Wastaafu wanavyoibua maumivu ya kikokotoo kwa mbunge

Muktasari:

  • Aitaka Serikali ilipe madeni ya mifuko ya jamii na kurekebisha kikokotoo cha malipo ya wastaafu.

Dodoma. Mbunge wa Viti Maalumu, Ester Bulaya amegeuka mbogo bungeni akitaka Serikali ya Tanzania ilipe madeni ya mifuko ya jamii na pia kikokotoo ni maumivu kwa wastaafu.

 Bulaya amesema hayo leo Alhamisi Aprili 4, 2024 wakati akichangia hotuba ya Ofisi ya Waziri Mkuu ya mapitio na mwelekeo wa kazi za Serikali na makadirio ya mapato na matumizi ya fedha ya Ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Bunge kwa mwaka 2024/2025.

“Tunajua adha wanayopata wastaafu wetu, sote tunajua kikokotoo, bado ni janga  na hii haijaisha mpaka iishe, ilianza kulalamikiwa tangu sheria inatungwa, hitaji lao lilikuwa wachukue asilimie 50 ya mafao kwa mkupuo, mkaleta asilimia 33 ndio yawe mafao ya mkupuo, bado kuna manung’uniko ya watumishi,” amesema Bulaya.

Bulaya amesema hoja yake anajielekeza kwenye mfuko mmoja wa watumishi wa umma wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF), kwa kuwa amekuwa akitumiwa meseji na wastaafu wengi.

“Nashukuru kupata nafasi hii na kaimu Waziri Mkuu anasikilize vizuri (Kaimu Waziri Mkuu leo ni Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu).

“Nikiwanonyesha meseji zangu za maaskari, za walimu, za manesi, za madaktari. Shida mtu anastaafu anapewa milioni 17 hajajenga, tunajua mtumishi wa umma anafanya kazi kwenye mazingira gani?” amehoji Bulaya.

“Kuteleza si kuanguka, turudi tukae, tuwasikilize, hizi ni pesa zao Serikali inaweka, wapeni mafao kwa mkupuko kwa asilimia 50, hiyo nyingine muwape kidogo kidogo.

“Yale mafao ya mkupuo ndiyo yanayowasaidia, si hiki ambacho mnawapa kila mwezi, wakiweka misingi haya mengine yatakuwa ya kawaida,” amesema Bulaya.

Bulaya amesema walionyesha hofu tangu inabadilishwa sheria ya kikokotoo, lakini Serikali ilikuja na hoja kwamba sheria hiyo inabadilishwa, ili kuwe na manufaa.

“Lakini tulikuwa tunajua, mlikuwa mnajua mifuko inakufa na hamkufanya tathimini mkaenda mkaunda huko huko madhara yake ndio hayo.

“Kwa mujibu wa sheria ya mifuko ya hifadhi ya jamii, ukwasi unatakiwa uwe asilimia 40. Kila ripoti ya CAG (Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali) ya kila mwaka inaonyesha ukwasi asilimia 20 kwa sababu gani, Serikali mnachukua hela kwenye mifuko mnaenda kuwekeza hamlipi.

“Wakati mnapitisha bajeti hapa 2020/2021 mlisema mlilipa kwa ‘non cash bond’ (dhamana isiyo ya pesa) Sh2.1 trilioni, mkasema mwaka ujao wa fedha mnalipa Sh2.4 trilioni mpaka leo hamjalipa, sasa hii mifuko itawezaje kuwa ‘stable’ (imara)?” amehoji.

Bulaya ambaye alikuwa akichangia kwa hisia (kwa namna alivyokuwa akizungumza) ametoa mfano wa takwimu za Juni 2020 kuhusu michango ya wanachama kwenye mfuko ambayo ilikuwa ni Sh1.364 bilioni, mahitaji ya mafao ilikuwa Sh1.554 bilioni, nyongeza waliokwenda kuchukua kwenye vyanzo vingine ilikuwa Sh190 bilioni.

“Sasa kwenye hiyo nyongeza, umeenda kuchukua kwenye ‘investment income’ yao ambayo kwa mwaka huo ilikuwa milioni 400 (Sh400 milioni) ‘can you imagine’ (hebu fikiria) wakipunguza hapa unabaki na nini, yaani hapa wamekusanya kwenye ‘investment’ zao kwa mwaka PSSSF milioni 400 (Sh400 milioni).

