumza na askari polisi.

“Kikokotoo tupo tunakifanyia kazi na kuona jinsi ambavyo tunaenda vizuri,” ilikuwa na kauli ya Rais Samia ambayo Gambo ameinukuu.

“Maneno haya yanaonyesha kabisa sisi tuliobaki tuna kazi kubwa ya kufanya kuhakikisha tunamsaidia Rais kwenye nia yake njema hii kwa wafanyakazi.

“Lakini, nimeweza pia kupitia kanuni mbalimbali kama hii Mei 20, 2022, kanuni pia ya Agosti 17, 2018, nimepitia pia sheria ya SSRA (Mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii-SSRA) ya 2008, na nimeweza pia kupitia kanuni ya SSRA ya Julai 17, 2018. Lakini pia na maoni ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya 2017 pamoja na maoni ya Kambi ya Upinzania ya 2017.

“Ukiangalia kwa ujumla wake wenzetu ambao wanashughulikia masuala ya kikokotoo, kwanza kabisa kikokotoo cha kabla ya mwaka 2014 kilikuwa ni kikokotoo kizuri sana na kikokotoo ambacho Watanzania wengi ndio wanakitaka kwa sababu chenyewe kilikuwa kimechukua asilimia 50. Kilikuwa kimetaja kwamba miaka ya kuishi baada ya kustaafu ni miaka 15.5.

“Pia, kilikuwa kimechukua mshahara wa mwisho wa mfanyakazi, kwa kawaida ni mshahara mkubwa. Lakini, kikokotoo cha sasa chenyewe kwanza kimepunguza, ukiangalia inayotumika pale ni moja chini ya 540, chenyewe (kipya) kimefanya moja chini ya 580 wakijua kwamba ‘manometer’ ikiwa kubwa itakwenda kupunguza jawabu kule mwisho.

“Lakini, bado pia wamechukua ‘range’ ya miaka 10, halafu wakasema wanatafuta miaka mitatu iliyo bora, kama mshahara wako ni milioni 2.5 (Sh2.5 milioni), na ulikuwa na mwingine laki mbili (Sh200,000) na mwingine laki tano (Sh500,000), lazima mshahara wako utapungua na utaathiri pia mafao yako, lakini pia wamepunguza miaka ya mtu kuishi, kwa sababu wanajua wanachowalipa ni kidogo wameona hata ile miaka 15.5 hawawezi kufika, kwa hiyo wameishusha sasa wameipeleka miaka 12.5, kitu ambacho siyo sawa,” amesema Gambo.

Gambo pia amesema amechukua sampo ya mishahara na amefanya hesabu ya mafao anayopata mstaafu kwa kikokotoo kipya na kile cha zamani.

“Kwa mfano, mfanyakazi ambaye anastaafu akiwa na wastani wa mshahara wa laki nane kwa kikokotoo cha kabla ya Julai 2014 wale waliokuwa kwenye mifuko ya LAPF (Mfuko wa Jamii wa Serikali za Mitaa- LAPF) na PSPF (Mfuko wa mafao ya kustaafu wa umma –PSPF) alikuwa anapata Sh57 milioni, kwa kikokotoo cha sasa atapata Sh28 milioni,  tofauti yake ni Sh29 milioni.

“Lakini kwa mwezi atakuwa anapata Sh401,000 kwa kikokotoo cha zamani na cha sasa atakuwa anatapa Sh388,137. Mtu ambaye mshahara wake ni Sh1.5 milioni kwa kikokotoo cha kabla Julai 2014 alikuwa anapata Sh108 milioni, kwa kikokotoo cha sasa anapata Sh53 milioni,  tofauti yake ni Sh54 milioni.

“Kwa yule ambaye mshahara wake kwenye kiwango cha wakurugenzi, labda Sh3 milioni kwa kikokotoo cha kabla ya Julai 2014 angepata Sh266 milioni kwa kikokotoo cha sasa angepata Sh133 milioni ambayo anakuwa amepunjwa Sh135 milioni,” amesema Gambo.

Hoja ya Gambo

Mbunge huyo ameliambia Bunge kwamba yamefanyika makosa kwenye sheria mpya ya kikokotoo ambacho kwa maoni yake kilitakiwa kuwagusa watumishi wapya na si wale ambao sheria imewakuta.

“Kwanza yamefanyika makosa makubwa sana, mimi nafahamu sheria yoyote inavyotungwa huwa kuanzia pale ilipotungwa. Kwa hiyo mfanyakazi yeyote ambaye sheria hii imemkuta kwa maoni yangu alitakiwa alipwe kwa sheria ya zamani, maana mimi nimeajiriwa leo nafahamu kwamba nikistaafu nimeshakokotoa fomula yangu ni hii nitalipwa kiasi fulani.

“Tunakuja hapa 2018 tunaweka mambo yetu, tumekwenda 2022 tumebadilisha kabisa kikokotoo chenyewe tumeenda kumuathiri mfanyakazi ambaye sheria iliyotungwa 2022 imemkuta, kitu ambacho mimi nadhani si sawa,” amesema.

Gambo amesema kama kuna ulazima sasa kikokotoo kipya kingeanza kwa wale waajiriwa wapya ambao wataajiriwa mara baada ya sheria kusainiwa kwa sababu baada ya hapo miaka itakuwa mingi, kutakuwa na muda pia wa kuendelea kujadiliana na kushauriana huko mbele ya safari.

