Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mradi wa njia ya umeme Kilovolti 400 Chalinze –Dodoma wafikia Asilimia 94

Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano na Huduma kwa Wateja wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), Irene Gowelle akizungumza leo Julai 28, 2026 mara baada ya kitembelea mradi wa kusafirisha umeme wa msongo wa kilovolti 400 kutoka Chalinze kwenda Dodoma uliofikia asilimia 94.

Muktasari:

  • Baadhi ya maeneo nchini yatakumbwa na katakata ya umeme ikilenga kukamilisha kazi ya mradi kwa usalama zaidi.

Pwani. Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) limetangaza kuwa mradi wa njia ya kusafirisha umeme wa msongo wa Kilovolti 400 kutoka Chalinze hadi Dodoma, umefikia asilimia 94 ya utekelezaji na unatarajiwa kukamilika ifikapo Agosti 21, 2026.

Kutokana na hatua za mwisho za ujenzi huo, shirika hilo limesema kutakuwa na katizo la muda la umeme katika baadhi ya maeneo nchini ili kuwezesha kukamilika kwa kazi za mradi huo kwa usalama.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumanne Julai 28, 2026, Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano na Huduma kwa Wateja wa Tanesco, Irene Gowelle amesema katizo hilo litafanyika kwa awamu mbili.

Amesema awamu ya kwanza itaanza Julai 30 hadi Agosti 4, 2026, na awamu ya pili kuanzia Agosti 11 hadi 17, 2026.

Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano na Huduma kwa Wateja wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), Irene Gowelle akizungumza leo Julai 28, 2026 mara baada ya kitembelea mradi wa kusafirisha umeme wa msongo wa kilovolti 400 kutoka Chalinze kwenda Dodoma uliofikia asilimia 94.

Gowelle amesema hatua hiyo inatekelezwa kufuatia ombi la mkandarasi wa mradi huo, kampuni ya TBEA, ili kuruhusu kazi za mwisho za ujenzi kufanyika katika mazingira salama.

"Mradi huu umefikia hatua muhimu sana ya utekelezaji ambapo baadhi ya njia za kusafirisha umeme za kilovolti 220 na 132 zitalazimika kuzimwa kwa muda ili kuruhusu kazi za kuvuta na kuunganisha nyaya mpya kufanyika kwa usalama. Hii ni hatua ya kawaida katika utekelezaji wa miradi mikubwa ya miundombinu ya kusafirisha umeme na inalenga kukamilisha mradi huu wenye manufaa makubwa kwa Taifa," amesema Gowelle.

Amefafanua kuwa baadhi ya maeneo katika Kanda ya Kati, Kanda ya Ziwa, Kanda ya Kaskazini, Kanda ya Magharibi na Kanda ya Kusini Magharibi yataathirika kwa nyakati tofauti kulingana na ratiba ya utekelezaji wa kazi hizo.

Aidha, amesema Tanesco itaendelea kutoa taarifa kwa wananchi kupitia vyombo vya habari, mitandao ya kijamii na majukwaa mengine ya mawasiliano ili kuwawezesha wateja kupanga matumizi yao ya umeme kwa kuzingatia ratiba zitakazotolewa.

Amesisitiza kuwa nchi ina umeme wa kutosha na kwamba, katizo hilo ni la muda, likiwa sehemu ya kukamilisha mradi wa kimkakati unaolenga kuimarisha uwezo wa mfumo wa usafirishaji wa umeme nchini.

Gowelle amesema mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Lindi na Mtwara haitahusika katika ratiba hiyo ya katizo.

Kwa upande wake, Meneja wa Mradi wa Njia ya Kusafirisha Umeme wa Kilovolti 400 Chalinze–Dodoma, Mhandisi Newton Mwakifwamba amesema mradi huo una urefu wa kilomita 345 na unagharimu takribani Sh514 bilioni, huku ukifadhiliwa kwa asilimia 100 na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Amesema mradi unahusisha ujenzi wa njia mpya ya kusafirisha umeme pamoja na upanuzi wa vituo vya kupokea na kusambaza umeme vya Chalinze na Dodoma.

"Katika hatua hizi za mwisho, tutafanya kazi za kuvusha na kuunganisha njia mpya ya umeme katika maeneo ya Mkambarani, Kikombo na Mkonze. Hatua hizi ni muhimu ili kuhakikisha mradi unaanza kufanya kazi kwa ufanisi na usalama," amesema Mwakifwamba.

Amesema kukamilika kwa mradi huo kutaimarisha uwezo wa mfumo wa taifa wa usafirishaji wa umeme na kuwezesha usafirishaji wa umeme unaozalishwa katika Bwawa la Kufua Umeme la Julius Nyerere kwenda maeneo mbalimbali nchini.

Kwa mujibu wa Tanesco, mradi huo unatarajiwa kuongeza uhakika wa upatikanaji wa umeme, kuboresha uthabiti wa gridi ya taifa na kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii kupitia huduma bora ya nishati.