“Nakuja mwaka unaoishia Juni 2022 michango ya wanachama bilioni 1.526 (Sh1.526 bilioni), mahitaji ya mafao bilioni 1.697 (Sh1.697 bilioni), pungufu waliokwenda kuongeza ni milioni 171 (Sh171 milioni) kwa mwaka huo ukiangalia ‘investment return’ yao ni milioni 587 (Sh587 milioni), sasa wakitoa hapa wanabaki na nini.

“Mfuko ambao Serikali inakwenda kukopa haliwalipi, inaenda kuwekeza katika maeneo mbalimbali, hairudishi pesa, nilikuwa naangalia ukusara wa 28 wa bajeti, Waziri Mkuu (Kassim Majaliwa) kaongelea vizuri tu, hatukatai kuwekeza kwenye huko Mkulazi ambako wamezalisha sukari.

“Wamewekeza asilimia 96, lakini kwa miaka minne wamepata hasara bilioni 11 (Sh11 bilioni), hawa watu ambao ‘investment income’ yao ni milioni 500 (Sh500 milioni).

Bulaya pia amezungumzia uwekezaji kwenye kiwanda cha ngozi kwamba wamewekeza mtaji asilimia 86, lakini wamepata hasara kwa miaka minne mfululizo (Sh4.5 bilioni).

“Sasa mnachukaje hela za wanachama mnakwenda kupeleka sehemu ambayo mnapata hasara inaonekana mlikuwa hamjafanya tathimini ya kina kuhusiana na ‘investment’ kwenye eneo hilo.

“Wastaafu hizi pesa ni zao, hatukatai kuchukua kuwekeza, lipeni basi madeni, tuone basi hata kwenye ‘mshiko’ wao kwa mwaka unaeleweka sasa mnakomba mabilioni na wenyewe wanabakiwa na milioni 500 (Sh500 milioni), hata wakitaka kulipa wastaafu ni shida,” amesema Buaya.

Kikokotoo

Kikokotoo hicho ni matokeo ya makubaliano ya pamoja kati ya Serikali, Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (Tucta) na Chama cha Waajiri Tanzania (ATE) na kilianza kutumika Julai mosi, 2022.

Hata hivyo, baadaye Tucta ilipinga kanuni mpya ya kukokotoa mafao ya wastaafu kwa kuwa inakandamiza wafanyakazi na kusema pendekezo la wafanyakazi lilikuwa ni kuunganishwa kwa mifuko ya hifadhi ya jamii na si kanuni mpya ya vikokotoo inayolalamikiwa.

Baada ya kutangazwa kanuni hiyo mpya, Rais wa Tucta, Tumaini Nyamhokya alizungumza na waandishi wa habari akisema kanuni hizo ni kandamizi na zimepokewa na wafanyakazi kwa mtizamo hasi na zitashusha ari yao na ufanisi.

“Kuunganishwa kwa mifuko ni hoja ya Tucta tangu mwaka 2004, lakini kanuni mpya ni kinyume cha mapendekezo yetu. Sisi tulitaka kanuni zibaki kuwa za mwaka 2017 ambapo kikokotoo ni 1/540 na mkupuo ni asilimia 50, huku wastani wa umri wa kuishi ukiwa ni miaka 15.5,” alisema Nyamhokya.

Alisema hoja ya ufanisi wa mifuko kwa mkupuo wa asilimia 50 hakutakuwa na shida yoyote endapo Serikali italipa madeni yote ya mifuko na mifuko kuacha uwekezaji usio na tija au kuuza kabisa.

Mamlaka ya Usimamizi wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii (SSRA) imewahi kufafanua kuhusu deni hilo ikisema Serikali haijakopa katika mifuko ya hifadhi ya jamii tangu mwaka 2013 kwa sababu tayari ilifikia ukomo ambao ni asilimia 10 kwa mujibu wa mwongozo.

“Kwenye vitabu vya Serikali madeni yake kwa mifuko ya hifadhi ya jamii bado yapo. Serikali haijakana madeni yake tangu kuunganisha mifuko hii na mara ya mwisho ilisema itatoa hati fungani, ili kulipa hayo madeni yake,” alisema mkurugenzi mkuu wa wakati huo wa SSRA, Irene Isaka.