Mpambe wa Nyerere aeleza kilichombeba bosi wake

Muktasari:

  • Melkizedeck Temu ambaye alikuwa msaidizi au mpambe (ADC) wa aliyekuwa Rais wa kwanza wa Tanganyika na baadae Tanzania, hayati Julius Nyerere amesema kiongozi huyo alikuwa muumini wa ukweli.

  

Melkizedeck Temu ambaye alikuwa msaidizi au mpambe (ADC) wa aliyekuwa Rais wa kwanza wa Tanganyika na baadae Tanzania, hayati Julius Nyerere amesema kiongozi huyo alikuwa muumini wa ukweli.

Mzee Temu ambaye alikuwa ADC wa Nyerere kwa miaka mitano mara tu baada ya Tanganyika kupata Uhuru wake, anasema Nyerere hakupenda mtu anayejikweza na alichukua ubaguzi wa kikabila na kidini.

Wakati Tanzania ikitimiza miaka 22 tangu kifo cha Baba wa Taifa Julius Nyerere kilichotokea Oktoba 14, 1999 katika hospitali ya Mtakatifu Thomas nchini Ungereza, falsafa na hotuba zake zimeendelea kuishi ndani na nje ya Tanzania.


Watanzania bado wameendelea kuwa wamoja, wanashirikiana na kudumisha Amani mambo aliyokuwa akiyasisitiza Nyerere.

Picha za Mzee Melkizedeck akiwa ADC zinaonekana zaidi katika picha za kukabidhiana hati za Muungano kati ya Nyerere na Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Sheikh Abeid Aman Karume mwaka 1964.

Kwa sasa mzee Melkizedeck anaishi kijijini kwake Marangu jimbo la Vunjo akiwa na mkewe Bathilda Temu mwenye umri wa miaka 76, akijishughulisha na shughuli za kilimo cha ndizi na zao la Kahawa.

Kabla ya kustaafu mwaka 1989, mzee huyo baada ya kumalizana na kazi ya ADC, mwaka 1979 alipelekwa Uganda kulisuka Jeshi la Polisi la nchi hiyo na aliporejea mwaka 1982 alipelekwa Zimbambwe kufanya kazi kama hiyo.

Mwalimu Nyerere niliyemfahamu

Akizungumza na gazeti hili katika mahojiano maalumu nyumbani kwake Marangu, mzee Melkizedeck anasema Nyerere anayemfahamu alikuwa na sifa zaidi ya tano, ukiacha sifa ya kuwa Rais wa kwanza wa Tanganyika.

“Nina miaka 85 sasa karibu nakimbilia 86 sasa. Nyerere alitaka uwe mtu wa ukweli na usiyependa makuu. Alitaka uwe ordinary person (mtu wa kawaida) hakutaka kiongozi anayejikweza,”anasema mzee Melkizedeck.

Mbali na sifa hizo, lakini anasema Nyerere alichukia sana ubaguzi unaotokana na ukabila na udini na alifanikiwa kuyaunganisha makabila yote kupitia lugha ya Kiswahili na leo watu hawatambuani kwa makabila.

“Alikuwa ni mtu mkweli na alikuwa anapendwa na watu. Alikuwa msomi mzuri na mwenye akili. Yeye alikuwa anaipenda Tanzania na muungano wa Afrika Mashariki”anasema mzee huyo na kuongeza kuwa:-

“Alitaka sana kuwe na umoja wa Afrika Mashariki imara lakini malengo yake hayakutimia lakini alikuwa ni mtu mkweli sana. Yapo mengi ambayo Watanzania wamerithi kwake. Alituachia upendo, umoja na mshikamano”

“Kazi zikipatikana alikuwa anawapa watu bila ubaguzi wa jinsia. Hata nilipokuwa Zimbambwe kila nikija likizo nilikuwa siachi kwenda kumsalimia Nyerere iwe Msasani au Butiama”anasema Mzee Melkizedeck.

