Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Moto wateketeza ghalaMwanza, uchunguzi waanza

Muktasari:

  • Hili ni tukio la pili la moto ndani ya mwezi mmoja ambapo la kwanza lilitokea Julai 3, 2026 na kuteketeza maduka zaidi ya 50 katika eneo la Lumumba jijini Mwanza.

Mwanza. Jeshi la Zimamoto na Uokoaji linaendelea na uchunguzi kubaini chanzo cha moto ulioteketeza ghala la kuhifadhia bidhaa katika eneo la Kauma, kando ya Barabara ya Kenyatta jijini Mwanza, huku likikamilisha pia uchunguzi wa moto mwingine uliounguza maduka ya biashara katika Mtaa wa Lumumba mapema mwezi huu.

Kaimu Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Mwanza, Elisa Mugisha akizungumza na Mwananchi leo Jumatano, Julai 22, 2026, amesema moto huo ulizuka jana saa 3:20 usiku na taarifa zake zilitolewa na askari wa jeshi hilo aliyekuwa akipita eneo hilo.

"Tulipokea taarifa za moto uliokuwa ukiwaka katika godown lililopo Barabara ya Kenyatta, mbele ya jengo la NSSF. Taarifa hizo zilitolewa na askari wetu aliyekuwa akipita eneo hilo na kuona moto ukianza," amesema Mugisha.

Amesema vikosi vya zimamoto vilifika kwa haraka, lakini vilikuta moto ukiwa umeenea kwa kiwango kikubwa, hali iliyowalazimu kutumia mbinu maalumu za kuudhibiti kwa kuuzunguka kutoka pande tatu.

"Tulipofika tulikuta moto ni mkubwa sana, hivyo tulilazimika kuuzunguka kwa kutumia mistari mitatu ili kuudhibiti na kuzuia usisambae," amesema.

Kaimu Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Mwanza, Elisa Mugisha akizungumzia moto uliotoke  barabara ya Kenyatta jana.

Kwa mujibu wa Mugisha, mazingira ya eneo hilo yalirahisisha operesheni ya kuzima moto kwa kuwa ghala lilikuwa limeachwa na nafasi pande zote, hivyo vikosi vya zimamoto vilipata urahisi wa kulifikia kutoka kila upande.

Licha ya moto huo kudhibitiwa, amesema uchunguzi wa kubaini chanzo chake umeanza mara moja.

Aidha, amesema ucheleweshaji wa utoaji wa taarifa za matukio ya moto bado ni changamoto inayolikabili jeshi hilo, akibainisha kuwa baadhi ya matukio huripotiwa baada ya moto kuenea.

"Kumekuwa na matukio ya moto mfululizo katikati ya jiji, lakini taarifa zinachelewa kutufikia. Katika tukio hili tulibahatika kupata taarifa mapema kupitia askari wetu aliyekuwa eneo hilo. Tunawahimiza wananchi kupiga simu namba ya dharura 114 mara wanapoona dalili za moto," amesema.

Ameongeza kuwa uchunguzi wa tukio la moto ulioteketeza maduka takribani 50 katika Mtaa wa Lumumba Julai 3, 2026 upo katika hatua za mwisho na matokeo yake yatatangazwa baada ya kukamilika.

Mugisha pia amewataka wananchi kuzingatia kanuni za usalama wa moto, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha michoro ya majengo inapitishwa na wataalamu na majengo yanasajiliwa na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji ili kurahisisha usimamizi wa tahadhari za moto.

Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Wilbrod Mutafungwa amesema moto huo umedhibitiwa bila kusababisha vifo wala majeruhi.

Amesema Jeshi la Polisi lilifika eneo la tukio mapema kwa ajili ya kulinda usalama wa wananchi na mali zao, sambamba na kusimamia mtiririko wa magari ili kurahisisha shughuli za uokoaji.

"Tulihakikisha usimamizi wa magari unafanyika ili kuzuia ajali na kutoa nafasi kwa vikosi vya uokoaji kufanya kazi kwa ufanisi," amesema.

Mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo, Yassin Haji amesema hatua za haraka zilizochukuliwa na Jeshi la Zimamoto zimezuia moto huo kusababisha hasara kubwa zaidi, akieleza kuwa eneo hilo limezungukwa na majengo mengine pamoja na kituo cha mafuta.

"Kama zimamoto wangechelewa kufika, madhara yangekuwa makubwa zaidi kutokana na uwepo wa majengo mengi na kituo cha mafuta jirani," amesema.