“Kwa nini tumefika hapa, tumefika kwa sababu moja ya waliosababisha  changamoto hii kwa watumishi ni Serikali yenyewe, tumesikia ripoti za CAG (Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali) mara nyingi hapa, wametueleza namna ambavyo kumekuwa na madeni mengi ambayo Serikali inatakiwa ilipe, lakini Serikali imeshindwa kulipa.

“Tumeelezwa hapa kumekuwa na changamoto kubwa sana, kumekuwa na uwekezaji usiokuwa na tija na mifano iko mingi, kuna mradi uliowekwa lakini hakuna tija.

“Tumeelezwa pia hapa kulikuwa na changamoto kubwa ya gharama za uendeshaji, mifuko ilikuwa mitano, kila mfuko una bodi yake una uendeshaji wake na maofisi yake, kwa hiyo unagundua kwamba kuyumba kwa mfuko siyo tu kikokotoo, sababu yake kubwa ni namna ambavyo tumekuwa tunaisimamia na kuiendesha mifuko siku za nyuma.

“Changamoto ninayoiona mimi badala ya Serikali itafute namna ya kurekebisha changamoto zilizopo, badala yake sasa wanakwenda kumuadhibu mtumishi ambaye yeye ni mwathirika wa yanayofanyika,” amesema.

Mbunge huyo pia ameshauri Serikali irejeshe fedha zote ambazo imezichukua kwenye mifuko ili kuirudishia uhai mifuko yetu ya hifadhi za jamii, itenge bajeti ya kulipa ili ipeleke amani kwa watumishi.

“Ushauri wangu wa tatu, kanuni mpya kikokotoo kama nilivyosema ni vizuri sasa isiwaadhibu wale ambao wameikuta hii sheria, kama inataka kuanza basi ianze pale ilipotungwa ili watumishi wa zamani wasipewe changamoto kubwa zaidi. Tunaona Serikali wamehangaika kwa muda mrefu sana kuhusiana na suala hili. Bunge liunde kamati maalumu, kamati ndogo kwa ajili  ya kwenda kulifanyika kazi jambo hili,” amesema.

Wakati Gambo akiendelea kuchangia, Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Patrobas Katambi aliomba kumpa taarifa.

Katambi amesema si kweli kwamba Serikali inawapa mzigo au inawaumiza wananchi. “Katika mchango wake ni vizuri pia akumbuke na aweze  kuelezea kama amelisoma vizuri jambo hili, aelezee masilahi wanayopata wale ambao katika mifuko awali walikuwa wanapewa mafao bila hata kuchangia shilingi moja kwenye Serikali na Serikali ikawa inalipia, lakini baada ya mabadiliko ya sheria hata wale ambao hawakuwahi kuchangia ilibidi Serikali ibebe mzigo huo kutengeneza nafuu kwao.

“Kwa hiyo nilikuwa natamani tutoe ule usawa wa kutokuonea katika maelezo, tuangalie pia wangapi waliopata nafuu. Kuna zaidi ya asilimia 81 ya wachangiaji ambao wanaenda kupata nafuu kulingana na hali ilivyokuwa awali kwenye hali ya mifuko,” amesema Katambi.

Hata hivyo, Gambo amesema hawezi kuipokea taarifa hiyo.

“Kwanza niwe wazi taarifa yake siipokei na Naibu Waziri ni miongoni mwa watu ambao nawaheshimu sana.

“Tunatetea hapa wananchi, nimshauri tu kwamba kwa sababu wanafahamu kikokotoo hiki hakitugusi sisi kama wabunge, nimuombe tuungane ili tuweze kupata ‘sapoti’ kuwasemea wananchi wenzetu,’ amesema.

Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Nkenge, Florent Kyombo amesema anawaunga mkono walitoa hoja kuhusu kikokotoo na kuitaka Serikali iwe sikivu. Amemtaka waziri mkuu ofisi yake itazame upya na kwenda kuwasikiliza wafanyakazi.

 “Wafanyakazi wanasononeka kila unayekutana naye salamu atakayokuanzishia ni hiyo ya kikokotoo na Serikali ni sikivu, sisi Bunge ni sikivu, tusichongeane hali ya kuwa na kutokuwa na imani na sura nzuri na watumishi wetu.

“Jambo hili linazungumzika Waziri Mkuu. Mheshimiwa Waziri Mkuu watumishi wote wako chini yako, sisi tuko chini yako tutazame jambo hili upya kama Serikali, tuwe na nia ya staha, tuanzishe jukwaa la kuzungumza na vyama vyao, tuje na sisi tujadili bungeni, hata tukienda kwenye kijiji hakuna mzee wa miaka 70, wazee wote wa miaka 70, 80 wamesharudisha namba (wameshafariki dunia). sisi huko tunakokwenda tunaenda na lawama kwa sababu wao wanalalamika,”  amesema.

Kyombo pia ametaka pensheni ya kila mwezi ya wastaafu iongezwe na hasa kwa wale wenye mishahara midogo, kiasi cha kushindwa hata kukata bima ya afya.

“Serikali itazame upya viwango tunavyolipa iviongoze walau na wao waweze kumudu maisha yao na kuweza kuhudumiwa na Taifa hili kwa jinsi ambavyo hali ya maisha yao inazidi kuwa mbaya. Kadiri ya umri unavyokwenda wanapata majanga mengi, majanga ya afya na majanga ya kupoteza nguvu kazi,” amesema.