Mbunge apeleka malalamiko bungeni kikokotoo kuwapunja wafanyakazi

Muktasari:

  • Serikali imesema malipo ya mkupuo wa asilimia 33 yana tija kwa wafanyakazi wengi kuliko ilivyokuwa mwanzo.

Dodoma. Sakata la kikokotoo kwa Wastaafu limetua tena bungeni leo Jumanne Novemba 8, 2023 lakini Serikali imesema hali ilivyo sasa kuna faida kubwa kwa wanuifaika.

Mbunge wa Arusha Mjini, Mrisho Gambo ameuliza Serikali ina mpango gani wa kufanya mapitio ya malipo ya mkupuo (Kikokotoo) ya asilimia 33 kwa wafanyakazi.

Katika swali la nyongeza Gambo amesema hali ilivyo sasa imeonekana kuna mapunjo ikilinganishwa na awali lakini kwa sasa mfuko umepunguza mafao kwa asilimia 50.

Kingine amehoji ni umri wa mstaafu kupungua toka miaka 15 na nusu hadi miaka 12 na nusu akataka ifanyike tathmini.

Akijibu maswali hayo kwa pamoja, Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu, Patrobas Katambi amesema tathimini inawaonyesha kwa asilimia za sasa kundi kubwa linapata faida kuliko ilivyokuwa kabla ya kuwekwa asilimia 33.

Naibu Waziri amesema Serikali ilitangaza matumizi ya kanuni mpya ya mafao ya pensheni kuanzia Julai 1, 2022.

"Kanuni hiyo iliandaliwa kwa kushirikisha wadau wote (Serikali, wafanyakazi na waajiri) kwa lengo la kufanya maboresho ya Pensheni ili kuwianisha mafao ya wanachama na kuifanya mifuko kuwa endelevu," amesema Katambi.

Amesema Serikali inatambua umuhimu wa kuboresha mafao ya pensheni ikijumuisha malipo ya mkupuo kwa wafanyakazi ambapo sheria inaitaka Mifuko kufanya tathmini ya kupima uhimilivu kila baada ya miaka mitatu (3) na kutoa ushauri na mapendekezo ikijumuisha maboresho ya mafao ya wanachama na kuifanya mifuko kuwa endelevu.

Katambi amesema mifuko itafanya tathmini kwa hesabu zinazoishia mwezi Juni 2023 na kwamba Serikali itazingatia ushauri wa mtaalamu ambaye atafanya tathimini hiyo ili kuongeza pensheni ya wastaafu ambayo inajumuisha malipo ya mkupuo wa asilimia 33.