Ushauri wake kwa Rais Samia

Msaidizi huyo wa zamani wa Nyerere alipoulizwa kama angepata bahati ya kukutana na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan leo, anasema atamwambia mwanamke na mwanaume ni sawa.

“Nikukutana na Rais Samia leo ningemwambia mwanaume na mwanamke akili zao ni sawa ni umbile tu ambalo linawatofautisha. Hata Nyerere alitambua mwanamke na mwanaume ni sawa sawa,”anasema mzee huyo.

“Huku Afrika kuna watu hawawathamini sana wanawake jambo ambalo ni baya. mwanamke ni mtu. Naona hata Rais Samia amekuwa akilisema hili sana. Tuthamini binadamu sio kwa jinsia”.

Alipoulizwa kuhusu kama Rais Samia atapitishwa na CCM mwaka 2025 kupeperusha bendera ya CCM, mzee huyo anasema “Nafikiri tusimnyime 2025 tumuache amalize miaka yake 10. Huu ni utamaduni upo”

“Ile itatuletea sifa na msimamo wa nchi yetu kwamba wanaume na wanawake tumehitilafiana kwa maumbile vinginevyo akili zetu ni sawa,” anasema mzee Melkizedeck anayependa utani saa zote.

“Ningetamani Samia (Rais) amalize vipindi viwili kama utamaduni ndani ya chama chao ulivyo. Tena ukimuona kwenye picha ya haya magazeti anavyoongoza baraza la mawaziri ana anatosha kabisa,”anasema.

Septemba 15, 2021, Rais Samia ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM alitoa kauli juu ya mbio za urais 2025 na kusisitiza katika uchaguzi huo wanakwenda kumweka Rais mwanamke bila kufafanua kauli yake hii.

“Nataka niwaambie wanawake bado hatujaweka Rais mwanamke. Rais mwanamke huyu amekaa kwa sababu ya kudra ya Mungu na matakwa ya Katiba,”alisema akizungumza na wanawake siku ya Demokrasia.

“Tulichokichangia sisi na mama zetu na dada zetu akina Anna Abdalah ni kusukuma mpaka mwanamke akawa makamu wa Rais. Ule ndio mchango mkubwa tumeufanya wanawake,”alisema na kuongeza kusema;-

“Lakini kufika hapa kama isingekuwa kudra za Mungu ingekuwa ngumu. Sasa ndugu zangu Rais mwanamke tutamweka 2025.Tukishikamana, tukimweka Rais wetu tutakutana hapa kwa furaha kubwa sana”

“Wameanza kutuchokoza kuandika kwenye vigazeti kuwa Samia hatogombea nani kawaambia. Fadhila za Mungu zikija mikononi mwako usiziachie. Hizi ni fadhila za Mungu,”alisisitiza Rais Samia siku hiyo.

Mzee Mekizedeck ni nani

Mzee Melkizedeck alizaliwa Mei 19, 1936 huko Marangu mkoani Kilimanjaro na alisoma shule za msingi za Ashira, Marangu na Kirua na baadae sekondari za Old Moshi na Tabora na baadae Chuo cha Makerere, Uganda.

Mwaka 1960 alijiunga na Jeshi la Polisi la Tanganyika lililokuwa chini ya wakoloni akiwa na cheo cha Cadet Assistant Superintendent na baada ya mafunzo ya kipolisi huko Uingereza, alirejea nchini kuendelea na kazi.

Baada ya Tanganyika kupata Uhuru wake, alihudumu kama Aide-de-Camp (ADC) wa Nyerere na baadae alishika nyadhifa mbalimbali ambapo aliweza kupelekwa Uganda na Zimbabwe kama mkuu wa Polisi wa nchi hizo.

Mwaka 1979 baada ya Vita ya Uganda, mzee Melkizedeck aliingizwa Jeshi la Wananchi wa Tanzania na kupewa cheo cha Luteni Kanali.